Wednesday, December 12, 2018

MTALAAM BoT AFAFANUA UKUAJI WA UCHUMI



Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

UKUAJI wa uchumi wa Taifa kutojionesha katika  kuongezeka kwa kipato cha kila mwananchi ni jambo la kawaida ambalo halimaanishi kuwa takwimu za ukuaji huo wa uchumi ni za kupikwa.

Hayo yameelezwa kwa Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Suleiman Missango alipokuwa akitoa mada katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara
inayoendelea jijini Dodoma.

Akifafanua Dk Missango alisema kuwa takwimu za ukuaji wa uchumi zinatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa jumla katika taifa ambapo mapato yake yanatofautiana katika kumwendea kila mmoja kutegemeana na shughuli za uzalishaji.Akitoa mfano kuhusiana na suala hilo, alisema kuwa shughuli za uzalishaji za jamii moja zinaweza kuwa zimeongezeka kwa kuhesabu wastani wa ongezeko la uzalishaji, lakini haina maana kuwa kila mwanajamii atakuwa ameona ongezeko katika kipato chake, kutokana
na shughuli za kiuchumi alizonazo.

Katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko miongoni mwa wananchi wakihoji takwimu za ukuaji wa uchumi zinazoonekana kuimarika ilhali wananchi wengi wamekuwa hawana pesa. Uchumi wa Tanzania unakaridiwa kukua kwa kasi ya asilimia 7 kwa mwaka.Dk Missango alisema kuwa hali ya baadhi ya wananchi kupungukiwa fedha mifukoni inatokana na kupunguza matumizi yao ya kawaida na kuyaelekezwa katika matumizi ya maendeleo, ambapo athari za kushuka chini (trickledown effect) hupungua.

“Kwa mfano kama fedha za sherehe za uhuru zingetumika kwa shughuli hiyo, kungekuwa na watu ambao wangepta fedha na kuzitumia kwenye jamii kwa matumizi mbalimbali, lakini zinapoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, kuna maumivu yanayoonekana lakini kuna kuwa na manufaa mbeleni…huwezi kwenda mbinguni bila kwanza kufa,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalendo Tanzania (CHAWATA) Eliud  alisema kuwa takwimu za ukuaji uchumi zinawezak ueleweka kuwa nitambo za kisiasa kwa kuwa Hakuna uchimu usioleta manufaa kwa wananchi wake.“Wataalam wetu wanatueleza namba wakati hali ya mwananchi wa kawaida inazidi kuwa mbaya. Uchumi unaokua unapaswa kujiakisi kwenye maisha ya watu kuwa bora zaidi,” alisema.

Hata hivyo, Dr Missango alisema kuwa ni wajibu wa Serikali kutengeneza sera zinazowezesha kuleta manufaa kwka wananchi, hasa wa kipato cha chini kutokana na kukua kwa uchumi.Alisema dhana na ‘robbing Peter to pay Paul’ hutumiaka na serikali zote duniani kwa kutoza kodi mbalimbali ambnapo mwenye kipato zaidi hulipa kodi zaidi na fedha hizo kwenda kwenye huduma za jamii.

“Mambo haya unaweza kusiyaone moja kwa moja lakini kunapo kuwa na barabara nzuri zaidi, hospitali zenye dawa na kadhalika, hii ndio dalili ya ukuaji uchumi ambapo sio lazima ujieneshe kwenye kutuna
kwa mifuko,” alisema.

 Mkurugenzi wa Sera za Uchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Suleiman Misango akifafanua kuhusu hali ya uchumi kwenye mafunzo ya waandishi wa habari za uchumi na biashara mjini Dodoma
Meneja wa Idara ya Itifaki na Uhusiano wa Umma wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Zaria Mbeo (kushoto), akijadiliana jambo na wakurugenzi wa Idara ya uchumi wa BoT, Tawi la Dodoma
 Mwenyekiti wa mafunzo ya waandishi wa habari za uchumi na fedha, Nurdin Selemani kutoka Azam Media, akijadiliana jambo na mtunza muda wa mafunzo hayo, Bakari Kimwanga kutoka Gazeti la Mtanzania Bakari Kimwanga (aliyekaa)
 Baadhi ya maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) wakifuatilia mjadala wakati wa semina ya waandishi wa habari za uchumi na fedha inayoendelea mjini Dodoma

No comments: