Kutoka kushoto, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephraim Mushi, Msaidizi wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mhandisi Noel Baraka wakipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Migodi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Madini ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Aidan Mhando kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo Wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Afisa Tarafa wa Ziwani, Fransis Mkuti (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo Wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akichimba mchanga pamoja na wachimbaji wa madini ya mchanga kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo Wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akikagua madini ya chumvi katika ghala la kuhifadhi madini hayo kwenye shamba la chumvi linalomilikiwa na Jeshi la Magereza la Kiwanda Chumvi lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wazalishaji wa madini ya chumvi kutoka katika Chama cha Wazalishaji wa Madini katika Mkoa wa Mtwara (MTWAREMA) mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara.
Na Greyson Mwase, Mtwara
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amezitaka halmashauri zote nchini kutokutoza kodi zilizofutwa kwenye madini ya chumvi ili wazalishaji wa madini hayo waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri na kulipa kodi stahiki serikalini.
Naibu Waziri Nyongo ameyasema hayo leo Desemba 12, 2018 kwenye mkutano wake na wazalishaji wa madini ya chumvi kutoka katika Chama cha Wazalishaji wa Madini katika Mkoa wa Mtwara (MTWAREMA) kilichofanyika kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara mjini Mtwara ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini iliamua kufuta baadhi ya kodi walizokuwa wanatozwa wazalishaji wa madini ya chumvi ambazo zilikuwa ni mzigo kwao na kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea. “Ninaziagiza halmashauri zote nchini kutoza kodi kwa kuzingatia sheria zilizopo huku zikihakikisha kodi zilizofutwa kisheria hazitozwi tena.” Alisema Naibu Waziri Nyongo.
Akielezea mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kuwasaidia wazalishaji wa madini ya chumvi katika mkoa wa Mtwara, Naibu Waziri Nyongo alieleza kuwa ni pamoja na kuangalia namna ya uanzishwaji wa kiwanda cha chumvi katika mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuongeza ubora na thamani ya madini ya chumvi.
Katika hatua nyingine akizungumza na kikundi cha Umoja wa Vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini ya mchanga katika eneo la Ziwani lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara, mbali na kupongeza kikundi hicho kwa kazi nzuri Naibu Waziri Nyongo aliomba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kuendelea kukisaidia kikundi hicho kwa kuwapa mikopo ya fedha ili waweze kuzalisha zaidi.
Aidha, aliwataka wakandarasi wanaopewa zabuni za ujenzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na majengo kununua mchanga na tofali kutoka katika vikundi vya wachimbaji wa mchanga katika mkoa wa Mtwara ambao wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kuwainua kiuchumi. Pia aliagiza Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuwapa ushauri wa kitaalam wachimbaji wa madini ya mchanga ili kufanya uchimbaji uwe wenye tija na kuzingatia sheria na kanuni za madini zilizopo.
Wakati huohuo Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara katika shamba la chumvi linalomilikiwa na jeshi la magereza la Kiwanda Chumvi lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara na kupongeza jeshi hilo kwa kazi nzuri.
No comments:
Post a Comment