MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru kumkamatwa kwa Mwenyekiti Wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge Wa Tarime Mjini, Esther Matiko ili waje kujieleza kwa nini wasifutiwe dhamana zao baada ya kukiuka masharti ya dhamana
Amri hiyo imetolewa leo Novemba 8.2018 na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya Awali (PH).
Akitoa uamuzi huo Hakimu Mashauri amesema, Novemba Mosi mwaka huu, dhamini wa mshtakiwa Mbowe, alifika ifika mahakamani hapo na kudai kuwa, mshtakiwa amepelekwa South afrika kutibiwa akiwa Mahututi na Mahakama iliamuru leo (siku ya kesi) alete taarifa kuhusu kuumwa kwake lakini hajaleta na badala yake amefika na kudai kuwa mshtakiwa yuko Dubai.
"Hii inaonesha kuwa, mdhamini huyu wa mshtakiwa Mbowe siyo muaminifu", amesema hakimu Mashauri.Pia kuhusu Mshtakiwa Matiko Hakimu Mashauri amesema kitendo cha mshtakiwa Matiko kusafiri nje ya nchi bila ridhaa ya Mahakama wala Polisi wanapotakiwa kuripoti kama masharti ya dhamana yanavyowataka ni matumizi mabaya ya haki yake ya dhamana.
Kutokana na sababu hizo mahakama inaamuru mshtakiwa Mbowe na Matiko wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo ili kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana zao" amesema Mashauri. Awali kabla ya amri hiyo Wakili Nchimbi, alihoji kwanini Mbowe na Matiko hawapo mahakamani.
Mdhamini wa Mbowe alisimama na kueieleza mahakama kwamba Mbowe yupo Dubai kwa ajili ya matibabu na hajawahi kusema kwamba yupo Afrika Kusini."Nimeongea naye moja kwa moja yupo nchini Dubai,"ameeleza.
Naye mdhamini wa Matiko alisimama na kuieleza mahakama kwamba Matiko amepata ziara ya Kibunge na yuko nchini Burundi, ambapo anawasilisha vielelezo ikiwemo tiketi ya ndege.
Aidha wakili anayemtetea Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Jamuhuri Johnson amejitoa kumtetea mshtakiwa akidai, kwa miaka 20 aliyofanya kazi mahakamani hajawahi kuona mwenendo wa Kesi kama huo."Niombe mie nijitoe, Mimi mwenyewe nisipoteze muda wa Mahakama na alipomaliza ilikuwa saa 7 : 24 mchana akaondoka zake.
Hiyo ni mara ya pili kwa mawakili wanaomtetea mshtakiwa Msigwa Kujitoa. Awali, Agosti 23 mwaka huu Wakili Jeremiah Mtobesya alijitoa kumtetea Msigwa.Hatua hiyo ya wakili Jamuhuri kujitoa ilikuja kufuatia wakili wa serikali Mkuu Faraja Nchimbi kuiharifu Mahakama kuwa washtakiwa saba wapo mahakamani lla washtakiwa wiwili Mbunge Wa Tarime mjini, Esther Matiko na Mbowe hawapo.
Pia Wakili John Malya aliiarifu mahakama kuwa yupo kwa ajili ya kumshikia wakili Peter Kibatala ambaye anaumwa.Baada ya kueleza hayo, Wakili Nchimbi aliiambia Mahakama Kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa PH na akaomba iendelee kusikiliza chini yakifungu cha 226 (1) cha sheriaya makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 hata kama washtakiwa hao hawapo.
Hata hivyo, wakili Johnson kabla ya kujitoa aliiambia Mahakama kuwa kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa na kwa upande Wa washtakiwa Mbowe na Matiko wapo wadhamini wao.Pia kufuatia taarifa za wadhamini, Wakili Johnson kabla ya kujitoa aliiomba Mahakama isiruhusu upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa hayo PH hadi washtakiwa ambao hawapo wawepo na Wakili Kibatala pia ambaye anaumwa.
Haya hivyo, Hakimu Mashauri alikubaliana na upande Wa mashtaka na kuruhusu washtakiwa wasomewe Maelezo ya awali kwa sababu kinachofanyika hakiwezi kuathili kitu
Wakili Nchimbi aliwakumbusha washtakiwa hao mashtaka 13 yanayowakabili kwa kuwasomea yakiwamo ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali, wenye vurugu na uchochezi Wa uasi ambapo mshtakiwa Msigwa kwa kuwa alikuwa na Wakili Johnson alikanusha huku wenzake Mwalimu, Mnyika, Mdee,Heche,Mashinji na Bulaya waliieleza Mahakama kuwa hawawezi kujibu wala kuongea chochote bila ya kuwepo Wakili wapo.
Baada ya washtakiwa hao kueleza hayo, Hakimu Mashauri alisema kuwa Msigwa amekataa mashtaka hayo moja kwa moja lakini washtakiwa wengine waliobaki walitaka uwepo Wa Wakili wapo hivyo yeye kwa mujibu Wa kifungu cha 228 cha sheria ya Makosa ya Jinai aliandika kuwa wamekataa.
Wakili wa Serikali, Zainabu Mwango alidai kuwa Februari, mwaka huu kulikuwa na uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni ambapo vyama 12 vilishiriki ikiwemo Chadema.
Alidai vyama vyote vilipaswa kuheshimu na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi za nchi kwani zimetoa taratibu za kufuatwa katika shughuli za uchaguzi na kampeni zilitakiwa kuisha Februari 16, mwaka huu na Februari 17,mwaka huu ilikuwa tarehe ya uchaguzi.
Alidai washitakiwa wote tisa na wengine 12 ambapo hawako mahakamani walikula njama kushawishi wananchi kufanya mkusanyiko usio halali, kuinua hisia za chuki kwa watanzania na kuleta chuki na dharau dhidi ya utawala halali wa serikali halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo baada ya kusomewa Maelezo hayo, washtakiwa waligoma kujibu na kudai kuwa hawaelewi kitu wanaomba uwakilishi wa wakili wao
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 12 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment