*Dola za Marekani milioni 100 kutumika katika ujenzi
*Ahimiza Watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MWENYEKITI
wa Makampuni ya Kiluwa Group Ltd Mohammed Kiluwa amesema katika
kuhakikisha anaunga mkono jitihada za Rais Dk.John Magufuli za ujenzi wa
Tanzania ya viwanda amefanikiwa kuwashawishi wawekezaji kutoka nchini
China kuja kujenga viwanda kuwekeza nchini.
Kiluwa amesema
kupitia ushawishi wake na kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji
Tanzania(TIC) wawekezaji hao kutoka China wamekubali kujenga kiwanda cha
kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi, Kiwanda cha Saa pamoja na Kiwanda
cha Simu na kwamba awamu ya kwanza ya uwekezaji huo jumla ya dola za
Marekani milioni 100 zitatumika.
Akizungumza leo jijini Dar es
Salaam kuhusu ujio wa wawekezaji hao Kiluwa amesema viwanda hivyo
vitajengwa Mlandizi mkoani Pwani na wakati wowote kuanzia sasa baada ya
kukamilisha taratibu zote ikiwemo za vibali ujenzi wa viwanda hivyo
utaanza mara moja.Pia amesema mbali ya kujengwa kwa viwanda hivyo
wawakezaji hao wameonesha nia ya kujenga kiwanda cha kubangua korosho
mkoani
Mtwara na kinachoendelea sasa ni mazungumzo ambayo
yanakwenda vizuri na hakuna kitakachoshindikana."Wawekezaji hawa
wameonesha nia kujenga kiwanda cha korosho na walikuwa tayari kwenda
mkoani Mtwara kuona mazingira."
Kiluwa amefafanua kwenye
mazungumzo yake na wawekezaji hao aliwagusia kuhusu zao la korosho
nchini na hivyo wamekubali kujenga kiwanda cha korosho.Amezungmzia
umuhimu wa wananchi kuwa na uzalendo kwa nchi yao katika kuhakikisha
wanashiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi na hasa kuelekea
ujenzi waTanzania ya viwanda.
"Tuwe wazalendo kwa nchi yetu kwa
kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Rais Dk.John Magufuli katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara kupitia
viwanda.Ni jukumu letu Watanzania kusimama imara kufanikisha dhamira ya
Rais wetu mpendwa,"amesema Kiluwa na kuongeza kwa kutambua malengo ya
Rais ameamua kushiriki kwa vitendo kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza
nchini.
"Kushawishi wawekezaji ni kazi ngumu lakini naifanya kwa
moyo wangu wote huku nikitanguliza uzalendo kwa taifa langu.Nitoe rai
kwa wanaohusika na utoaji wa vibali kuhakikisha wanatoa kwa wakati ili
wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza waanze shughuli za uwekezaji nchi
kwetu,"amesema Kiluwa na kuongeza kuwa anafurahishwa pia na ushirikiano
uliopo kati yake na TIC.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kukuza
Uwekezaji kutoka TIC John Mnali amesema moja ya mikakati yao ni
kuendelea kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania ambako
kuna mazingira mazuri ya uwekezaji.Pia amefafanua pamoja na kuandaa
mazingira mazuri ya uwekezaji nchini wamekuwa wakisaidia kuhakikisha
wawakezaji wanapata vibali vyote muhimu vinavyotakiwa katika
uwekezaji."Moja ya jukumu letu ni kuwasaidia wawekezaji waweze kupata
vibali kwa haraka ili waendelee na uwekezaji."
Wakati huo huo
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yinengda New Material Techonology
Mayi Hong ambaye amesema wamefurashiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji
ya nchini Tanzania na kutokana na
mazingira mazuri yamewavutia kuwekeza kwa kujenga viwanda hivyo katika eneo la Mlandizi mkoani Pwani.
"Tutajenga
kiwanda cha kuongeza thamani ya ngozi na kisha kutengeneza bidhaa
zitokanazo na ngozi.Pia tutajenga kiwanda cha saa na kiwanda cha
simu.Tumetenga Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya viwanda
hivyo.Pia katika mazungumzo yetu na Kiluwa tumejadiliana kuhusu ujenzi
wa kiwanda cha korosho na tunaamini tutajenga,"amesema Hong.
Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. John Mathew Mnali akizungumza jambo mbele ya waandishi wa Habari leo jijini Dar kuhusu masuala mbalimbali ya uwekezaji wa viwanda,ikiwemo na kuwapokea wageni wa uwekezaji wa viwanda kutoka nchini China na wenyeji wao kutoka kampuni ya Kiluwa Group Ltd.
MWENYEKITI wa Makampuni ya Kiluwa Group Ltd Mohammed Kiluwa (pichani kushoto) akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa habari leo alipokwenda kuwatambulisha Wadau wake wa Uwekezaji katika masuala ya Viwanda kutoka nchini China,kwa kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),na kueleza mikakati yao mbalimbali waliyonayo kuhusiana na uwekezaji wa viwanda nchini Tanzania,kulia ni Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. John Mathew Mnali.
Wawekezaji wa Kampuni ya Yinengda New Material Techonology kutoka nchini China,wakiwa wameambatana na Mkurugenzi wao Mayi Hong wakisikiliza mambo mbalimbali yaliyokuwa yakizungumzwa kwenye mkutano huo,uliofanyika katika kituo cha Uwekezaji (TIC),jijini Dar
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji (TIC),Geofrey Mwambe akisalimia na Mkurugenzi wa kampuni ya Kiluwa Group,Naima Mohamed Kiluwa,walipokwenda kwenye ofisi za kituo hicho kuwatambulisha wadau wao wa uwekezaji katika mambo ya Uwekezaji wa Viwanda,anaeshuhudia pichani kati Mwenyekiti wa Kampuni ya Kiluwa Group,Mohamed Kiluwa (pichani kati) na kuwasilisha mikakati yao mbalimbali ya uwekezaji wa viwanda.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji (TIC),Geofrey Mwambe akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yinengda New Material Techonology Mayi Hong alipokuwa akifafanua jambo kuhusiana na mambo ya uwekezaji wa viwanda hapa nchini Tanzania,maara aada kuzungumza na waandishi wa habara katika ofisi za kituo hicho .
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yinengda New Material Techonology Mayi Hong akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji (TIC),Geofrey Mwambe walipowasili leo kwenda kutambulishwa na Mdau wake Mkubwa kwenye mambo ya Uwekezaji wa Viwanda,Mwenyekiti wa Kampuni ya Kiluwa Group,Mohamed Kiluwa (pichani kati) na kuwasilisha mikakati yao mbalimbali ya uwekezaji wa viwanda.
Wakiwa katika picha ya pamoja
No comments:
Post a Comment