Friday, November 30, 2018

BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA DK.YOUQING


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BALOZI wa China nchini Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Geoffrey Mwambe wamekutana na kufanya kikao cha kazi ambapo wametumia kikao hicho pia kuzungumzia masuala yanayohusu uwekezaji hasa kwa kampuni za kutoka nchini China.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za TIC jijini Dar es Salaam ambapo Mwambe ametoa ufafanuzi pia kuhusu sheria ya kutoa vivutio vya uwekezaji hasa vinavyohusu msamaha wa kodi kwa wawekezaji huku akiendelea kutoa ufafanuzi zaidi kuwa kampuni za Kichina ziache kutumia taarifa za madalali na badala yake wafike TIC kupata taarifa mbalimbali za nchi kuhusu uwekezaji.

"Kituo hakipo hapa kukwamisha mwekezaji, tupo kwa ajili ya kusaidia kuanzisha uwekezaji wake nchini kwa kuwa tunatambua umuhimu wa uwekezaji huo kwa nchi,"amesema Mwambe.Baada ya maelezo hayo Balozi ameridhishwa na amepongeza Serikali kwa kusimamia uwekezaji kwa uwazi na kufuata sheria na China inafurahia jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha mazinga ya biashara na uwekezaji nchini."Mazingira ya biashara na uwekezaji yanaboreshwa na ndiyo sababu kubwa ya makampuni mengi ya China kuendelea kuonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania,"amesema Balozi

Pia Balozi amemtaarifu Mwambe kuwa Desemba 1 mwaka 2018 msafara wa wafanyabiashara wapatao 50 unaojumuisha kampuni 26 kutoka China utafika nchini ikiwa ni mojawapo ya mpango wao wa kutembelea nchi tatu za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda. "Lengo la ziara ya wafanyabiashara hao Afrika Mashariki ni kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali. Hata hivyo kwa kutambua uwepo wa mahusianao mazuri tena ya muda mrefu yaliyopo kati ya Tanzania na China msafara ulikubaliana uanzie Tanzania kabla ya kwenda nchi nyingine. Msafara unaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Kukuza Uhusiano kati ya Nchi zinazoendelea Bw. Lyu Xinhua.


Kampuni zinazokuja nchini zipo katika sekta za viwanda, ujenzi, afya, maji, tehama, fedha, elimu, miundo mbinu, kilimo na biashara ya maduka makubwa,"amesema.Katika kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanznaia (TPSF), Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI),Ubalozi wa China nchini na Ubalozi wa Tanznaia nchini China wanaratibu Kongamano la Biashara na Uwekezaji Kati ya Tanzania na China litakalofanyika Desemba 3,2018 katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.

Balozi amewaomba Watanzania kutumia kongamno hilo kama chombo muhimu cha kutolea taarifa za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka China kwa kuzingatia kwamba wafanyabiashara wanaokuja ni wale wenye nia ya kuwekeza Afrika; na watatembelea pia nchi nyingine kwa madhumuni ya kujionea mazingira na fursa za uwekezaji. Hivyo matarajio ya Balozi ni kwamba Tanzania kama nchi itatumia fursa hiyo kueleza kinagaubaga fursa za uwekezaji na sababu za kuwekeza Tanzania na sio nchi nyingine.

Wakati huo huo Mwambe, amemshukuru Balozi kwa kukitembelea Kituo kwa lengo la kufanya mazungumzo yaliyoweka bayana utayari wa Ubalozi wa China kuisaidia TIC katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kuboresha huduma kwa wawekezaji. Pia imeelezwa kwa wafanyabiashara wenye nia ya kushiriki kongamano kati ya Tanzania na China wanaweza kuwasiliana na Bi. Diana

Ladislaus 0719 653 079 kwa maswali au Bi. Lilian Ndossi 0784323068

kwa usajili.
Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam

Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing akifafanua jambo wakati wa kikao chake na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe kilichofanyika kwenye ofisi za Kituo hicho jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe (kushoto) akifafanua jambo kwa Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (kulia) walipokutana jijini Dar es Salaam

Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe (wa pili kushoto)

No comments: