Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi akitoa mada kuhusu Nafasi na Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wakati wa mkutano unaoendelea wa Mawakili wa Serikali waliokatika utumishi wa umma. Pamoja na mambo mengine Dk. Kilangi amesema Mawakili wa Seriakali walio katika utumishi wa umma watakuwa na chama chao.
Sehemu ya mawakili wa serikali kutoka wizara mbalimbali, Idara na Taasisi zinazojitegema, Wakala na Serikali za Mitaa ambao wapo Jijini Dodoma kwa mkutano wao wa siku mbili.
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi amesema, anakusudia
kuanzisha Chama cha Wanasheria walio katika utumishi wa Umma.
Dk. Kilangi ameyaeleza hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Nafasi na
Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Mawakili wa
Serikali walio katika utumishi wa umma wanaokutana katika mkutano wao wa
siku mbili unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango
Jijini Dodoma.
Mawakili hao wa Serikali wapatao mia tisa ( 900) wanatoka Wizara
mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi na Mashirika yanayojitegemea, Wakala
na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mkutano huo ambao ni wa pili kufanyikia
ulifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kwamba, kuanzishwa kwa Chama
hicho ni kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Muswaada wa Sheria ya Marekebisho
Mbalimbali ( Na.2) 2018 inayoeleza kuwa , “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali
anaweza kuanzisha Chama cha Wanasheri katika Utumishi wa Umma”.
Amewaeleza Mawakili wa Serikali kwamba Chama hicho kitakuwa
kinakutana mara moja kwa mwaka kwaajili ya kujadili masuala mbalimbali ya
kisheria ikiwamo maendeleo ya taaluma hiyo.
Dk. Kilangi amesema, pamoja na wanachama wa chama hicho kukutana mara
moja kwa mwaka, Waziri mwenye dhamana na mambo ya sheria anaweza
kuitisha mikutano ya wanasheria waliokatika utumishi wa umma kila anapoona
kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Amefafanua zaidi kwa kusema, ripoti ya mikutano ya chama hicho
itawasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba, Waziri atatunga
Kanuni kuhusu usimamizi, uongozi, muundo na uendeshaji wa shughuli za
chama.
Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuanzishwa kwa chama cha
Mawakili wa Serikali walio katika utumishi wa Umma hakutawanyima fursa
mawakili hao ya kujiunga au kuwa wanachama wa vyama vingine vya
kitaaluma kikiwamo Tanganyika law Society ( TLS).
Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa daftari la mawakili wa serikali,
Mwanasheria Mkuu amesema, daftari hili litaanzishwa kwa mujibu wa Ibara
ya 74 ya Muswaada wa Sheria ya Marekebisho mbalimbali ( Na. 2) 2018
unaotamka kwamba, “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataanzisha Daftari la
Mawakili wa Serikali ( Roll of State Attorneys)”.
Amesema daftari hilo likuwa na majina ya mawakili wa serikali kwa kuzingatia
ukuu ( seniority ) miongoni mwao na kusisitiza kwamba, hatua hiyo haitaathiri
sifa au hadhi ambayo mtu alikuwa nayo kabla ya kuazishwa kwa daftari hilo.
Kuhusu mawakili hao sasa kutambulika kama wanasheria wa Serikali ( State
Attonerys ) Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelitolea ufafanuzi kwa kusema
Kila Afisa Sheria aliyeteuliwa au kuajiriwa katika Wizara, Idara
inayojitegemea, wakala au serikali za mitaa sasa anakuwa wakili wa serikali na
kwa sababu hiyo yuko chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
isipokuwa kwa Wanasheria wa Serikali ambao wapo chini ya Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
“Hivyo Afisa huyo anachukuliwa kuwa anafanya kazi na kutekeleza majukumu
na mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Wizara zao , Idara
zinazojitegemea, wakala wa serikali na Serikali za mitaa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ataweweza kutoa maelekezo ya jumla au maelekezo mahsusi kwa
mawakili wa serikali walio katika utumishi wa umma kuhusu utekelezaji wa
majukumu yao ya kisheria.
Akawahimiza wanasheria hao kila mmoja wao kuendelea kutekeleza majukumu
yake kwa bidii, maarifa na ujuzi wake huku akitanguliza maslahi ya taifa lake
katika kila jambo analokishughulikia.
Akahadharisha kwamba, hatasita kuchukua hatua dhidi ya mtumishi yeyote
atakaye kiuka maadili ya Mawakili katika utumishi wake.
Awali akifungua Mkutano huo Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma,
amewataka Mawakili wa Serikali kutumia njia mbadala ya usuluhi katika
baadhi kesi za madai pale inapobidi na kufikia usuluhishi nje ya Mahakama.
Jaji Mkuu amesema , ikiwa njia ya usuluhishi nje ya mahakama utafanyika,
basi utapunguza muda wa undeshaji kwa kesi hizo ambazo nyingine huchukua
hadi miaka kumi bila kufikia muafaka.
“Niwaombe wanasheria wa Serikali katika kesi nyingine za madai pale
inapobidi wajaribu sana kulenga kufikia usuluhishi wa nje ya mahakama badala
ya kuendesha kesi kwa miaka hata kumi, kuanzia kesi inapoanza ngazi ya chini
hadi kufikia Mahakama ya Rufani” amesema Jaji Mkuu na
Akasisitiza kwamba, “ Kuna wakati wanasheria wa Serikali wanakiri kwa
pembeni, kuwa kesi wanayoendesha haina nafasi ya kushinda au hata
wakishinda gharama hadi kupata ushindi huyo ni kubwa. Wanapambana tu
kwa sababu Mkuu wa Idara au Kitengo amesema hivyo”.
Akasisitiza kwa kusema. “Hapa ndipo ipo haja ya kujenga Imani ya Mawakili
hawa ( wa Serikali) na kuwaruhusu wapate usuluhisho wa mashauri nje ya
mahakama”.
Akitoa takwimu za Kituo cha Usuluhishi ( Mediation Centre) cha Mahakama
Kuu Dar es Salaam kwa mwaka jana ( 2017) kinaonyesha kuwa jumla ya
mashauri 41 yalisuluhishwa na kituo bila ya kufikishwa Mahakama Kuu kwa
ajili ya kusikilizwa na kati ya hizo, ni 10 tu zilikuwa za taasisi ya Umma.
No comments:
Post a Comment