Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Yusuph Mazana (wa tatu kushoto), wakati akikagua nguzo ya daraja la mto Halali katika barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 wilaya ya Wanging'ombe, mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole- Sendeka, akisikiliza.
Serikali imesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM
64.6 kwa kiwango cha lami kumepunguza ajali zilizokuwa zikitokea na kutarahisisha shughuli za
kibiashara na usafirishaji wa mazao katika kanda ya nyanda za juu kusini. Amezungumza hayo mkoani Njombe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Isack Kamwelwe, wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa na
mkandarasi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group.
Waziri Kamwelwe amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo pamoja na
madaraja yake ambao kwa sasa umefikia asilimia 97.
"Nimeridhika na ujenzi wa barabara hii kwa kuwa hapo awali ilikuwa inaelezwa kuwa na ajali
nyingi lakini sasa zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upana wa barabara hii kufikia
mita tatu na nusu kila upande na mabega ya mita moja na nusu" amesema Waziri Mhandisi
Kamwelwe.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Yusuph Mazana, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia), na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole- Sendeka (kulia), kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kitengo cha mizani iliyopo eneo la Makambako mkoani humo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara nyingi hapa
nchini kwa ubora na viwango vya juu ikiwa na lengo la kurahisisha usafirishaji, kuleta
maendeleo kwa wananchi na kupunguza ajali.
"Hakuna Serikali inayopenda kupoteza wananchi wake katika ajali za barabarani hivyo ujenzi
wa barabara utaenda sambamba na usalama wa wananchi wetu kwa kuwekewa alama, taa na
michoro barabarani", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.
Kuhusu mzani wa makambako, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa mwarobaini wa foleni
katika eneo hilo umepatiwa tiba kwa kuwa sasa magari yanapimwa pande zote mbili ili kuondoa
msongamano. Aidha, amewataka wananchi kutoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za
barabarani, taa pamoja na vyuma vinavyowekwa chini ya madaraja kwani vitu hivyo vina
umuhimu wake na huongeza umakini kwa madereva wawapo barabarani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa kwanza) na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, wakitoka kukagua kingo za daraja la mto Halali lililopo katika barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 wilaya ya Wanging'ombe, mkoani humo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, pamoja na
kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa miradi ya barabara za wilayani amemuomba Waziri
Kamwelwe kujenga kipande cha barabara kwa kiwango cha lami kinachoelekea katika eneo la
mgodi wa madini ya chuma tarafa ya Mndindi wilayani Ludewa. Amemuelezea pia umuhimu wa kujenga barabara ya Kibena-Lupembe ambayo bado haijaanza
kujengwa na inatengewa fedha kila mwaka kwani ndio eneo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao
na barabara hiyo inaunganisha mkoa wa Njombe na mkoa wa Morogoro.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusuph
Mazana, amesema kuwa mpaka sasa kazi zilizobaki katika barabara hiyo ni uwekaji wa alama
za barabarani, michoro ya barabarani, kingo na taa za barabarani na kazi ya mifereji ya maji.
Mhandisi Mazana amemueleza Waziri Kamwelwe kuwa katika eneo la Makambako barabara
mpya imehamia upande wa kulia mita 2.5 na kuathiri baadhi ya maeneo ya wananchi wapatao
kaya 22 na hivyo tathimini ya mali zilizoathirika zinaendelea kuandaliwa kwa ajili ya malipo ya
fidia.
Ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 ni sehemu ya mradi wa barabara
ya Mafinga-Igawa KM 138.7 ambao umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa
Benki ya Dunia chini ya mradi wa Southern Africa Trade and Transport Facilitation Project
(SATTFP) na utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 103.
Kaimu Mhandisi Mkazi kutoka kampuni ya LEA JV South Asia, Manish Kumar
(kushoto), akimuonesha ramani Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Isack Kamwelwe (katikati), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye
urefu wa KM 64.6 kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Wa pili kushoto ni Mkuu wa
Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka akifuatilia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akisalimiana na
mkazi wa kijiji cha Ilembula wilaya ya Wanging'ombe Bi. Hadija Samuli, wakati
alipokuwa akikagua barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 inayojengwa
kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyigo-Igawa KM 64.6 inayojengwa kwa
kiwango cha lami, mkoani Njombe. Mradi wa ujenzi huo utakamilika mwezi Disemba
mwaka huu na utagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 103.
No comments:
Post a Comment