Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Sibtain Meghjee ambaye pia ni Mwenyekiti wa The Bilal Muslim Mission of Tanzania Kanda ya Ziwa akisisitiza jambo katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Bwiru jijini Mwana, mwenyekiti huyo na waumini baadhi ya dini ya Kiislamu waliakwa kushiriki kwenye ibada hiyo ambayo imeandika historia mpya baina ya Waislamu na Wakristo kuwa wote ni wamoja na wanamuabudu Mungu mmoja.Kutoka kushoto wa pili ni Kaimu Katibu Mkuu wa kanisa hilo Philipo Majuja.
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAISLAMU wa madhehebu ya Shia Ithna Asheri Imamia wamesema kitendo cha Wakristo wa Kanisa la
African Inland Church Tanzania (AICT) cha kuwaalika kushiriki Ibada kanisani kimefungua ukurasa mpya
kwa waumini wa madhehebu hayo nchini.
Mwenyekiti wa Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) Tawi la Tanzania Alhaji Sibtain Meghjee
ametoa kauli hiyo juzi katika Ibada iliyofanyika katika Kanisa la AICT Bwiru jijini Mwanza ambapo
alikabidhi fimbo 11 kwa walemavu wa macho,vitabu vya Kuran na kalenda kwa waumini wa kanisa hilo.
"Mambo mengi yaliyopo kwenye Biblia na Kuran asilimia 90 yanafanana na kinachotakiwa kwa waumini
wa dini zote za Kikristo na Kiislamu ni kuvumiliana kutokana na imani zao na hivyo ushirikiano huo
utadumisha amani na utulivu kwenye jamii bila kubaguana kwa kutofautiana kiimani,"amesema.
Sheikh wa Bilal Muslim Mission of Tanzania Sheikh Hashim Ramadhan akitoa neno kwa waumini wa kanisa la AICT Bwiru wakati wa ibada iliyowashirikisha pia waumini wa dini ya Kiislamu akisema wote ni watoto wa baba na mama mmoja na wanamwabudu Mungu mmoja na hakuna sababu ya kuchukiana bali kupendana.
Meghjee ambaye pia ni Mwenyekiti wa The Bilal Muslim Mission of Tanzania Kanda ya Ziwa amesema
wapo baadhi ya watu wenye nia mbaya wamekuwa wakieneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu
wakiwahusisha na mambo mabaya kwenye jamii na kuipongeza serikali kwa kuanzisha kamati ya amani
Mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa wa jamii moja bila kubaguana.
"Jamii imejenga tabia ya kuamini propaganda hizo na sisi Waislamu tulianza kurekebisha hali hiyo kwa
kufanya kazi za kijamii kwa kuzingatia mafunzo ya dini na malezi ya wazazi.Tujiepushe na propaganda
chafu zinazofanywa na watu wanaoropoka mambo bila ya kuwa na elimu (ufahamu) kwani kitendo cha
kuwaalika Waislamu kuja kanisani kimefungua ukurasa mpya kwa waumini wa dini zote,"amesema.
Alhaji Meghjee amesema nchini Iraq (nchi ya Kiislamu) maeneo matakatifu ya Wakristo yanalindwa na
Serikali na wana uwakilishi bungeni huku gharama za uendeshaji wa makanisa zikilipwa na serikali jambo
linaloonyesha waislamu si watu wabaya.
Mmoja wa waumini wa kanisa la AICT Bwiru akipokea kalenda na Kuran kutoka kwa Alhaji Meghjee.
Kwa upande wa Sheikh wa Bilal Muslim Mission Of Tanzania Kanda ya Ziwa Sheikh Hashimu Ramadhani
amesema wanadamu wote kwa imani ya dini ya Kiislamu wote ni watoto wa baba na mama mmoja
(Adam na Hawa) ingawa makanisani na misikitini kuna waumini wa makabila na rangi mbalimbali lengo
ni kushirikiana, kupendana na kushikamana.
Wakati huohuo Mhariri wa Star TV ambaye pia ni Mwenyekiti wa miradi ya maendeleo ya Kanisa hilo la
AICT Moses Buhilya amesema Ibada hiyo ya pamoja ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo
imeonesha ushirikiano, upendo na kuondoa mitizamo ya watu kuwa waumini wa dini hizo
waliohasimiana kutokana na imani zao za kidini.
“Kikubwa tumeweza kuondoa tofauti za kidini na kuonyesha tu Watanzania wamoja. Wenzetu wamekuja
kujifunza mafunzo yetu (Biblia) na sisi pia kujifunza yao (Kuran), tumeshiriki chakula cha pamoja na
kuangalia mahitaji ya kibinadamu na kuyatatua,”amesema Buhilya.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa AICT Mchungaji Philipo Majuja amesema kuwa "kwa niaba ya Wakristo wa
AIC Tanzania, siku ya leo(juzi) imeonyesha Wakristo wa Kanisa hili na Waislamu wameketi pamoja
kushiriki Ibada na kula pamoja.
"Ujio wenu umetufundisha kuwa Mungu wetu tunayemuabudu ni mmoja na anatupenda sote bila
ubaguzi, maana yake Yesu alikuja kuleta amani na hata sisi tunatakiwa kuleta amani katika jamii.”
Ameeleza jamii inapohaingaika na maji ujue hapo hakuna amani na kunukuu katika kitabu cha Zaburi
24: kuwa Nchi na vitu vyote vilivyomo duniani ni mali ya Bwana (Mungu) na hata Nabii Nehemia
alipokuwa na mradi wa ujenzi wa ukuta wa Yeruselemu alihitaji ushirikiano na vifaa kutoka kwa watu
ambao hawakuwa waumini akafanikiwa na hivyo ushirikiano baina na Waislamu na Wakristo upo hata
kwenye maandiko na kwenye jamii na si jambo geni.
No comments:
Post a Comment