Wednesday, April 11, 2018

TASAF YAENDELEA KUWANUFAISHA WANANCHI MKOANI SIMIYU


Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu wakikagua shamba la pamba la mnufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini(TASAF), Bibi . Rebecca Masunga (mwenye kitambaa cheupe kichwani) wa Mtaa wa Nyakabindi wilayani Bariadi wakati wa Ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA B
Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu wakiangalia mifugo ya mnufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini(TASAF), Bibi . Rebecca Masunga wa Mtaa wa Nyakabindi wilayani Bariadi wakati wa Ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA C
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akimpongeza mnufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini(TASAF), Bibi . Rebecca Masunga wa Mtaa wa Nyakabindi wilayani Bariadi kwa kununua jembe la kukokotwa na ng’ombe (plau) kwa ajili ya kulimia, wakati wa Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA D
Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu walipotembelea na kuona nyumba ya mnufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini(TASAF), Bibi . Stella Masamaki  wa Mtaa wa Old Maswa wilayani Bariadi, wakati wa Ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA E
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa maelezo ya awali juu wanafaika wa TASAF III wilayani humo wakati wa Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA F
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi  akitoa maelezo ya awali juu mradi wa Maji ulioibuliwa na wanafaika wa TASAF III katika Kijiji cha Nkoma wilayani humo wakati wa Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa  wa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA G
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani (kulia) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Simiyu na baadhi ya viongozi wa Serikali kuelekea kwenye ukaguzi wa Jengo la Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu, wakati wa ziara ya viongozi hao ya kukagua Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA H
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Ndg..Fabian Manoza akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Simiyu na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusu Jengo la Wodi ya Wazazi linalojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu, wakati wa ziara ya viongozi hao ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
PICHA I
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt. Seif Shekalaghe akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Simiyu na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusu Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Mwandete inayojengwa kwa ushirikiano wa Serikali na wananchi, wakati wa ziara ya viongozi hao ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.

…………………..
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Awamu ya tatu umeendelea kunufaisha wananchi  wakiwemo wakazi wa kijiji cha  Nkoma wilaya ya Itilima  na  Nyakabindi    wilaya ya  Bariadi  mkoaniSimiyu.

 Hayo yamebainishwa na baadhi ya Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini katika Kijiji cha Nkoma wilayani Itilima, Mtaa wa Nyakabindi na Mtaa wa Old Maswa wilayani Bariadi wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mmoja wa wanufaika wa Mpango huo, Bibi. Rebecca Masunga kutoka Mtaa wa Nyakabindi wilayani Bariadi, amesema TASAF imemsaidia kutoka katika umaskini sasa anapata kipato kinachomwezesha kujikimu, kwa kuwa amelima ekari tatu za pamba, ekari moja ya mahindi, ana ng’ombe 14 na mbuzi wanne na amenunua plau kwa ajili ya kulimia.  

“Nilikuwa maskini wa kutupwa , nilipoingia TASAF na kuanza kupokea zile elfu 36 nilikopa fedha nikalima nyanya ekari moja nikauza, nilipata shilingi laki sita nikanunua ng’ombe watatu wakakua;  baadaye nikawauza nikapata milioni moja na laki tano nilinunua ng’ombe 14 ndiyo hao mnaowaona tunawachunga sasa” alisema Rebecca Masunga

“Tuna kikundi chetu ambacho tunaweka fedha zetu baadaye tunagawana, tukisha gawana tunaenda kuzalisha, tunalima nyanya, kabeji, pamba halafu tunauza; mpango wangu wa baadaye niwe na mtaji mkubwa na nijenge nyumba bora ” alisisitiza Bibi.Masunga.

Nae Bibi. Stella Masamaki mkazi wa Old Maswa wilayani amesema kupitia mpango wa Kunusuru kaya maskini aliweza kukodi mashamba nakulima pamba, baada ya kuuza pamba akajenga nyumba bora ya vyumba vitatu na akatoka kwenye nyumba ya udongo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amewapongeza wanufaika wa TASAF ambao wamezitumia fedha hizo kwa manufaa na akawashauri kuanzisha miradi midogo midogo na kuwatumia wataalamu wa kilimo pamoja na mifugo kuwasaidia katika uendelezaji wa miradi yao ya kilimo na mifugo.

Katika hatua nyingine Mratibu wa TASAF Wilaya  Itilima Bw. John Rajabu amesema wanufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini wameibua mradi wa maji ambao pia utawanufaisha na wananchi wengine, ambapo mpaka kukamilika kwake utatumia takribani milioni 15.

Wakati huo huo Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu wamefanya ziara katika Wilaya ya Meatu, Itilima na Maswa na kukagua miradi ya Maji, Afya na Elimu nakuwataka viongozi na watendaji katika maeneo husika kutimiza wajibu wao na kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma wanazostahili.

Sanjali na hilo wajumbe hao wamewataka viongozi kutambua fedha zinazochangwa na wananchi na kusimamia vizuri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,  ili zitumike kama ilivyokusudiwa.


No comments: