Saturday, April 7, 2018

CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KAGERA (KCU) CHAFAFANUA KUHUSU MALIPO YA AWALI YA KAHAWA YA WAKULIMA


Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo Niyegila (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima wa Chama Kikuu cha Kagera KCU (1990) Ltd, Leo 7 Aprili 2018, Mwingine ni Kaimu meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg John kanjagaile. Picha Zote Na Mathias Canal, WK 

Waandishi wa habari wakifatilia Mkutano wa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo Niyegila wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima wa Chama Kikuu cha Kagera KCU (1990) Ltd, Leo 7 Aprili 2018, Katika Ukumbi wa Ofisi za Wizara ya Kilimo (Kilimo 4).

Na Mathias Canal, WK-Dodoma

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo Niyegila ametoa ufafanuzi kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima wa Chama Kikuu cha Kagera KCU (1990) Ltd kama ilivyojadiliwa kwenye Mkutano wao Mkuu tarehe 27/03/2018.

Amebainisha hayo wakati akizingumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Mjini Dodoma na kusema kuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera si Kampuni ya kununua kahawa bali ni ushirika wa wakulima wadogo wadogo wenye lengo la kuunganisha nguvu zao kwa  pamoja katika kuhudumia zao la  kahawa na kuliwasilisha sokoni kwa utaratibu wenye tija endelevu na kisha kugawana mapato  baada ya kufanya mauzo.

Alisema bei halisi ya mkulima kwa upande wa Ushirika inapatikana mara baada ya mauzo ya kahawa kufanyika ambapo  wakulima hulipwa malipo ya mwisho kwa kadri ya bei ya kuuzia iliyopatikana sokoni na hesabu ya mwisho kuwasilishwa kwenye mkutano mkuu.

Hivyo kwa vile mchakato wa mauzo huchukua si chini ya kipindi cha mwezi mmoja tangu mkulima awasilishe kahawa yake kwenye ushirika hadi malipo ya mwisho kufanyika, basi ili kumuondolea mkulima adha ya kusubiri malipo yake yote baada ya mauzo wakati anahitaji kujikimu na kukidhi mahitaji yake muhimu, wakulima wenyewe kwa utashi wao kupitia  Mkutano Mkuu, wanajadili malipo ya awali atakayotanguliziwa mkulima wakati anasubiri malipo ya mwisho.

Niyegila alibainisha kuwa mnamo tarehe 27/03/2018, Chama Kikuu cha Kagera kilifanya Mkutano wake Mkuu ambao pamoja na mambo mengine wanachama walijadili malipo ya awali ya mkulima (Advance Payments). Katika makisio hayo,  Menejimenti na Bodi ya KCU (1990) Ltd walipendekeza malipo ya awali yawe ni TZS 1,000 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda.

Alisema kuwa baada ya mjadala, wanachama waliagiza kupitiwa upya kwa makisio hasa katika upande wa malipo ya awali na kuangalia namna ya kupandisha kiwango cha malipo ya awali. Aliongeza kuwa Kiwango kipya pendekezwa kitawasilishwa kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kwa ajili ya kuidhinishwa.

Alisisitiza kuwa kile kilichojadiliwa kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama si tangazo la bei bali ni malipo ya awali kwa mkulima ambapo Kwa mujibu wa sheria, bei elekezi ya zao la kahawa inatolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania kwa utaratibu wa ushirika, bei halisi itajulikana mara baada ya mauzo ya kahawa kufanyika sokoni na si vinginevyo.

Niyegila aliongeza kuwa kwa utaratibu wa sasa wa Serikali, kahawa yote itakusanywa kupitia kwenye Vyama vya Ushirika na kupelekwa sokoni Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo wanunuzi wote watanunulia hapo mnadani.

Kwa mantiki hiyo, hakuna mkulima yeyote atakayeruhusiwa kuuza kahawa nje ya mfumo wa ushirika

No comments: