Tuesday, March 27, 2018

RIPOTI YA CAG YASABABISHA MAGUFULI KUSIMAMISHA WAKURUGENZI WAWILI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad Ikulu jijini Dar es Salaam. 




*Aagiza wachunguzwe dhidi ya tuhuma zilizobainika kwenye ripoti
*Ataka iwe fundisho kwa wakurugenzi wengine nchini, atoa angalizo
*Azungumzia ucheleweshaji kesi unaosababsha Serikali kukosa Trilion 4.4/-

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii


RAIS Dk.John Magufuli amewasimamisha kazi kuazia leo wakurugenzi wa 
Halmashauri ya Kigoma Ujiji na Pangani baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kubaini madudu yakiwemo ya kupata hati chafu.

Ametoa maagizo hayo leo asubuhi hii baada ya kupokea ripoti ya CAG Profesa Juma Asaad ambapo mbali ya kumshukuru kwa kazi nzuri aliyoifanya akatangaza kuanza kuchukua hatua kwa kuwasimamisha wakurugenzi hao ili iwe fundisho kwa wakurugenzi wengine.

"Ripoti ya CAG imezitaja halmashauri mbili iko ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ujiji na Pangani ,Nitoe maagizo wakurugenzi hao wawili wasimamishwe kazi mara moja na hata kama si vizuri kuchukua hatua basi ni vema nikachukua hatua haraka ili uchunguzi ufanyike kuhusu tuhuma ambazo CAG amezisema kwenye ripoti yake.

"Wakati natangaza kuchukua hatua za kuwasimamisha wakurugenzi hawa naona mmenyamaza najua kwasababu wengine hawependi hatua zichukuliwe lakini nimeanza kuchukua hatua iwe fundisho kwa wengine kwani tusipochukua hatua wengine wataendelea,"amesema Rais Magufuli.

Amesisitiza ni bora kuanza kuchukua hatua na kwamba hata CAG kwenye 
maelekezo yake kwa Serikali amezungumzia umuhimu wa kuchukua hatua na hivyo amenza kutekeleza hapo hapo baada ya kukabidhiwa ripoti na mengine wataendelea kuyatekeleza kwa kuchukua hatua mbalimbali ili mambo yaende.

Mbali ya kuchukua hatua za kuwasimamisha wakurugenzi hao amempa ripoti ya CAG Waziri Mkuu ili akajadiliane na makatibu wakuu wa wizara pamoja na mawaziri wote ili kuchukua hatua mbalimbali za utekelezaji wa ripoti hiyo.Rais Magufuli amesema fedha hizo ni za wananchi masikini ambao wanahitaji kupata mrejesho wa fedha zinavyotumika na kufafanua kwenye zile kesi za kodi ambazo hazijashughulikiwa basi zifanyiwa kazi kwani zimekaa muda mrefu.

Amesema hafahamu kazi za mahakama zinakwendaje na anajua kuna uhaba wa majaji na hivyo ataangalia namna ya kutafuta majaji lakini akaomba msaada wa Jaji wa Mahakama Kuu kusaidia katika hilo ambako kuna kesi za kodi zimekwama kusikilizwa na hivyo kuifanya Serikali kukosa fedha Sh.trilioni 4.4 ambazo zikipatikana zinaweza kutumika kufanya maendeleo.

"Mambo hayo yanategemeana na kama fedha haijakusanywa inakuwa ngumu kufanya mambo mengine.Kuna maombi mengi yanatolewa lakini nashindwa kutokana na mahitaji ya fedha ,wabunge wanataka kuongezewa posho lakini inakuwa ngumu, polisi wanahitaji kuongezwa lakini inashindika.kamati zinataka kufanya kazi zake lakini hakuna fedha.

"Nchi hii ni yetu na hivyo kila mmoja kwenye eneo lake akisimamie majukumu yake mambo yatakwenda na nchi itasonga mbele.Pia nirudie tena kumshukuru CAG ambaye ametoa maelekezo mazuri na hivyo nikuhakikishie tutayatekeleza,"amesema.

Pia amemhakikishia ripoti hiyo imepokelewa kwa mikono miwili na amemthibitisha kuta itafanyiwa kazi kikamilifu na amefurahi kusikia kuna maendeleo ya kupata hati safi kwa mashirika ya umma ambapo yamefikia asilimia 96 kwa kupata hati safi na TAMISEMI asilimia 90 na Serikali Kuu kutokana na vyama vya siasa imeshuka na kufikia asilimia 80.

Amesema kazi ya kumkagua mtu ni ngumu maana unapomkagua mtu anachukia ,hivyo anajua ugumu ambao CAG na watumishi wake wanaipata katika kutekeleza majukumu yao."Na ninyi kwa bahati nzuri mimi ndio mkagauzi wenu hivyo angalieni huko mnakofanya kazi msichukue hela mara mbili mbili,"amesema.

Hata hivyo amesema anataka kuona mambo yaliyopendekezwa na CAG 
yanafanyiwa kazi haraka na kufafanua kuna hoja ambazo zimekaa kwa zaidi ya miaka 20 hivyo zitatafutiwa ufumbuzi wake.Pia amesema iwapo kuna watu ni sugu ambao wamekuwa wakiambiwa kila mwaka hawasikii basi ni vema akapa taarifa za nani atolewe na nani akapumzike.

Rais amezungumzia pia uchumi wa nchi kuendelea kuimarika na kueleza kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa uchumi wake kwenda vizuri.Ameongeza kuwa Serikali inayo akiba ya fedha ya kutosha ambao inaweza kuendesha nchi kwa miezi kati ya mitano na sita.

"Ni bahati mbaya watanzania mazuri yetu hatutayasemi kwasababu ya wema wetu .Ushauri wa Profesa Asaad ni Super nimebaki nao ili nifuatilie utekelezaji wa maagizo ya CAG wakati Waziri Mkuu na mawaziri wake na makatibu wake wanaendelea kuyatekeleza,"amesema.

Wakati huohuo Rais Magufuli amesema kuna watendaji na viongozi ambao 
wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya wananchi kwasababu zao binafsi au za kisiasa.Amefafanua jana amepokea barua kutoka Tamisemi inayoelezea kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu wa kuamua makao makuu ya Wilaya ya Bumbuli yawe wapi na fedha Sh.bilioni 1.5 zimeshatolewa lakini hakuna kinachofanyika kutokana na mabishano ya viongozi wa wilaya hiyo.

"Kwa muda mrefu wanabishana na jana nimetoa maelekezo fedha zirudi Hazina ili ziende maeneo mengine ambayo wanazitaji maendeleo na wao waendelee kubishana,"amesema Rais Magufuli.

No comments: