SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limepokea tamko la Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuhusu mada tajwa hapo juu Februari 20, 2018 kwa barua yenye Kumbukumbu namba: BMT/A/2/Vol. 18/69, pia kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
BMT imeagiza kusitishwa ada hizo hadi Machi 5 itakapotoa maelekezo mengine baada ya kukutana na RT na waandaaji.
Sisi RT tumefedheheshwa na uamuzi huo na jinsi njia iliyotumiwa na BMT katika kulishughulikia tatizo linalodaiwa kuwa malalamiko ya waandaaji wa marathon kudai kuwa tozo hizo ni kubwa, tofauti na wanachokiandaa au kukifanya.
Kwani tuliamini, kutokana na miongozo ya kiutendaji, BMT ingekuwa mstari wa kwanza kulinda matakwa ya Katiba ya RT kiutendaji.
Tuliamini BMT inajua mamlaka ya utendaji ya RT, hivyo kabla ya kufikia uamuzi huo, ingetuita RT kwanza na kujadili hicho kinachodaiwa kuwa malalamiko, ndipo ingefikia kuanza kuchukua hatua.
KUPANDISHWA ADA;
Kutokana na mwenendo usioridhisha kwa muda mrefu kuhusu uandaaji wa mbio za Marathon kiholela, ambao ulikuwa haufuati taratibu zinazotakiwa, hata BMT yenyewe ni shahidi kutokana na matamshi mbalimbali ya Watendaji wake, RT iliamua kuchukua hatua kwa mujibu wa Katiba yake kama msimamizi mkuu wa mchezo wa Riadha nchini.
Mnamo Septemba 16, 2017 RT ilitoa mwito kwa waandaaji wa mbio za Marathon na kukutana katika moja ya kumbi za Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambako takribani waandaaji 28 - 30 walijitokeza.
Katika kikao hicho ambacho kilikuwa cha wazi na huru, RT iliwaeleza waandaaji kuhusiana na utaratibu mzima wa uandaaji wa mbio za Marathon na utaratibu mpya unaotakiwa kuanza kutumika kuanzia January 2018, ikiwamo kujisajili na kuzitenga mbio hizo katika makundi manne ya A, B, C na D kulingana na ukubwa wa mbio husika na kila kundi na gharama zake.
RT ilifikia uamuzi huo baada ya tathmini za kiufundi na uzoefu wake kama msimamizi mkuu wa mchezo wa riadha hapa nchini.
Katika kikao hicho yalifanyika majadiliano ya kina na waandaaji hao kutoa maoni yao kuwa viwango vya kwanza vilivyowasilishwa na RT vilikuwa vikubwa sana na kuomba kutazamwa upya.
RT ilipokea maoni hayo na Kamati Tendaji kuketi na kuvipitia upya na kisha kuja na mapendekezo mapya (siku hiyo hiyo), ambayo yaliridhiwa na pande zote katika kikao hicho.
RT ilisisitiza na kuwafafanulia wahusika kuwa, Marathon ni biashara na kama mdau ana nia njema ya kukuza na kuendeleza mchezo wa raidha kuna matukio mengi tu na si marathon pekee.
Kiufundi, waandaaji walishauriwa ili kuepuka gharama ambazo hawawezi kuzimudu, wajikite kuandaa mashindano ya Uwanjani ‘Track and field’ na mbio chini ya Kilomita 21, ambayo ni bure kabisa, zaidi ya kuhakikisha wamejisajili.
SINTOFAHAMU:
Baada ya maazimio hayo hatukuwahi kusikia au kupata malalamiko rasmi wala maoni kutoka kwa muandaaji yeyote kuhusiana na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao cha Septemba 16, 2017 Uwanja wa Taifa.
Lakini cha kushangaza, tukasikia kuna malalamiko yamepelekwa BMT kuhusiana na uamuzi halali wa kikao cha Septemba 16, 2017 baina ya RT na Waandaaji.
Tuliamini kama kuna nia ya kweli na si ovu juu ya RT, hao waliokimbilia BMT wangeweza kuja tena RT na hoja zao na wangeona hakuna ufumbuzi, ndipo wangeenda ngazi nyingine. Tofauti na kilichofanyika na kwa masikitiko makubwa BMT kulibeba na kukimbilia kutoa uamuzi bila hata ya kuketi na chombo husika kilichopewa dhamana ya kusimamia mchezo wa riadha nchini.
Kwa kuonyesha BMT haikujipa muda kulijua jambo kwanza kwa kina kabla ya kuchukua hatua yoyote, ndio maana hata katika taarifa yake imenukuu vikao ambavyo katika kumbukumbu ya RT havipo.
Sehemu ya barua ya BMT inanukuu;
“Kufuatia malalamiko yanayotolewa na waandaaji wa mashindano hayo ya marathon kufuatia kupandishwa kwa ada za kuendesha mbio hizo, hayo yamesemwa kupitia kikao kilichokaliwa Oktoba 7, 2017 kati ya Msajili, uongozi wa RT na wadau wa mashindano hayo"
“Katika kikao cha Oktoba 7, pamoja na mambo mengine uongozi wa RT ulifahamishwa na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini, umuhimu na ulazima kwa kufuata sheria, kwa waandaaji wa mashindano ya marathon kusajiliwa kama wakuzaji na mawakala wa michezo kwa mujibu wa kanuni ya 19 (1), (2), na (3)”.
RT katika kumbukumbu zake, haijawahi kuwa na kikao (specific kwa agenda ya kanuni za waandaaji wa marathon na msajili), kama ilivyoelezwa hapo juu, kuhusu taratibu RT ilihimizwa kufuata utaratibu kama vyama vyote vya michezo vinavyohimizwa na msajili.
UAMUZI WA RT
Kwanza unasisitiza uamuzi uliofikiwa katika kikao na waandaaji Septemba 16, 2017 Uwanja wa Taifa uko pale pale. BMT haiwezi kuipangia RT ada kama ambavyo haiwezi kuipangia TFF ada za viingilio nk. RT ni chombo huru na lenye majukumu makubwa ya kuhakikisha taifa letu linaleta medali za ushindi, ni jukumu la RT kujitafutia vyanzo halali vya mapato ili tusiitegemee serikali kwa kila jambo.
Tunasisitiza waandaaji wote kuhakikisha wanalipa ada kulingana na makundi yaliyopangwa na kujisajili kabla ya kuendesha matukio yao.
Pili kutokana na Kalenda ya RT, itakuwa ni ngumu Kamati ya Utendaji kuhudhuria kikao kilichoitishwa Machi 5 na BMT huko Moshi Kilimanjaro.
Sababu ni kutokana na wito mfupi wa kikao hicho, wajumbe wengi wametawanyika sehemu mbalimbali kutokana na majukumu ya kichama ikiwemo kushughulikia kambi za Taifa.
Kumbukumbu: BMT mara nyingi ilishawahi kutuhimiza tukae na waandaaji ili tupunguze msururu wa mbio za marathon ambazo hazina tija kwa taifa,
Uhalali: Chama cha waandaaji mbio sio mdau wa RT kwa maana haitambuliki rasmi kwetu, wadau halali wa RT ni waandaaji wa mbio moja moja waliojisajili na RT na kulipa ada (annual fee) pamoja na ada ya usajili.
Muundo: Categorization (madaraja) ya mbio ni jambo la kawaida duniani kote (standard practice all over the world - how can TZ be an exception? New York, Boston na London Marathon ni Lebel A wakati mbio zingine ni B,C nk.
Mwisho, tunaiomba BMT kuangalia namna ya kushughulikia masuala hususan ya kiufundi na uhuru wa kikatiba wa vyama vya michezo, ili kuepusha misigano ambayo itarudisha nyuma maendeleo ya michezo hususan riadha.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki michezo yetu.
Imetolewa na:
Wilhelm Gidabuday
Katibu Mkuu RT
24/20/2018
No comments:
Post a Comment