*Profesa Janab amesena alipopata taarifa ya kupewa tuzo hiyo hakuamini kwani...
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Profesa Mohamedi Janabi ameupongeza uongozi wa Redio Times Fm kwa kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo nchini.
Prof. Janab amesema hayo jijini Dar es Salaam baada ya uongozi wa Redio Times FM wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Rehule Nyaula kufika katika taasisi hiyo kwa lengo la kukabidhi tuzo maalum kama ishara ya kutambua mchango wao wa kizalendo wa kuokoa maisha ya watanzania.
Akizungumzia tuzo hiyo, Prof. Janab amesema baada ya kupata taarifa kuwa uongozi wa radio hiyo wanataka kutoa tuzo kwao hakuamini kwani uzoefu unaonesha mgonjwa akitibiwa na kupona hawezi kusema ahsante na utamuona tena akiumwa na kuja hospital kwa matibabu.
"Tunashukuru Radio Times kwa kutambua kazi ambayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inafanya katika kuwahudumia wa Watanzania kwa kuhakikishia tunaokoa maisha yao. "Tuzo hii ni ishara ya ninyi kutambua huduma nzuri ambazo tumekuwa tukizitoa. Malengo yetu ni kuendelea kuhudumia wagonjwa wengi wenye magonjwa ya moyo na ikiwezekana mwaka huu tuhudumie hata wagonjwa 70,000 au 80,000 kwani uwezo tunao, amesema Profesa Janab.
Kuhusu huduma za matibabu ambazo wanazitoa katika Taasisi hiyo amesema zipo katika ubora wa hali ya juu na kwa Bara la Afrika Kwan nchi za Sub Saraha wanashika nafasi ya pili na ya kwanza ni Afrika Kusini.
Ameongeza uwepo wa taasisi hiyo mbali ya kuokoa maisha ya Watanzania ambao wanafika kupatiwa matibabu, pia wameisaidia Serikali kuokoa fedha nyingi ambazo zilikuwa zinatumika kugharamia wagonjwa wa moyo wanaopelekwa nchi India kwa matibabu.
Amesema wameokoa zaidi ya Sh. bilioni 29 kwa 2017 ambazo Serikali ingetumia kwa ajili kupeleka wagonjwa nje ya nchi.Amesema kuwa ikitokea kwa mwaka wagonjwa wanaokwenda India kwa matibabu 400 basi na ya wagonjwa watakuwa wenye matatizo ya moyo.
"Kuna mgonjwa anaweza kuletwa hapa kwetu ametokea Katavi na kisha akapelekwa Bugando halafu akaja Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na kote ambako amekwenda anaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini tukimfanyia vipimo tunabaini haitaji kufanyiwa upasuaji.
"Sasa kuna wagonjwa wangapi wamepelekwa India ikionekna wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wakati si kweli na fedha Serikali inakuwa imelipa fedha tayari. "Serikali inadaiwa mabilioni ya fedha kwasababu tu kupeleka wagonjwa wa moyo nje. Tunataka wagonjwa wa moyo hapa kwetu iwe mwisho kwa kupata matibabu na si kuwapeleka nje ya nchi,"amesema Profesa Janab.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Radio Times Fm, Nyaulawa amesema wametoa tuzo hiyo maalum ya kutambua mchango wao umetokana na ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo."Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inafanya kazi kubwa na nzuri katika kuokoa maisha ya watanzania wenzetu wanaofika kupata huduma za magonjwa ya moyo.
"Kwa kutambua umuhimu wao tumeona ipo haja ya kutambua mchango wao wa kizalendo kwa nchi yetu,"amesema Nyaulawa. Pia amesema wanatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuwa bora.
No comments:
Post a Comment