Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafikisha huduma ya maji kwenye maeneo yao kwa wastani wa asilimia 75 hadi kufikia mwakani.
Akihutubia wadau wa Sekta ya Maji jijini hapa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Usambazaji Maji nchini, Mhandisi Kamwelwe alisema Halmashauri zinatakiwa kufikia asilimia hizo, ili kutekeleza Ilani ya chama tawala ya kuwapatia wakazi wa mijini wastani wa asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.
“Nitumie fursa hii kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafikisha asilimia 75 mwakani, na zile Halmashauri ambazo wanahisi hawatafika waje tuzungumze tuone namna gani ya kuweza kufika hapo” aliagiza Waziri Kamwelwe.
Mkutano wa wadau wa usambazaji maji hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau wa sekta hiyo, ambapo mada mbali mbali hutolewa na wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi, na kwa mwaka huu jumla ya mada 20 zitatolewa kwa washiriki wa mkutano huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, amewashukuru Jumuiya ya Wasambazaji Maji (ATAWAS) kwa jitihada zao za dhati za kuhakikisha Sekta ya Maji inapiga hatua kimaendeleo.
Pia, amewahakikishia kuwa wizara itatoa ushirikiano wa kutosha, kuhakikisha lengo la kuwapatia wananchi wa Tanzania huduma bora na endelevu ya majisafi na usafi wa mazingira linafikiwa. “Wizara yote leo ipo hapa, Waziri na Katibu Mkuu wote tupo, sasa ni nguvu gani mnayoitaka tena? Tuwahakikishie kuwa tupo pamoja na nyie ili kutimiza lengo la Serikali yetu,’’ alisema Prof. Mkumbo.
Mkutano wa mwaka wa ATAWAS umeanza tarehe 23 na kukamilika tarehe 25 mwezi Novemba na hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu katika Sekta ya Maji.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi. Isack Kamwelwe akihutubia washiriki wa mkutano katika Ukumbi wa Tanga Beach Resort.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati alipokuwa akitoa neno.
Mwenyekiti wa ATAWAS, Mhandisi Mkama Bwire wakati alipokuwa akitoa maelezo.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mkutano na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe.
No comments:
Post a Comment