Thursday, November 23, 2017

DK.MAHENGE: HALMASHAURI ZIHAKIKISHE ASILIMIA 10 YA FEDHA ZA VIJANA, WANAWAKE NA WALEMAVU ZINATUMIKA KUTEKELEZA MKAKATI WA SERIKALI YA VIWANDA.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amezitaka Halmashauri za Wilaya, Mji na Manispaa Mkoani Dodoma kuhakikisha zinatenga asilimia kumi (10%) ya makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na Walemavu kuanzisha miradi ya viwanda vidogo na vya kati.

Lengo ni kuitikia kampeni ya Serikali inayoitaka Mikoa kuanzisha viwanda kama ilivyozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo.

Akizungumzia hilo, ameonya tabia ya baadhi ya Halmashauri kutotoa asilimia kumi (10%) ya makusanyo yake ya ndani au kutoa kiasi kidogo kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu na kuwa utaratibu unaotumika sasa wa Halmashauri kukopesha fedha hizo wakati mwingine sio muafaka sana badala yake Halmashauri zitumie fedha hizo kuwafungulia vijana, wanawake na walemavu viwanda vidogovidogo na kuwakabidhi waendeleze uzalishaji na kuviendesha.

Dkt. Mahenge amebainisha hayo wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Wilaya za Mkoa wa Dodoma kujitambulisha na kukagua miradi ya maendeleo ambapo amesema kuwa viwanda vinavyoweza kuanzishwa ni vya uchakataji wa nafaka, usindikaji mazao na utengenezaji vyakula vya Mifugo.

Amesema kuwa asilimia kumi hiyo ikitumika na kusimamiwa vizuri inaweza kutekeleza kampeni ya kuanzisha viwanda ambapo vijana na wanawake wanaweza kufaidika kuanzia ngazi za chini kama vijijini kwa kupata ajira kipato na halmashauri kupata ushuru. 

Aidha, ameongeza kuwa mbali na uanzishaji viwanda miradi mingine Halmashauri inayoweza kuwaanzishia vijana, wanawake na walemavu ni pamoja na ufugaji samaki kwa kuwachimbia mabwawa.

Ametaja miradi mingine mbali na viwanda kuwa Halmashauri zinaweza kuchimba visima na kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili vijana, wanawake na walemavu waendeshe kilimo cha umwagiliaji kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yanaweza kuwa malighafi kwenye viwanda vinavyoanzishwa.

“Sisi ni Viongozi, maana ya kuwa viongozi ni pamoja na kuwasaidia wananchi kuweza kufanya maamuzi yenye manufaa kwao na uanzishwaji wa viwanda utawanufaisha wananchi wengi na Mkoa kwa ujumla” alimalizia Dkt. Mahenge.

No comments: