NA HAMZA TEMBA - WMU.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeunga mkono uamuzi uliofikiwa na kamati maalum iliyoundwa na Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na wananchi wa kitongoji cha Uvinje walioanzisha makazi ya kudumu ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadan kinyume cha sheria.
Kamati hiyo iliyoundwa na wajumbe watatu ambao ni Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo, Uongozi wa Kitongoji cha Uvinje na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Saadan ilifikia maazimio kuwa wananchi wa kitongoji hicho walioanzisha makazi ndani hifadhi hiyo waondolewe kwa utaratibu wa kulipwa fidia ili kumaliza mgogoro huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Wilayani Bagamoyo, Mwenyekii wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Ndetiye alisema baada ya kutembelea eneo hilo wamejiridhisha kuwa Kitongoji hicho cha Uvinje kimeanzishwa ndani ya eneo la hifadhi ambapo ni kinyume cha sheria.
"Kiuhalisia tumeona kuna kitongoji ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadan, tumewasikiliza wananchi, tumesikiliza upande wa Serikali, kwa mujibu wa taratibu na sheria wale wananchi wanapaswa watoe ushirikiano, tunaamini kuna taratibu za Kiserikali zinafanywa kuhakikisha wale wananchi wanalipwa ili waondoke kwa usalama" alisema Ndetiye.
Aliongeza, "tumeona jinsi ambavyo baadhi ya wananchi hawako tayari kulipwa, lakini nadhani wakieleweshwa vizuri wataelewa kuwa ile ni hifadhi ya Taifa, na kama ni hifadhi ya Taifa basi inahusu maslahi ya Taifa, hivyo kila mwananchi anatakiwa atoe ushirikiano ili angalao Serikali ifanye uwekezaji wa kueleweka"
Ndetiye alisema kamati hiyo imeshaweka maazimio kwa ajili ya kushauri Bunge ili liazimie ni nini kifanywe na Serikali kumaliza mgogoro huo. Alisema, "Kwa udharura wake na kutokana na maelezo ya mkuu wa Wilaya, kwa ujumla kamati inakubaliana nayo kwasababu ameeleza vitu ambavyo tumeona vina tija zaidi kwa watanzania na tunaenda kulishauri Bunge na Serikali haraka iwezekanavyo ili hatua ziweze kuchukuliwa kumaliza mgogoro huo".
Awali akielezea kuhusu mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga alisema baada ya maazimio ya kamati iliyoundwa na Serikali ya wilaya kumaliza mgogoro huo baadhi ya wananchi walikubali maazimio yaliyowekwa ya kulipwa fidia huku wengine wakikaidi kuondoka akiwemo muwekezaji aliyeshikilia sehemu ya eneo hilo kwa zaidi ya miaka tisa bila kuwekeza mradi uliokusudiwa ambapo wamepewa kipindi cha mwezi mmoja waondoke kwa hiari kabla ya nguvu kutumika kuwaondoa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uvinje, Hussein Akida alisema kitongoji hicho kilianzishwa ndani ya kijiji cha Saadan katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani zaidi ya miaka 100 iliyopita huku kikiwa na ukubwa hekta 3,000 na mpaka sasa Kitongoji hicho kina wakazi wasiopungua 72. Aliiomba Serikali kutambua mipaka ya kitongoji hicho pamoja na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walitilia mashaka uwiano wa kimahesabu wa taarifa hiyo na uhalisia ambapo walihoji iweje kitongoji chenye miaka mingi kiasi hicho kiwe bado hakijapewa hati ya kuwa kijiji kamili pamoja na idadi ndogo ya wananchi wasiongezeka ndani ya muda mrefu wa miaka zaidi ya 100 toka kuanzishwa kwa Kitongoji hicho.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema, mgogoro huo uko wazi na unapaswa kumalizika mara moja kwa kuwa Serikali ya Wilaya kupitia kamati iliyoundwa imeshafikia maazimio ya kuwaondoa wananchi walioanzisha makazi ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha Sheria. Alitoa wito kwa wananchi kutii sheria za hifadhi na kuheshimu mipaka iliyowekwa kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya Serikali na wananchi.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (kushoto) akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi atashasta Ndetiye kwa ajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadan hususan eneo lenye mgogoro wa ardhi baina ya kitongoji cha Uvinje na Hifadhi hiyo wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani jana. Wananchi wa kitongoji hicho ambao wameweka makazi ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria wametakiwa kuondoka kwa hiari katika kipindi cha mwezi mmoja kupisha eneo la hifadhi kabda ya kuondolewa kwa nguvu ambapo watalipwa fidia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Ndetiye (wa tatu kushoto) akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Uvinje wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya kitongoji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani humo jana. Wananchi wa kitongoji hicho ambao wameweka makazi ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria wametakiwa kuondoka kwa hiari katika kipindi cha mwezi mmoja kupisha eneo la hifadhi kabda ya kuondolewa kwa nguvu ambapo watalipwa fidia.. Wengine pichani ni Naibu Waziri,Wizara ya Maliasili, Mhandisi Ramo Makani(wa pili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga (kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa tatu kushoto) akiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kutembelea eneo lenye mgogoro baina ya Kitongoji cha Uvinje na Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya kamati hiyo kwenye eneo hilo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani jana. Wananchi wa kitongoji hicho ambao wameweka makazi ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria wametakiwa kuondoka kwa hiari katika kipindi cha mwezi mmoja kupisha eneo la hifadhi kabda ya kuondolewa kwa nguvu ambapo watalipwa fidia. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Ndetiye (wa nne kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Hemed Mwanga (wa pili kushoto).
Wajumbe wa kamati hiyo wakijadili baadhi ya mambo waliyoyaona katika eneo hilo lenye mgogoro.
Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mtango Mtahiko ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo akiwasilisha taarifa ya Shirika hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadan jana wilayani Bagamoyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Hemed Mwanga (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu mgogoro baina ya kitongoji cha Uvinje na Hifadhi ya Taifa ya Saadan.
Wajumbe wa kamati wakikagua eneo hilo la mgogoro.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),ambaye alikuwa Muhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan Dkt. James Wakibara (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Utalii wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Imani Nkuwi kandokando ya fukwe za Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wilayani Bagamoyo jana.
Baadhi ya maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wakitembelea fukwe za Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wilayani Bagamoyo jana.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete (kushoto) na Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Gerald Magiri wakitembelea fukwe za Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya kamati hiyo kwenye hifadhi hiyo jana.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Uvinje, Hussein Akida akitoa maoni yake kuhusu mgogoro huo mbele ya kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii jana. Kulia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Ndetiye.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuri (katikati), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dkt. James Wakibara (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Wizara hiyo, Dkt. Iddi Mfunda wakisikiliza maoni ya wananchi wa kitongoji cha Uvinje katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wilayani Bagamoyo jana.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho wakitoa maoni yao mbele ya kamati.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Moses Nnauye (kulia) akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Uvinje wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya kitongoji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani humo jana. Wananchi hao ambao wameweka makazi ndani ya hifadhi hiyo wametakiwa kuondoka katika kipindi cha mwezi mmoja kupisha eneo la hifadhi ambapo watalipwa fidia. Nyuma yake kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Ndetiye.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Moses Nnauye (kushoto) akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Uvinje wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya kitongoji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani humo jana. Wananchi wa kitongoji hicho ambao wameweka makazi ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria wametakiwa kuondoka kwa hiari katika kipindi cha mwezi mmoja kupisha eneo la hifadhi kabda ya kuondolewa kwa nguvu ambapo watalipwa fidia. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Ndetiye.
Nyumba inayodaiwa kuwa ni ya muwekezaji anaeshikilia moja ya eneo katika hifadhi ya taifa ya Saadan kwa madai kuwa alipimiwa eneo hilo na Serikali. Taarifa zilitolewa ni kuwa eneo hilo lilipimwa kiholela bila ya kufuata taratibu za kisheria. Hata hivyo licha ya muwekezaji huyo kutoka nchini Botswana kukaa katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka tisa ameonekana hajaendeleza eneo hilo kwa lengo lililokusidiwa.
No comments:
Post a Comment