UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa
Spika,
leo tumefika mwisho wa Mkutano wa Saba wa Bunge la 11
ulioanza Jumanne ya tarehe 4 Aprili, 2017. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii, tena baada ya kuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu
na kwa umahiri mkubwa. Huu ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu
kutokana na jukumu kubwa la kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka
wa Fedha 2017/2018 ulioanza tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni
nzuri na ya kihistoria ni ya pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali
ya Awamu ya Tano zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.
2.
Mheshimiwa
Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 13 Aprili, 2017
tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari polisi
wetu 8 waliopoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa na kundi la
wahalifu katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti mkoani Pwani. Askari
hao waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC
Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub. Pia, hivi
karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani
walivamiwa na kupigwa risasi na majambazi katika Kijiji cha Bungu “B” kilichopo
Wilayani Kibiti. Aidha, wananchi wetu wengi wamepoteza maisha kutokana na
uhalifu unaofanywa na majambazi waliopo katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na
Mkuranga.
3.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kulaani
kitendo hicho cha kihalifu, na kutoa pole kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa
kuondokewa na vijana hao shupavu. Aidha, natoa pole kwa familia za wafiwa wote
kwa kuondokewa na wapendwa wao. Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu
hayakubaliki na wala hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja
na mali zetu. Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio
kwetu sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa
na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza
kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.
4.
Mheshimiwa Spika, asubuhi ya tarehe 6 Mei, 2017,
nchi yetu iliamka na simanzi kubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha ya watu
36, wakiwemo wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye safari
ya kimasomo Wilayani Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na kuacha
vilio kwenye familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema Peponi
roho za marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na marafiki wa watoto
hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani huo mkubwa walioupata.
Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na ukaguzi wa vyombo vya
moto vya usafiri kwa wanafunzi na abiria wafanye ukaguzi wa kina na wa mara kwa
mara ili kuliepusha Taifa na ajali zinazoweza kuzuilika.
5.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia ilipata pigo la
kuondokewa na watumishi wawili wastaafu waliolitumikia Taifa hili kwa umahiri
na uadilifu mkubwa. Watumishi hao ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa Katibu wa
Rais wa Awamu ya Kwanza; na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma. Namwomba Mwenyezi Mungu awape
pumziko la amani marehemu wote baada ya kulitumikia Taifa letu kwa utumishi
uliotukuka na umahiri mkubwa.
SHUGHULI
ZA BUNGE
6.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na kupitisha bajeti za Wizara zote 19 na
Bajeti nzima ya Serikali Kuu, kupitisha Maazimio
matano (5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kupitisha Miswada ya
Sheria mbalimbali, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi; Muswada wa
Sheria ya Fedha wa mwaka, 2017; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa Mwaka 2017; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu
Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa
Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.
7.
Mheshimiwa
Spika, katika
Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya msingi na mengine 1,834 ya
nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu. Vilevile, katika
kipindi hiki Ofisi ya Bunge iliendesha Semina mbalimbali kwa Waheshimiwa
Wabunge kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala
mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.
8.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu pia lilipata
fursa ya kuchagua Wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ambapo Wabunge tisa walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao, watano ni
wanawake, na wanne ni wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge hao
wataiwakilisha vema nchi yetu na kwamba watatimiza kikamilifu wajibu wao kwa
mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaelekezwa kufanya kazi kwa karibu na Wabunge
hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano unaostahili ili waweze kutekeleza
vizuri majukumu yao kwenye Bunge hilo.
9.
Mheshimiwa
Spika, nitumie
fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika,
Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake,
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja
na watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa
kwenye Mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa.
10.
Ninawapongeza pia na
kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo mazuri ya
ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ya
Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za Kudumu za Bunge na hoja
zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi ndani ya Bunge zima. Serikali
inathamini sana maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea
kuzingatia maoni na ushauri wao.
AZIMIO LA BUNGE KUUNGA MKONO JITIHADA
ZA MHESHIMIWA RAIS
11.
Mheshimiwa
Spika,
tarehe 14 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali
katika Sekta ya Madini. Aidha, tarehe 29 Juni, 2017 Bunge lako lilikubali kwa
kauli moja kuridhia mabadiliko ya ratiba ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti ili
kuongeza siku tano za kazi kwa lengo la kuwezesha kujadili
Miswada mitatu ya mwaka 2017 inayohusu kulinda maliasili na rasilimali za Taifa
ikiwemo madini. Hii inadhihirisha kwamba Bunge hili ni la wananchi
na linazingatia maslahi ya nchi.
12.
Mheshimwa
Spika,
napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi
wake mahiri, juhudi na hatua stahiki anazoendelea kuchukua ili kuhakikisha
kwamba Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali za Taifa. Nawasihi
wananchi wote na viongozi, tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika
jitihada zake hizo za kulinda maliasili za nchi yetu.
HALI YA ULINZI NA
USALAMA:
13.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya
ulinzi na usalama nchini ni shwari. Usalama wa raia na mali zao unaendelea
kulindwa, na mipaka yote ya nchi yetu iko salama. Aidha, vikosi vya ulinzi na
usalama viko imara na madhubuti katika kulinda mipaka na usalama wa nchi yetu.
Hata hivyo, wapo baadhi ya wenzetu wanaotishia usalama wetu kwa kushiriki kwenye
vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha. Mathalan, katika miezi ya hivi karibuni,
kumekuwa na mauaji ya kuvizia katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
14.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni
kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania, wakiwemo wananchi wa Wilaya za
Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanakuwa huru kufanya shughuli zao za maendeleo bila
kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi
na za muda mrefu ili kurejesha hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza
doria na vitendea kazi kwa askari. Vilevile, tumefanya maamuzi ya kuunda Kanda
Maalum ya Kipolisi katika Mkoa wa Pwani itakayojumuisha Wilaya za Mkuranga,
Kibiti na Rufiji na tayari Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Maalum
amekwishateuliwa. Hivyo, natoa wito kwa raia wema katika Wilaya hizo, waendelee
kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuwezesha watuhumiwa wote kukamatwa.
15.
Mheshimiwa Spika, sanjari na mikakati ya
kudhibiti uhalifu unaofanywa ndani ya nchi, tunaendelea pia kudhibiti uhalifu
unaovuka mipaka (cross border crimes). Ili kutimiza jukumu hilo, tunaendelea
kuboresha huduma za uhamiaji na kudhibiti nyaraka zinazotolewa na Idara ya
Uhamiaji. Tumeanzisha mfumo wa kuhakiki nyaraka, hususan vibali vya kuishi
nchini pamoja na Hati za Kusafiria. Vilevile, tumehuisha utaratibu wa kisheria
wa kutoa “migrant pass” kwa wahamiaji walowezi, ili kuweza kuwatambua kwa
urahisi. Kwa jitihada hizi, tutaweza kudhibiti nyaraka za kughushi na kudhibiti
wahalifu wa kimataifa wanaovuka mipaka.
URATIBU WA MAAFA:
16.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa
masika, baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalipata mvua za juu ya wastani na hivyo
kusababisha maafa na madhara kwa wananchi ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu
mkubwa wa makazi na miundombinu. Mikoa iliyoathirika zaidi ni Tanga, Arusha,
Kagera, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba. Kutokana na mvua hizo, watu
15 walipoteza maisha, 78 walijeruhiwa, nyumba 1,845 na majengo 36 ya taasisi
mbalimbali yaliharibiwa katika viwango tofauti. Vilevile, miundombinu ya
barabara 48 katika mikoa 11 iliathiriwa na hivyo kuzorotesha kwa muda usafiri
na usafirishaji katika maeneo husika. Aidha, viwanja vya ndege vya Arusha,
Musoma, Ziwa Manyara, Mafia na Sumbawanga navyo viliathiriwa na mvua hizo.
Natoa pole kwa waathirika wote kutokana na kadhia hiyo.
17.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na
athari za mvua hizo, Serikali iligharamia matibabu ya majeruhi na mazishi ya
waliopoteza maisha. Aidha, Serikali imetoa misaada ya kibinadamu kama vile
chakula, dawa, nguo na kufanya matengenezo ya dharura kwa miundombinu
iliyoharibika. Zoezi la ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua
linaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.
18.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kutoa elimu kwa umma kuhusu menejimenti ya maafa hususan kuzuia na kuweka
mipango thabiti ya wananchi kujiandaa na maafa ili kupunguza athari za maafa
pindi yanapotokea. Aidha, tutaendelea kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa
mara kwa mara na kwa wakati, ili kutoa fursa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa
na wananchi kujiandaa.
Vilevile, tutakamilisha mifumo ya ufuatiliaji wa maafa kwenye kituo chetu
cha Uratibu
na Mawasiliano wakati wa Dharura; kuainisha na kutambua maeneo hatarishi kwa
maafa pamoja na kuendelea kuijengea
uwezo Idara yetu ya Uratibu wa Maafa.
19.
Mheshimiwa
Spika, kuanzia tarehe 4 Aprili, 2017 hadi tarehe 20 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu lilipokea, kujadili
na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Taasisi mbalimbali za
Umma, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Mfuko wa Bunge na Mfuko wa
Mahakama. Aidha, Bunge lilipokea na kujadili Hoja ya Serikali kuhusu Hali ya
Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016, Mpango wa Maendeleo pamoja
na makadirio ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka
2017/2018 ya jumla ya Shilingi Trilioni
31.7.
20.
Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza kwa
dhati Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu
Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb.) kwa hotuba nzuri ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti
ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. Nawapongeza pia
Watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa umakini mkubwa wa maandalizi ya
Bajeti yenyewe. Aidha, nawapongeza kwa kutoa maelezo na ufafanuzi wa
kina kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuhitimisha Hoja hiyo. Kipekee
kabisa, nawapongeza na kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa hoja za maboresho na kwa kupitisha Bajeti ya Serikali
kwa kura nyingi.
21.
Mheshimiwa Spika, kura
za Waheshimiwa Wabunge kupitisha Bajeti ya
Mwaka 2017/2018 ni kielelezo kwamba, Bajeti hii inajibu kiu ya wananchi ambao
ninyi Waheshimiwa Wabunge mnawawakilisha. Kupitia michango yenu na kwa pongezi
zenu kwa Serikali, nimepata faraja kwamba mnathamini na kuheshimu usikivu wa Serikali
kwa maoni ya wananchi. Serikali hii ni sikivu, makini na inazingatia maslahi ya wananchi
walio wengi na hasa wa kipato cha chini. Hivyo,
napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali siyo
tu itaendelea kusikia, bali itasikiliza na kuchukua hatua, kama tulivyofanya
kwenye Bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa kufuta kodi
mbalimbali za kero hasa katika kilimo na mifugo ili kuwawezesha wananchi
kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
22.
Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako kuidhinisha Bajeti ya Serikali, tutahakikisha
tunasimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/2018. Tayari
tumeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, ambao unaainisha hatua
za utekelezaji, vigezo vya kupima ufanisi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa
katika kukamilisha miradi husika. Vilevile, tunaandaa mfumo wa kuhifadhi
taarifa za miradi ya maendeleo (National Project Databank) ili kufuatilia kwa
karibu utekelezaji wa miradi na changamoto zinazoikabili, kwa lengo la
kuikwamua. Sanjari na hatua hizo, Serikali imetoa maelekezo kwamba, Vitengo vya
Ufuatiliaji na Tathmini viimarishwe na kupewa nyenzo stahiki ili vifuatilie
miradi ya maendeleo hatua kwa hatua. Shabaha yetu ni kuhakikisha kuwa miradi
inasimamiwa kikamilifu, inaleta tija na kutekelezwa kwa ubora na viwango
vilivyoainishwa kwenye Mikataba.
23.
Mheshimiwa Spika, ni
ukweli usiopingika kwamba, mipango tuliyojiwekea haiwezi kufanikiwa, endapo
tutazembea katika ukusanyaji wa kodi na mapato ya Serikali. Hivyo, Serikali
itaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato;
kuimarisha ukusanyaji wa mapato; kudhibiti biashara
ya magendo; kuhimiza matumizi ya mashine za
kielektroniki katika ukusanyaji mapato na kudhibiti udanganyifu katika
ukadiriaji wa ushuru wa forodha. Wito
wangu kwa Waheshimiwa Wabunge ni kuhakikisha kuwa mnashirikiana na Halmashauri
kubuni vyanzo vya mapato na kuhamasisha ulipaji wa kodi bila shuruti.
24.
Mheshimiwa Spika, kulipa
kodi ni uzalendo, tuwahamasishe wananchi wenzetu waone fahari kuwa sehemu ya
mafanikio ya nchi yetu kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi. Ahadi yetu
ni kuendelea kusimamia kila senti itakayokusanywa, ili
itekeleze jukumu lililokusudiwa. Aidha, tutaendelea kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha kwamba
fedha zilizotengwa zinatumika kwa umakini na kuleta tija
kwa maendeleo ya nchi yetu. Tulipe kodi kwa maendeleo ya nchi yetu!
SEKTA YA
KILIMO
Hali ya chakula
nchini
25.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu
kwamba, hali ya chakula siyo ya
kuridhisha sana, bado kuna maeneo yenye upungufu wa chakula. Pia,
yapo maeneo yaliyopata mvua nyingi ambayo yamepata chakula cha kutosha. Hii ni
kutokana na mazao
ya chakula katika maeneo hayo kuanza kukomaa. Aidha,
kutokana na wakulima katika baadhi ya maeneo kuanza kuvuna mazao yao, mwenendo
wa bei za vyakula hususan mahindi imeanza kushuka katika masoko mbalimbali.
Hata hivyo, kutokana na nchi
zinazotuzunguka kuwa na upungufu mkubwa wa chakula, na umuhimu wa kuwa na
usalama na kujitosheleza kwa hifadhi ya chakula, ni vizuri kila kaya
ikahakikisha kwamba inakuwa na akiba ya chakula kwa matumizi ya baadaye. Aidha,
tumepiga marufuku usafirishaji mahindi nje ya nchi bila kibali, badala yake
tunahamasisha uongezaji wa thamani ya mazao badala ya kusafirisha nafaka ghafi.
Hii inatokana na kuwepo na maeneo ambayo hadi sasa hayana chakula cha kutosha. Nashauri
Wafanyabiashara wasambaze mahindi huko. Aidha, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ya
Mipakani kutekeleza agizo la Serikali la kuchukua hatua kwa watakaokiuka agizo
hilo.
Mfumo mpya wa
Usambazaji wa Mbolea
26.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inajipanga vyema msimu ujao wa kilimo kwa
kusambaza pembejeo na kuhamasisha matumizi ya mbolea. ili kufanikisha azma
hiyo, katika bajeti ya Mwaka 2017/18 Serikali imeamua kuimarisha utaratibu
wa upatikanaji na usambazaji mbolea kupitia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa
Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement
System).
27.
Mheshimiwa
Spika,
kupitia
mfumo huo,
mbolea itaagizwa na waagizaji watakaopitishwa kwenye utaratibu wa zabuni, na wakulima wataweza kununua mbolea
hiyo katika maduka ya pembejeo vijijini kwa bei dira itakayopangwa na Serikali.
Mfumo huo mpya utaanza kwa kuingiza mbolea ya kupandia aina ya DAP na mbolea ya
kukuzia aina ya UREA ambazo zinatumiwa na wakulima wengi. Mbolea za aina
nyingine zitaendelea kuletwa kwa utaratibu wa zamani. Napenda kurejea maelekezo
yangu kwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwamba isimamie kikamilifu zoezi
hili la usambazaji wa mbolea ili kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima
miezi miwili au mitatu kabla ya msimu wa kilimo haujaanza.
Maboresho kwenye
Sekta ya Mifugo
28.
Mheshimiwa
Spika,
pamoja na idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo nchini, lakini mchango wake kwenye
Pato la Taifa na katika kutuingizia fedha za kigeni siyo
wa kuridhisha. Kutokana na hali hiyo, tarehe 15 Juni 2017 nilikutana na Maafisa
Mifugo wa Wilaya zote nchini kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya
kuboresha sekta ya mifugo nchini ili iweze kuleta tija na kuongeza mchango wake
kwenye Pato la Taifa. Miongoni
mwa mikakati tuliyojiwekea ni pamoja na kuwawezesha wafugaji
kupata maeneo mahsusi ya malisho ya mifugo yao na kuwapatia mafunzo ya stadi za
ufugaji bora. Vilevile, tumetoa maelekezo kwa Maafisa Mifugo kuwatembelea
wafugaji ili kuwahudumia na kuwapa mafunzo ya ufugaji bora. Aidha, tumezindua
Mwongozo wa Ufugaji Bora nchini, ambao utakuwa ni dira ya kuwaongoza wafugaji
kuhusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo nchini. Lengo letu ni kuwa na mifugo
michache lakini yenye tija kubwa. Hata hivyo, tumekemea wafugaji wasilishe
mifugo yao katika mashamba yenye mazao ya chakula, na pia kuchungia kwenye misitu
iliyohifadhiwa. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo au katazo
hilo.
SEKTA YA ARDHI
Upimaji na Umiliki wa ardhi
29.
Mheshimiwa
Spika,
ardhi isiyopimwa ina thamani ndogo na ni chanzo cha migogoro isiyo ya lazima.
CCM iliona jambo hili, na kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015, iliielekeza Serikali
kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeweka Mkakati na Mpango Kazi wa
kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi
katika vijiji 1,500 na wilaya 5 kila mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua
hatua stahiki za kupunguza gharama za umilikaji wa
ardhi nchini. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imepunguza tozo ya
mbele (premium) kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu.
Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na
kumilikishwa ardhi.
Kuimarisha
Huduma katika Ofisi za Ardhi za Kanda
30.
Mheshimiwa
Spika, kazi
ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilimali watu. Serikali
itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada
mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi stahiki. Lengo letu ni
kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda badala ya
kufuata huduma hizo Makao Makuu ya Wizara. Nawasihi watumishi watakaohamishiwa
katika Ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika Halmashauri, wafanye kazi
kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya
ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi, bila
usumbufu na bila ya kuomba rushwa ya aina yoyote ile.
SEKTA YA WANYAMAPORI
Hifadhi ya Mapori
31.
Mheshimiwa Spika, asilimia 28
ya eneo la nchi yetu limetengwa kwa ajili ya kuhifadhi rasilimali za Taifa
ikiwemo misitu, wanyamapori, na utunzaji mazingira kwa ajili ya matumizi ya
binadamu na viumbe hai wakiwemo wanyamapori ambao wanachangia kwa kiwango
kikubwa katika shughuli za utalii. Changamoto kubwa iliyopo sasa katika mapori
yetu ya hifadhi ni uvamizi wa mifugo, na kwa bahati mbaya kwenye mikoa ya
mipakani, mifugo mingi imekuwa inatoka nchi jirani.
32.
Ili kuhakikisha
kwamba Hifadhi za Taifa na mbuga zetu za wanyamapori zinalindwa kikamilifu.
Mwezi Novemba, 2016 niliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na
Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka
alama za mipaka (beacons) kuainisha
maeneo yote ya hifadhi nchini kwa lengo la kuondoa migogoro iliyopo. Baada ya
kuweka alama hizo, Serikali imeanza rasmi zoezi la kuondoa mifugo yote ndani ya
hifadhi. Aidha, nimeelekeza kwamba, uwekaji wa alama au nguzo hizo uhusishe
Halmashauri za Wilaya na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Ramani zinazoonyesha mapori
zitumike. Aidha, mapori yote yaliyohifadhiwa kisheria yaheshimike.
33.
Mheshimiwa Spika, kufuatia kuwepo kwa migogoro baina ya Wafugaji na Wakulima na migogoro
baina ya wafugaji na wahifadhi wa mapori, nimeelekeza kwamba ifikapo mwisho wa
mwezi Julai 2017 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo yote ya
Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika vitalu (blocks) kwa wafugaji ili mifugo mingi
iondolewe vijijini na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili Serikali iweze kutoa
huduma za ugani za kisasa huko kwenye hizo blocks.
34.
Natoa wito kwa
wafugaji wote nchini kufuata Sheria za Hifadhi za Taifa, Mbuga za Wanyamapori, maeneo
tengefu pamoja na vyanzo vya maji. Mifugo yote itakayokutwa ndani ya hifadhi,
hatua kali zitachukuliwa na kufikishwa mahakamani. Aidha, tukumbuke kuwa ardhi
haiongezeki lakini wafugaji na mifugo vinaongezeka, hivyo ni lazima tufuge
kisasa na tufuge mifugo michache yenye tija ambayo tutaweza kuihudumia katika
maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya ufugaji.
SEKTA YA AFYA
Ununuzi
wa dawa na vifaa tiba
35.
Mheshimiwa Spika; kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza kuhusu umuhimu wa
afya bora kwa wananchi wetu, Serikali itaendelea kutoa
kipaumbele katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa tiba na
vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 236 zikiwa ni fedha za ndani kwa ajili
hiyo. Aidha, Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni
33 kwa ajili ya chanjo za watoto na makundi maalum. Nitoe rai kwa
wazazi/walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazotakiwa ili
kuwakinga na magonjwa na kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye. Aidha, kila mwananchi
ajenge utamaduni wa kupima afya yake mapema ili kubaini
tatizo lake la kiafya mapema, badala ya kusubiri hadi ugonjwa ufike hatua mbaya ndipo aende hospitali.
Vifo vitokanavyo na uzazi
36.
Mheshimiwa
Spika, tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto kubwa katika nchi
yetu. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na
uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Hali hii haikubaliki na
haivumiliki, kwani wanaopoteza maisha ni Watanzania wenzetu, ni mama zetu, ni
wake zetu, ni dada zetu na ni watoto wetu. Tumesikia maoni na michango ya Waheshimiwa
Wabunge kuhusu suala hili wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
bajeti ya Wizara ya Afya na Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa
Fedha na Mipango.
37.
Napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imewasikia na kwa hakika inaguswa sana na vifo vitokanavyo na
uzazi. Ndio maana Serikali imeamua kuongeza fedha
za ndani kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya
ya Mama na Uzazi. Serikali imeamua kwamba, itanunua,
kusambaza na kutoa bila malipo dawa
kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Hii ni pamoja na dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua, dawa kwa ajili ya
kifafa cha mimba na dawa kwa ajili ya kuongeza damu. Jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Vilevile, Serikali imejizatiti kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya afya
na zahanati vijijini pamoja na kuimarisha vituo vyote vya kutolea tiba nchini
kwa lengo la kuboresha huduma za Afya. Hivyo, napenda kuwahakikishia
wanawake wote nchini, kwamba hakuna
mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kwa kukosa dawa/sindano ya kuzuia kuvuja
damu au kukosa dawa ya kuzuia kifafa cha mimba.
SEKTA
YA ELIMU
Kuinua Ubora wa Elimu na Mafunzo
38.
Mheshimiwa
Spika,
kwenye hotuba yangu ya kufungua mkutano wa saba wa Bunge lako tukufu,
unaoahirishwa leo nilieleza kwa
kirefu umuhimu wa watoto wetu kutoa kipaumbele kwa masomo ya sayansi. Nilisema,
endapo watoto wetu hawatasoma masomo ya sayansi, watabaki kuwa watazamaji
kwenye uchumi wa viwanda. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu,
kwamba, Serikali imeanza kutimiza wajibu katika kuweka mazingira wezeshi kwa
watoto wetu kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.
39.
Tarehe 6 Juni, 2017 nilizindua zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara
kwa ajili ya shule za sekondari 1,696 vyenye thamani ya shilingi
bilioni 16.9. Vifaa hivyo
vinaendelea kusambazwa katika shule za Tanzania Bara ambazo zimekamilisha
ujenzi wa maabara. Hivyo, natoa wito kwa wanafunzi kutumia vifaa hivyo kusoma
kwa bidii masomo ya sayansi, na kuvitunza ili vinufaishe wanafunzi wengi zaidi.
Aidha, Halmashauri zote nchini ambazo hazijakamilisha ujenzi wa maabara
zinaelekezwa kukamilisha zoezi hilo mapema, ili vifaa vingine vitakapoletwa
visambazwe haraka.
Elimu Jumuishi
40.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na jitihada za kuinua ubora wa elimu
nchini, Serikali imeendelea kutafuta suluhu ya changamoto za kujifunzia
zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hivi karibuni Serikali imenunua
vifaa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye baki ya usikivu na kuvisambaza
katika shule 213 za msingi na 22 za sekondari. Aidha, Serikali imenunua vifaa vya upimaji ili kubaini watoto wenye
mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa mikoa
yote Tanzania Bara. Rai yangu kwa wazazi wenzangu kote nchini, ni kutumia fursa
hii kuwapeleka shuleni watoto wenye mahitaji maalum badala ya kuwaficha
majumbani. Shabaha ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila
mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa hiyo bila kujali uwezo wake wa kifedha au changamoto za kimwili.
Msimamo wa Serikali kuhusu Ujauzito shuleni
41.
Mheshimiwa
Spika,
moja kati ya mijadala iliyoibua hisia kali wakati wa mjadala wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ni pamoja na kuwaachisha
masomo wanafunzi waliopata ujauzito shuleni. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka
2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha
masomo kutokana na kupata ujauzito. Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata
ujauzito, ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni
za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana
na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi,
kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi
kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki,
kuchimba madini, n.k.
42.
Mheshimiwa Spika, msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito
kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala
sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati. Msimamo huo
wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao
badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Lengo hili pia nalo
ni la kuwaelimisha wazazi kila mmoja aendelee kumtunza binti yake na kuwafundishe
watoto wao mambo mema na maadili mema ndani ya familia. Wazazi wajishughulishe
kikamilifu katika kuweka katazo kwa watoto kujihusisha na ngono wakiwa na umri
mdogo. Dhamira ya Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili
ya manufaa yake na Taifa kwa ujumla. Sote tutakumbuka kaulimbiu ya mke wa Rais
wa awamu ya nne, Mama Salma Rashid Kikwete aliyesema: “Mtoto wa mwenzio ni
mwanao.” Kila mzazi hana budi kujikita kuwalea watoto hawa badala ya
kuwafanyisha vitendo ambavyo havistahili.
43.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata
elimu. Hivyo, ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na
masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito. Serikali imewekeza kwenye mtoto wa
kike. Kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353, kinatoa adhabu ya
miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa ujauzito mwanafunzi. Aidha, sheria
inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Shilingi Milioni 5, au vyote kwa pamoja kwa anayeshiriki kumuozesha
mtoto wa shule. Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa sheria
za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa
Wabunge, mshirikiane na Halmashauri zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito
kwa watoto wa shule. Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya
dola, ili wanaowapa wanafunzi ujauzito au kuwakatisha masomo ili waozeshwe
wapate adhabu stahiki.
SEKTA
YA MAJI
44.
Mheshimiwa
Spika,
katika mjadala wa Bajeti moja ya sekta
ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kwamba inahitaji kupewa kipaumbele
cha pekee ni sekta ya maji. Hakika nakubaliana na mtazamo huo wa Waheshimiwa
Wabunge kwani maji ni uhai na kichocheo cha maendeleo katika sekta
mbalimbali na nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini. Kwa kuwa suala
la maji lilitolewa ufafanuzi wa kina na Mheshimiwa Waziri wa Maji na
Umwagiliaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango,
naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba
tumewasikiliza na tumewasikia. Serikali inayo nia ya dhati
kuhakikisha kwamba vijiji zaidi vinapata huduma ya maji.
UBORESHAJI
WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA NCHINI
45.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali
za Mitaa nchini zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake
kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi
za ugatuaji wa madaraka kwenda katika vyombo hivyo pamoja na kuongeza mgawo wa
fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
46.
Mheshimiwa
Spika, katika
kutekeleza azma hiyo, Serikali katika mwaka
2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya
fedha hizo:-
(i)
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya majengo ya Ofisi na Makazi ya Viongozi katika Mikoa yote mipya.
Katika mgawo huo, Mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; Mkoa wa Katavi umetengewa
jumla ya shilingi bilioni 3.080;
Mkoa wa Simiyu umetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 3.775, Mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na Mkoa wa Songwe
umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812.
(ii)
Aidha,
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni
61.7 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri 64, Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 28.7 ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya Ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni
kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri mpya 20.
Kwa sasa Serikali haina mpango wa
kuanzisha maeneo mapya ya utawala mpaka tukamilishe maeneo tuliyoyaanzisha kwa
kuboresha miundombinu.
(iii)
Sambamba
na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na
Watoto imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
(iv)
Vilevile,
Serikali imeandaa mpango mahsusi wa kuwajengea uwezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata,
Vijiji, Mitaa na Vitongoji ili waweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi katika
kuwahudumia wananchi. Sehemu ya fedha za maendeleo zitatumika kwa ajili ya
kujenga uwezo wa watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
47.
Mheshimiwa
Spika,
juhudi za Serikali za kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina
lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua kero zao katika ngazi
hiyo. Aidha, jitihada hizo zimelenga kuongeza kasi ya maendeleo Vijijini na
kuboresha maisha na ustawi wa wananchi wetu. Kwa msingi huo, natoa wito kwa
Viongozi wa Mikoa na Wilaya pamoja na Halmashauri,
wahakikishe kwamba malalamiko yote ya wananchi
yanatatuliwa haraka katika ngazi husika. Si vyema na haikubaliki kwa wananchi
kusafiri umbali mrefu kutafuta suluhu za changamoto zao kwa viongozi wa Kitaifa
wakati wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo, na zina Viongozi wanaolipwa mishahara kwa fedha za walipa
kodi. Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo yanayotolewa kuhusu
suala hili.
MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya uzalishaji, uuzaji,
usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini. Tumeendelea kubaini mtandao
wa waingizaji wa dawa hizo hapa nchini na kuchukua hatua stahiki dhidi ya
wahalifu hao. Ili kuimarisha mapambano hayo na kuyaendesha kisayansi, Serikali
imekamilisha uteuzi wa watendaji mahiri wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za
Kulevya wanaojumuisha makamishna wanne waliobobea kwenye taaluma zao na wenye
uzalendo na uzoefu mkubwa kwenye mapambano haya.
49.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kifupi tangu mwezi Februari, 2017 Mamlaka hii
ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bhangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini. Aidha,
Mamlaka kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za
kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bhangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na
kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.
50.
Mheshimiwa Spika, dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa
kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono
jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu
watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, naendelea kutoa
rai kwa wazazi wenzangu kufuatilia mienendo ya watoto wetu ili wasijiunge
katika makundi mabaya ya kujihusisha na dawa za kulevya. Itakumbukwa kwamba
waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35,
kundi ambalo ni tegemeo kwa ustawi wa Taifa letu.
51.
Mheshimiwa Spika, Azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa
za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya
yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. Tuungeni mkono
kwenye mapambano haya, ili itokomeze kabisa mtandao huo.
SEKTA YA
MICHEZO
52.
Mheshimiwa
Spika, wakati
vikao vya Bunge hili vikiendelea, tmu yetu
ya vijana walio chini ya umri wa miaka
17, Serengeti
Boys ilishiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Barani Afrika ambapo ilimaliza ikiwa na jumla ya pointi
4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili. Hata hivyo, kutokana na kanuni za mashindano
hayo, Serengeti Boys haikuweza kuendelea na mashindano pamoja na matokeo hayo
mazuri.
53.
Mheshimiwa
Spika, binafsi nilifuatilia mechi zote za
Serengeti Boys nikiri kwamba, vijana hao wana
vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao. Kwangu mimi vijana wale ni
washindi bila hata ya kupewa taji lolote. Naomba nitumie Bunge lako tukufu, kuwapongeza kwa dhati
kudhihirisha kwamba hakuna linaloshindikana tukiamua. Msisitizo wangu kwa TFF ni kuendelea kuwatunza
vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza
kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.
54.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira
kwa vijana wetu. Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa
kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo
miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. Hivyo, tutaendelea
kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia
ufundishaji wa michezo kama somo. Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na
shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za
kufundisha michezo. Nawapongeza sana Walimu wetu kwa kusimamia vizuri michezo
shuleni. Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini,
wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili
kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao,
na walimu wanahimizwa wasimamie michezo mbalimbali shuleni.
55.
Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wadhamini waliodhamini
michezo yetu ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu wa 2017 ambao ni Coca Cola,
LAPF na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa mchango wao mkubwa.
56.
Mheshimiwa
Spika,
nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja
mkubwa wa michezo hapa mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa
rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.
Serikali ya Awamu ya
Tano itaendelea kusimamia michezo nchini na haitafumbia
macho usimamizi mbovu, na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa
vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo. Kwa msingi huo, leo hii naelekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini
kulifanyia mapitio na kutathmini upya Baraza
la Michezo Tanzania (BMT) ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini. Pale
itakapodhirika kwamba usimamizi siyo imara, anayo ruhusa ya kulivunja Baraza
hilo na kuunda Baraza jipya.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba nirejee masuala makubwa
niliyoyasisitiza wakati nafungua Mkutano wa Saba wa Bunge lako tukufu. Masuala
hayo niliyoyasisitiza, ambayo naamini bado yana umuhimu hadi sasa kwa ustawi wa
nchi yetu ni kama ifuatavyo:-
(i)
Moja, tuendelee kulinda na kudumisha amani nchini ili
wananchi washiriki shughuli za maendeleo bila hofu ya usalama wao.
(ii)
Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa
kila mwananchi.
Ni lazima kila mwananchi afanye
kazi kwa bidii na maarifa, alipe
kodi stahiki na afichue wanaokwepa
kulipa kodi.
(iii) Tatu, tujenge
utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kujilinda na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaigharimu sana nchi yetu;
(iv) Nne, tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali
zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi chetu na vizazi
vijavyo;
(v)
Tano, tuzingatie matumizi ya muda, tuongeze nidhamu
na uwajibikaji tuzingatie muda na kupiga vita tamaduni zote zinazohamasisha
uvivu na uzembe; na
(vi) Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi
yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa
wahusika wa dawa za kulevya.
58.
Mheshimiwa
Spika,
nihitimishe hotuba yangu, kwa kuwatakia safari njema Waheshimiwa Wabunge wanaporejea
majimboni kuwaeleza wananchi mambo mengi yaliyojiri hapa
Bungeni hususan kuhusu manufaa ya Bajeti na miswada tuliyoipitisha. Waelezeni wananchi matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga
mkono kwenye jitihada zetu za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua na
umaskini. Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano baina ya Waheshimiwa
Wabunge na Halmashauri zenu, katika ufuatiliaji wa fedha za maendeleo
tunazoleta kwenye Halmashauri, ili zifanye kazi iliyokusudiwa. Aidha, naitakia
maandalizi mema Timu yetu ya Bunge itakayoshiriki kwenye mashindano ya Mabunge
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakayofanyika mwaka huu mjini Dodoma. Tunayo
imani kubwa na Timu yetu, tuwakilisheni vizuri, kama ilivyo kawaida.
59.
Mheshimiwa
Spika,
baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu liahirishwe
hadi tarehe 05 Septemba, 2017 siku ya
Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
60.
Mheshimiwa
Spika, naomba
kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment