Na Atley Kuni - Mwanza.
Jumla ya mizani 3,070 Iliyo Hakikiwa katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa ajili ya
matayarisho ya ununuzi wa pamba kwa msimu wa 2017/2018 imekutwa salama baada ya kuhakikiwa na wakala wa Vipimo nchini.
Akizungumza nami Jijini Mwanza, kaimu Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na
Mawasiliano Bi. Irene John, amesema, Wakala wa vipimo Tanzania ( WMA) chini ya
usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu kwa
wakulima pamoja na kuhakiki mizani itakayotumika kununulia zao la Pamba ikiwa ni
maandalizi ya msimu wa ununuzi wa Pamba kwa mwaka huu.
Wakulima mkoani Shinyanga wakipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Mizani kabla ya msimu kuanza.
Bi. Irene amesema, Dhumuni kuu la utoaji elimu kwa wakulima wa zao la Pamba
Kanda ya Ziwa ni kuwawezesha wakulima kutambua mizani iliyosahihi
(inayoruhusiwa kwa biashara) na ile iliyochezewa (isiyoruhusiwa kwa biashara) ili
waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya
kuuzia Pamba yao, lakini pia ni kuwawezesha wakulima kupata faida ya thamani kamili
ya jasho lao.
Ameongeza kuwa, katika maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi wa Pamba zaidi ya
mizani 1,402 imekaguliwa katika mkoa wa Shinyanga, mkoa wa Simiyu wamekagua
zaidi ya mizani 302, mkoa wa Geita jumla ya mizani 40 tayari imekaguliwa, ilihali
katika mkoa wa Mwanza wamekagua mizani 448, mkoa wa Mara mizani 690, mkoa
wa Tabora wamekagua mizani 164 pamoja na mkoa wa Kagera wamekagua jumla
ya mizani 24 ikiwa ni maandalizi ya ununuzi wa zao la Pamba.
Wakulima mkoani Geita wakipatiwa Elimu.
Katika hatua nyingine Irene amesema, sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo
kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara ikiwa ni pamoja na
kuweka sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa na kukutwa kikiwa sahihi ili
iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara
kwa mwaka husika.
“Wakala wa Vipimo nchini itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza wakati wowote
baada ya msimu wa ununuzi wa Pamba kuanza ili panapokuwa na malalamiko kutoka
kwa wananchi kuhusu uonevu katika mizani yaweze kutatuliwa wa haraka” amesema
Irene
Aidha amewataka wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye
Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja sababu Sheria ya vipimo ipo
na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi wote kwa pamoja hawatakiwi
kufanya udanganyifu wowote katika biashara.
Afisa wa Vipimo Mkoani Kagera akitoa elimu na kuwaonesha wakulima mizani iliyo hakikiwa.
Bi Irene hakusita kutaja faini itakayotozwa kwa wote watakao banika kufanya udanganyifu
“faini itaanzia laki moja badala ya elfu kumi kama ilivyo zoeleka hadi milioni ishirini endapo
mkosaji atakubali kosa, endapo kesi itafikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli
alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa “ na kusema “mshitakiwa atatozwa faini
kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja”.
Irene alisema Tanzania ya viwanda itafanikiwa endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia
matumizi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa
pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao
yenyewe.
Maafisa wa Vipimo wakitoa elimu mkoani Shinyanga.
Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara ili wajue thamani
ya kuuza kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na kumsaidia
mkulima kupata fedha kulingana na thamani ya mazao yake, kufanya biashara ya haki na
kuepusha migogoro/migongano, kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla
Bi. Irene alisema "elimu kwa pande zote mbili (Mkulima na Mfanyabiashara) ni
muhimu lakini zaidi kwa mkulima kwani, mbali ya kutumia muda wake mwingi katika
kuandaa shamba, kulima, kupalilia na hata kuvuna bado ameoneka kuwa mnyonge
kwenye mazao yake ndiyo maana kwa sasa tunazunguka Kanda ya Ziwa mikoa
inayolima Pamba kwa wanunuzi na wakulima kwa ajili ya kutoa elimu ya matumizi
sahihi ya mizani kabla ya uuzaji wa zao la Pamba kuanza.
Meneja wa wakala wa Vipimo mkoani Mwanza akitoa elimu kwa Wakulima na wafanya Biashara.
Afisa huyo amesema kuanzia hatua ya awali ya kuandaa shamba hadi kuvuna mkulima
anahitaji matumizi sahihi ya vipimo lakini wakati wa kuuza mazao, umakini wa
matumizi sahihi ya vipimo unahitajika sana, ambapo kipimo kikiwa sahihi na kikatumiwa
kwa usahihi, kitatoa matokeo sahihi kumwezesha muuzaji (mkulima) kupata fedha sawa
na thamani ya bidhaa aliyouza.
Hivyo, nia na lengo la utoaji wa elimu pamoja na uhakiki mizani ni kuwasaidia
wakulima kabla ya msimu wa Pamba kuanza wapate elimu ya kutosha hatimaye
mkulima aweze kupata fedha kulingana na thamani ya bidhaa atakayoizalisha na
kuwasilisha sokoni. “Mwaka huu tutajitahidi kuongeza elimu zaidi kwa wakulima ikiwa ni
pamoja na kuongeza kaguzi za kushutukiza ili kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara
wasio waaminifu kuchezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima” alisema Kaimu
Meneja Bi Irene.
No comments:
Post a Comment