Tuesday, February 7, 2017

MUHIMBILI YAADHIMISHA SIKU YA KIFAFA DUNIANI WILAYANI MKURANGA

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Leo imeadhimisha siku ya kifafa duniani kwa kutoa elimu ya ugonjwa huo kwa madaktari, wauguzi na wakazi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Madaktari wa Muhimbili wameadhimisha siku hiyo ambayo hufanyika Februari 8 kila mwaka kwa kutoa elimu kwa jamii na wataalamu ili kupunguza vifo kwa watu wenye kifafa nchini.

Rais wa Chama Cha Wagonjwa wa Kifafa nchini (TEA), Profesa William Matuja amesema kwamba ugonjwa huo unatibika na amewataka wakazi hao kuacha imani za kishirikina na badala yake amewataka kuwapeleka wagonjwa hospitali mapema.

“Wengi wana imani potofu kwamba mtu mwenye kifafa, kimesababishwa na mashetani, lakini si kweli kwani karne ya 19 wanasayansi walibaini kuwa mshutuko wa ubongo ndio unasababisha kifafa kutokana na sababu mbalimbali,” amesema Profesa Matuja.


Naye Dk Njenje wa Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema mtu anapata kifafa wakati anapozaliwa endapo ataumia sehemu ya kichwani, kukosa hewa au mtoto kuumizwa kichwani atapata degedege.

“Mtu mzima anaweza kupata degedege endapo sukari yake itakuwa imeshuka sana na ukitibu kisukari anapona,”amesema Dk Njenje.Dk Njenje amesema kwamba ili kubaini mtu ana kifafa, lazima degedege itokee zaidi ya saa 24, degedege itokee zaidi ya mara mbili au mara kwa mara na wakati mwingine inatokea bila mtu kuwa na homa.
Profesa William Matuja wa Chuo Kikuu Kishiriki Cha Sayansi na Tiba (MUHAS) na Rais wa Chama Cha Wagonjwa wa Kifafa nchini (TEA) akiwakumbusha madaktari na wauguzi mambo yanayosababisha kifafa na kuwataka waongeze bidii katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa hao.
Madaktari na wauguzi wakimsikiliza Profesa Matuja leo katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga ambako maadhimisho yamefanyika.
Wakazi wa Wilaya hiyo wakimsikiliza Profesa Matuja leo.
Dk Njenje akitoa elimu kwa wananchi wa Mkuranga kuhusu ugonjwa wa kifafa na jinsi ya kutibu mtu mwenye ugonjwa huo leo.
Dk Yusuf S. Jammagerwalla akizungumza na wananchi wa Mkuranga leo kwamba waache kuhusisha kifafa na imani za kishirikina ili kuokoa maisha ya watu wenye ugonjwa huo. Amewasisitiza kuwapeleka hospitali mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Wakazi hao wakimsikiliza Dk Yusuf leo.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

No comments: