Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dk.Neema Rusibamayila akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa
Mkutano uliowahusiaha Wadau wa Wizara
hiyo na washirika wa maendeleo Maendeleo kutoka Mfuko wa Malkia Elizabeth
unaojihusisha na utokomezaji wa Ugonjwa wa Vikope na wale wa Idara ya Kimataifa
ya Maendeleo (DFID).
Mkurugenzi
Mkuu wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa
Vikope katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania (The Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust Trachoma Initiative) Dk. Aristid
Bonifield akieleza namna Mfuko huo utavyoendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri
katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini leo jijini Dar es salaam.
Mkuu wa
Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania (DFID) Vel Gnanendra akifafanua
namna wadau wa maendeleo walivyojipanga kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha
ugonjwa wa vikope (Trachoma) unatokomezwa nchini.
Mratibu
wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele,
Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es
salaam.
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Sightsavers kutoka Uingereza Dk. Caroline Harper akifafanua
jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope leo jijini Dar
es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Sightsavers kutoka Uingereza Dk. Caroline Harper akifafanua jambo wakati
wa Mkutano wa wadau wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope leo jijini Dar es salaam.
Washiriki
wa Mkutano wa Kutokomeza Ugonjwa wa Vikope kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wale wa
Mashirika ya Kimataifa wakiwa katika picha ya Pamoja leo jijini Dar es salaam.Picha/Aron
Msigwa – MAELEZO.
Na. Aron Msigwa
– Dar es
salaam.
Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa licha ya Tanzania
kuendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Vikope (Trachoma)
jamii bado inalojukumu la kuendelea kuzingatia na kufuata kanuni za afya kwa
kufanya usafi wa mwili na mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Akizungumza leo
jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Wadau wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele wenye lengo la kuutokomeza ugonjwa wa Vikope,
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.Neema Rusibamayila
amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza ugonjwa huo ikishirikiana
na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema kupitia idadi
ya wagonjwa wanaougua vikope imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kupitia afua
mbalimbali chini mpango ujulikanao kama “SAFE” ambao unahusisha huduma za Upasuaji,utoaji wa dawa za
Antibayotiki, kuosha uso pamoja na usafi wa
mazingira.
Ameeleza kuwa wizara kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imeweza kufanikisha upunguzaji wa ugonjwa huo
kwa kutoa dawa/tiba kinga kwa wananchi katika maeneo yaliyoathirika ambapo
amesema kufuatia utafiti uliofanyika mpaka sasa wilaya 22 ugonjwa huo umepungua
sana kiasi cha wananchi wa maeneo hayo kutohitaji dawa za tiba kinga.
Aidha, amesema kuwa juhudi
za sasa ni kuendelea kuwaelimisha wananchi kuendelea kuchukua hatua kwa kufanya
usafi ikiwemo unawaji wa uso pamoja pia kuwaangalia wale waliokwisha kuugua
ugonjwa wa Vikope (Trachoma) ili waweze kufanyiwa upasuaji.
“Baada ya mtu kupata
ugonjwa huu kope za mgonjwa huingia ndani , kope za mtu ambaye hana ugonjwa huu
hutoka nje, zikiingia ndani zinakwaruza jicho na mtu asipofanyiwa upasuaji kope
zake mapema na kuziacha zikaendelea kukwaruza jicho mwisho mgonjwa huyu hupata
upofu” Amesisitiza Rusibamayila.
Amefafanua kuwa
mashirika mbalimbali yamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha zoezi hilo
ikiwemo Shirika na la Msaada la Kimataifa la Uingereza (DFID) pamoja na Mfuko
wa Malkia ya Uingereza (The Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust) ambao umekua
ukitoa fedha kutokomeza ugonjwa wa Trakoma , shirika la Sightsavers, Shirika la
Helen Keller International (HIK) Tanzania pamoja na mashirika mengine yasiyo ya
kiserikali ambayo mengine yapo Kongwa mkoani Dodoma na Kilimanjaro ambao
hushirikiana na wizara kuwatafuta wagonjwa kwa lengo la kutoa matibabu.
Amesema mpaka sasa
kuna wilaya 18 ambazo zinakabiliwa na ugonjwa huo na kufafanua kuwa juhudi za
kuwapata walioathirika zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuwapata wale
walioathirika kwa lengo la kuwafanyia upasuaji na kuwapatia dawa ya tiba kinga
pia kuwaelimisha ili waweze kubadili tabia kwa kuwa wasafi.
“Tunaendelea kuchukua
hatua mbalimbali ikiwemo uelimishaji wa wananchi wa maeneo husika wachukue
hatua, tunajua ugonjwa huu unaletwa na nzi, tunawahimiza wananchi wanawe uso
kuondoa uchafu na kuzuia nzi wanaosambaza ugonjwa huo kutua kwenye macho yao”
Amesisitiza Dk. Dk.Neema Rusibamayila.
Aidha, amewashukuru
wadau hao wa maendeleo kwa kuendelea kutambua mchango wa Tanzania katika
mapambano dhidi ya magonjwa hayo na pia kuendelea kutimiza malengo ya kidunia
ambayo yanaeleza kwamba ifikapo mwaka 2020 Tanzania iwe imeondoa ugonjwa wa vikope
nchini.
Akizitaja baadhi ya changamoto
zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale walioathirika katika maeneo yaliyo na
ugonjwa huo hasa kwenye jamii za wafugaji amesema ni pamoja na hali ya wananchi hao huishi kwa
kuhamahama pia sababu za mazingira hasa miundombinu ya barabara ambayo imekua
kikwazo cha kuzifikia jamii hizo hasa wakati wa kipindi cha mvua.
Kwa upande wake Mratibu
wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Upendo
John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa Tanzania ni
miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo zimekuwa zikinufaika na fedha kutoka
Shirika la Kimataifa la Uingereza na DFID na mfuko wa ulioanzishwa wa kumuenzi
Malkia wa Uingereza kwa miaka 60 ya Utawala wake unaojihusisha na utokomezaji
wa ugonjwa wa Trakoma katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika Tanzania
ikiwemo.
Amesema ugonjwa wa
Vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa Takwimu uko katika wilaya 56 na kueleza
kuwa kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kuanzia mwaka
1990 hali inaonesha kuwa maabukizi yameshuka hasa katika wilaya 22 ambako
wananchi hawahitaji tena ugawaji wa dawa.
Amesema kuwa hali ya
maambukizi katika maeneo hayo imekuwa zaidi kwa watoto na wanawake kwenye
maeneo yenye ukame na shida ya maji ikiwemo mkoa wa Manyara na Dodoma na
kubainisha kuwa mpaka sasa ni wilaya 18 ambazo zinahitaji huduma ya dawa katika
mkoa wa Arusha , Manyara, Dodoma katika wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino.
“Naweza kusema
jitihada tunazofanya ni kubwa na kazi bado ipo hasa maeneo ya wafugaji ambao baadhi
yao wamekuwa wakitumia kifaa Fulani ambacho kinaweza kunyofoa zile kope
zinazowasumbua ili kuondoa usumbufu bila kujua hali hiyo inatengeneza tatizo
zaidi, ni changamoto kwetu, tunahitaji kuendelea kuwaelimisha” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa kupitia
juhudi mbalimbali zilizofanyika wanajiandaa kufanya tathmini katika wilaya
zipatazo 10 katika kipindi cha mwaka huu kuangalia maambukizi yamefikia wapi
kwa lengo la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma na
kupunguza hali ya maabukizi katika wilaya hizo.
Akizungumzia idadi ya
wagonjwa katika wilaya 56 ambazo maambukizi ya ugonjwa huo yapo ilikadiliwa
kwamba kuna maambukizi ya watu takribani 160,000 ambao wameambukizwa tayari
Vikope na kubainisha kwamba kuna mikakati mbalimbali ilifanywa na Wizara kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali kuendesha
upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo hali iliyoshusha kiwango hicho
hadi kufikia wagonjwa 80,000 mwaka huu.
Amesema chini ya
ufadhili wa wadau hao wa miaka 5 wagonjwa takribani 50,000 wenye tatizo la
vikope watafanyiwa upasuaji, huku Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine
ikiendelea kutafuta fedha za kuwafikia wagonjwa 30,000 watakaobaki.
Kwa upande wake Mkuu
wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania (DFID) Vel Gnanendra amesema
kuwa wao kama wadau wa maendeleo wataendelea kuiunga mkono Tanzania kwa
kuhakikisha ugonjwa wa vikope (Trachoma) unatokomezwa nchini.
“Tunafurahia
ushirikiano huu kutoa mchango wetu kuisaidia Tanzania kutokomeza ugonjwa wa
Vikope (Trachoma), kuzuia maumivu na mateso yanayosababishwa na ugonjwa huu
yanayowafanya watu kuangukia katika lindi la umasikini, Tunaiahidi Serikali ya
Tanzania kuwa kupitia ushirikiano huu tutautokomeza ugonjwa huu na kubadili
maisha ya wengi miaka ijayo” Amesisitiza Gnanendra.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Vikope
katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania Dk. Astrid Bonfield CBE
amesema kuwa Mfuko huo utaendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri
katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini.
Amesema Mfuko wa
Malkia Elizabeth utafanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara
ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha kuwa hakuna
mtanzania anayepoteza haki ya kuonakutokana na ugonjwa wa vikope.
" Kwa pamoja tutahakikisha hakuna mtanzania anayepata shida na madhara yanayotokana na ugonjwa wa Vikope, tutafanya kazi na Serikali ya Tanzania tukishirikiana na wadau wengine wa Maendeleo na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali kutokomeza ugonjwa huu" Amesisiza Dk. Astrid.
No comments:
Post a Comment