Wednesday, June 3, 2015

Makampuni, Wachimbaji madini watakiwa kuzingatia Sheria za Mazingira

 Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samwel Sitta (Mb) aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt . Mohamed Gharib Bilal, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani, akimsikiliza  Mhandisi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini Ephraim Mushi wakati alipotembelea banda la Wizara wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea  katika viwanja vya Tangamano jijini  Tanga.
 Wanafunzi kutoka shule za msingi mbalimbali jijini Tanga, wakiangalia madini ya ujenzi wakati walipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea  katika viwanja vya Tangamano jijiji Tanga.
 Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Mhe. Stephen Masele, akiongea jambo wakati alipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Tangamano Jijini Tanga.
Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Innocent Makomba (kulia) akiwaeleza akiwaonesha wananchi waliofika katika Banda la Wizara ya Nishati na Madini madini ya ujenzi  aina  Uranga wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Dunian yanayoendelea katika Viwanja vya Tangamano Jijijini Tanga.
Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samwel Sitta (Mb) aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt . Mohamed Gharib Bilal, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani, akisalimiana na wananchi na watumishi wa sekta mbalimbali baada ya kuwasili katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga kufungua maonesho ya Siku ya Mazingira .

Na Asteria Muhozya, Tanga.

Kampuni za uchimbaji madini, utafutaji mafuta na gesi wakiwemo wachimbaji wadogo nchini, wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira wakati wanapotekeleza shughuli zao, ili kuwezesha rasilimali zinazopatikana  ardhini ziweze kuwa endelevu  kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Rai hiyo imetolewa na   na Mhandisi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ephraim Mushi wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yanayoendelea kufanyika  katika viwanja vya Tangamano  Jijini, Tanga.
Mhandisi Mushi ameeleza kuwa, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania    ni muhimu mahitaji yao yakaenda sambamba na rasilimali zilizopo.

“Nafahamu uelewa wa makampuni ya uchimbaji madini na utafutaji wa mafuta na gesi katika usimamizi na kutunzaji wa mazingira ni mkubwa, kwani tayari  kampuni hizo zina mpango wa usimamizi mazingira ambao umeeleza masuala yanayopaswa kuzingatiwa, lakini bado wanapaswa kuzingatia jambo hili wakati wote kutokana na umuhimu wa wake”, alieleza Mushi.

Kuhusu wachimbaji wadogo ameeleza kuwa, bado wanafanya shughuli zao za uchimbaji bila kuzingatia sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira. “Wachimbaji wadogo bado hawazingatii suala hili lakini Wizara inafanya jitihada mbalimbali za mara kwa mara kuhakikisha wachimbaji wanafuata taratibu ikiwemo kuwaelimisha kuhusu usalama na mazingira”,aliongeza.

 Hivyo, amewataka wachimbaji wadogo kuwa na mpango wa utunzaji mazigira kwa kuwa utaonesha namna ya  kuhifadhi na kutunza mazingira na hivyo kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni husika.

Akieleza zaidi kuhusu jitihada zinazofanywa na wizara katika kusimamia masuala ya   uhifadhi na utunzaji wa mazingira, hususan katika sekta za nishati na madini,  ameeleza kuwa, Wizara imeshatoa mafunzo kadhaa kuhusu masuala hayo kwa maafisa mazingira mazingira wa halmashauri katika Wilaya mbalimbali za  mikoa ya Mwanza, Iringa  na Mbeya kuhusu sheria na kanuni za madini na athari za uchimbaji usiozingatia uhifadhi mazingira.

Vilevile ameongeza kuwa,  wizara mafunzo mengine ni pamoja na mpango kazi wa mazingira wa wizara ambapo maafisa mazingira hao wanatakiwa kuingiza masuala ya madini kwenye mpango kazi yao. Mafunzo hayo pia yanatarajiwa kuendelea kufanyika katika miningine katika mwaka wa fedha ujao.

Aidha, ameeleza  kuwa, wizara imekuwa ikishirikiana na taasisi kadhaa zenye uhusiano wa masuala mazingira kama vile Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira  (NEMC) na wizara nyingine katika masuala yanayohusu  miradi ya nishati na madini jambo ambalo limeleta matokeo mazuri kwa kuwa miradi yote ya nishati na madini haiwezi kuanza   bila kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira.

Siku ya mazingira duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 1 - 5 Juni, ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu  Ndoto Bilioni  Saba. Dunia Moja. Tumia Rasilimali kwa Uangalifu”. Aidha, maonesho hayo yalifunguliwa  rasmi na tarehe 1 Mei,2015, na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samwel Sitta  (Mb)kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt . Mohamed Gharib Bilal.

No comments: