Katibu wa Bunge Dkt. Thomas kashililah akisisitiza jambo wakati alipokutana na ujumbe kutoka taasisi inayojishughulisha na masuala ya kibunge ya Parliamentarians for Global Action Ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Ujumbe huo upo kwenye ziara yao ya kikazi kutembelea kila Bunge Duniani na kueleza malengo na mipango yao hususani kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana na wabunge kutatua baadhi ya masuala yahusuyo haki za Binadamu. Kulia ni Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge Ndg. John Joel, na kushoto ni Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Jossey Mwakasyuka na Msaidizi wa Katibu Ndg. Emmanuel Mpanda.
Katibu Mtendaji wa taasisi ya Parliamentarians for Global Action yenye makao makuu yake Mjini New York Marekani Dkt. David Donat Cattin akielezea baadhi ya shughuli za taasisi yake alipokutana na Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah (hayupo pichani) Ofisini kwake jana Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Kimataifa la Taasisi hiyo Duniani Mhe. Pindi Chana.
Katibu Mtendaji wa taasisi ya Parliamentarians for Global Action yenye makao makuu yake Mjini New York Marekani Dkt. David Donat Cattin akielezea baadhi ya shughuli za taasisi yake alipokutana na Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah (hayupo pichani) Ofisini kwake jana Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Kimataifa la Taasisi hiyo Duniani Mhe. Pindi Chana.
Kikao kinaendelea.
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas kashililah akimkabidhi zawadi Katibu Mtendaji wa taasisi ya Parliamentarians for Global Action yenye makao makuu yake Mjini New York Chini Marekani Dkt. David Donat Cattin mara baada ya kufanya nae mazungumzo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Dkt. Cattin walimtebelea Katibu wa Bunge kwa lengo la kueleza malengo na mipango ya taasisi hiyo hususani kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana na wabunge kutatua baadhi ya masuala yahusuyo haki za Binadamu.
Na Owen Mwandumbya
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Thomas Kashilila, amesema kila Bunge duniani lina wajibu wa kulinda na kutetea haki za Binadamu kupitia utekelezaji wake wa majukumu yake makuu ya Kutunga sheria, Kuisimamia serikali na pia kupitisha bajeti inayozingatiwa mahitaji ya wananchi.
Dkt. Kashilila ameyasema haya jumatatu wiki hii alipokutana na ujumbe kutoka taasisi inayojishughulisha na masuala ya kibunge ijulikanayo kama Parliamentarians for Global Action walipomtembelea Ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya kikazi kutembelea kila Bunge Duniani na kueleza malengo na mipango yao hususani kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana na wabunge kutatua baadhi ya Mmasuala yahusuyo haki za Binadamu.
Awali akielezea majukumu ya taasisi yake, Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo yenye makao makuu yake nchini Marekani Dr. David Donat Cattin alisema taasisi yake kwa kiwango kikubwa hushirikiana na Mabunge Duniani katika kutoa taarifa na kuwahamasisha wabunge dunia kote kutetea haki za binadamu na utawala wa sheria, Demokrasia, usalama wa binadamu, vita dhidi ya ubaguzi, na usawa wa kijinsia kwa kuwa maeneo haya kwa kiwango kikubwa yameigusa karibu kila jamii duniani na hususani watu wa hali chini sana.
Alisema kama taasisi ya kibunge duniani, wanayo kampeni mahusisi iliyozinduliwa mwaka 2013 ambayo kwa kiwango kikubwa imesaidia kutoa elimu na msaada wa kiufundi kwa wabunge na kuongeza utashi wa kisiasa kuunga mkono jitihada za kutetea na kulinda haki za Binadamu duniani kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa kimataifa.
Pamoja na ziara hiyo, Katibu Mtendaji huyo pia alimweleza Kashililah jinsi taasisi yake inavyotafakari namna ambavyo itaanzisha kampeni ya kibunge Duniani kote kupinga sheria ya kifo katika mataifa yote inakotekelezwa sheria hii. Alisema bado wanaangalia namna bora ambayo kwa kushirikiana na Mabunge duniani wataweza kuhamasisha serikali zote duniani kuondoa sheria hii kwa kuwa tafiti zinaonyesha kuwa adhabu ya kifo sio suluhu ya makosa ama vitendo viovu katika jamii.
Akifafanua nafasi ya Bunge katika Jamii, Dkt. Kashililah, alimweleza Katibu Mtendaji huyo kuwa, kila Bunge Duniani lina wajibu wa kulinda na kutetea haki za Binadamu na katika muktadha huo taasisi yake itaungwa mkono na kila Bunge kwa kuwa inalenga kuinua ustawi wa maisha kila Mwananchi jambo ambalo ndio jukumu la Bunge la uwakilishi.
“Wabunge wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kwamba wanatunga sheria zenye kuwawezesha kulinda haki ya kila mtu, hasa wanaoishi katika mazingira magumu zaidi, na katika kusimamia utekelezaji wa sheria hizo” alisisitiza Dkt. Kashililah.
Alisema kutokana na hili, Wabunge wanayo nafasi ya kushirikiana na taasisi hii kikamilifu hasa katika kutoa elimu juu ya kukidhi viwango vya kimataifa katika kutetea haki za binadamu na kulinda haki za watu wote bila kujali kijinsia na matabaka mengine.
Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Kimataifa la Taasisi hiyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Pindi Chana alimwelezea katibu wa Bunge jinsi taasisi hiyo ilivyoweza kusaidia kupambana na baadhi ya sheria kandamizi katika nchi mbalimbali za Afrika na hata Amerika ya kusini kwa lengo kuinua usawa wa kijinisa na uwakilishi wa wanawake katika ngazi za maamuzi.
No comments:
Post a Comment