Afisa kilimo wa mtandao wa kilimo hifadhi barani Afrika (ACTN) Nicholas Johanes (wa kwanza kulia aliyechuchumaa aliyeshika simu) akitoa maelezo kwa kulima(nyuma yake) kuhusu mambo ya kuzingatia wakati wa siku ya wakulima iliyofanyika katika kijiji cha Laela wilaya ya Sumbawanga . Wapili kushoto ni Joseph Mwangono , Afisa kilimo halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga.
Wakulima wakiangalia moja ya shamba darasa Mbeya vijini . Aliyechuchumaa ni Nicholas Johaness, afisa kilimo (ACTN)
Wakulima wakiangalia moja ya shamba darasa Mbeya vijini . Aliyechuchumaa ni Nicholas Johaness, afisa kilimo (ACTN)
Na mwandishi wetu
Mradi wa kutekeleza tija ya uzalishaji katika nyanda za juu kusini umekuwa na mafanikio kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kutumia kilimo hifadhi lakini changamoto kubwa imeonekana ni ukosefu wa masoko .
Mradi huo ambao unafadhiliwa na mtandao wa mapinduzi ya kijani barani Afrika (AGRA )unatekelezwa na mashirika manne katika wilaya sita za mikoa ya Mbeya na Rukwa katika mazao manne kutokana na eneo husika ambayo ni Mahindi , mpunga , Soya na maharage kwa kutumia kilimo hifadhi .
Katika siku ya wakulima iliyofanyika kijiji cha Laela wilaya ya Sumbawanga , Mwenyekiti wa chama cha ushiliki mazao na masoko Laela Amcos Limited bwana Edom Mwaisemba amesema wakulima wamelima kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kuzalisha mazao mengi lakini kinachowakwamisha ni soko .
‘’ Kwa mfano mwaka jana tulipata tani 2,500 lakini tukashindwa wapi tutapata soko . Tunauomba mtandao wa kilimo hifadhi barani Afrika (ACTN) kwasababu umetufundisha jinsi ya kulima na tumelima kikamilifu kwa kufuata kanuni bora na tunaweza kupata hadi tani 3,500 kwa hiyo tunauomba ututafutie soko’’ alisema bwana Mwaisemba .
Bwana shamba kutoka taasisi ya kilimo , biashara tegemezi ya mazao mengi ya mkoani Ruvuma(RUCODIA) bwana Evaresto Joshua amesema kwa kuondoa changamoto ya soko wamekubaliana na mashirika mengine ya mtandao wa kilimo hifadhi barani Afrika (ACTN) , CNV na micro finance limited kuwatumia mawakala wa pembejeo pia kununua mazao .
Changamoto ya matumizi bora ya mbegu pia imejitokeza katika siku hiyo ya wakulima ambapo wakala wa mbegu SEEDCO Tanzania Limited imewashauri wakulima kutotumia mbegu kutoka nje ambazo hazijapimwa na taasisi za ndani ya nchi .
‘’ Tunajaribu kuwasisitiza wakulima kuhusu matumizi bora ya mbegu bora . Lakini zaidi tunasisitiza uagizaji na ununuzi wa mbegu ambazo zinatoka nchi za jirani ziwe zimepimwa na taasisi mbali mbali za nchini mwetu ‘’ alisema bwana Joshua Zuberi , afisa mauzo kutoka wakala wa mbegu SEEDCO Tanzania Limited .
Nao wakulima wamesema kilimo hifadhi kimewasidia kuhifadhi udongo na pia kupunguza gharama za kilimo na kuongeza uzalishaji ikilinganishwa na awali .
‘’ Unakuta mwanzoni heka moja ulikuwa unatumia shilingi 500,000 lakini kwa sasa hivi angalau inapungua hadi shilingi laki mbili . Unaposema kupunguza gharama ni sehemu zote kuanzia uandaaji wa shamba . Kwa mfano kuandaa shamba kunahitaji kutumia moto lakini sasa hivi tunahifadhi udongo tunafukia mlemle ndani ‘’ alisema bwana Ezebius Chapita , mkulima kijiji cha Lula .
‘’ Faida nyingine za mradi huu ni kusogeza huduma ya ugani karibu kwa namna ya kwamba sio kila kijiji kina afisa ugani lakini kutokana na mafunzo haya ya kilimo hifadhi tumeweza kuwasaidia wakulima viongozi kutoa taarifa za ugani kwa wakulima wetu na pale inaposhindikana wanaweza kuwasiliana na sisi kwa kuwasaidia zaidi .’’ alisema Nicholas Johanes , afisa kilimo wa mtandao wa kilimo hifadhi barani Afrika ( ACTN)
Naye Joseph Mwangono , afisa kilimo halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga ambaye alimwakilisha mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Sumbawanga katika sherehe hizo alisema kumekuwa na mafanikio kutokana na wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo
‘’ Kwa upande wa zao la mahindi wengi sasa wanapanda kwa kutumia mistari ,wanatumia mbolea na wanapalilia kwa wakati tatizo tu linakuwa soko la zao hilo la mahindi . Kwa zao la maharage zamani walikuwa wanapanda kwa kumwagilia lakini sasa hivi wanapanda kwa mistari na kutumia mbolea ‘’ alisema bwana Mwangono .
Kanuni za kufuata katika kutumia kilimo hifadhi ni pamoja na kufunika udongo kwa kutumia mazao funika au mabaki ya mazao , kutosumbua udongo na kupanda bila kulima kwa kutumia zana maalum .
Kwa mujibu wa ACTN , mafanikio ya kwanza katika maeneo maalum Tanzania ni pamoja kupunguza mmonyoko wa udongo kwa zaidi ya asilimia thelathini .
No comments:
Post a Comment