Friday, February 27, 2015

MAANDALIZI YA KILIMANJARO MARATHONI YAPAMBA MOTO,KLABU YA RIADHA YA HOLILI YAPELEKA WANARIADHA WAKE MAZOEZINI KENYA

Mkurugenzi wa klabu ya riadha ya Holili (HYAC) Domician Genand akizungumza juu ya maandalizi ya mbio za kimataifa za Kilimanjaro Maratahoni kwa wanariadha wake ambao baadhi yao amewapeleka nchini Kenya kwa ajili ya mazoezi.
Baadhi ya wanariadha walioko katika kambi ya klabu ya riadha ya Holili wakicheza Draft ambapo miongoni mwao yumo mkimbiaji wa Kimataifa ,Osward Levelian ambaye anajiandaa na Mbio za Marathoni kilometa 42 zitakazofanyika nchini Nchina hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Klabu hiyo .Domician Genad akitoa maelezo namna kambi hiyo inavyoendeshwa.
Mwakilishi wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini Dixon Busagaga akifanya mahojiano na mkimbiajiwa kimataifa wa mbio ndefu Osward Levelian anayejiandaa na mbio za Marathoni nchini China.
Baadhi ya wakimbiaji wa kike wakiwa kambini Holili.
Mwalimu wa timu ya riadha ya Holili,Timoth Kamili(mwenye t-shirt nyeusi )akizungumza na mkurugenzi wa klabu hiyo,Domician Genand.

Na Dixon Busagaga,Moshi.


BAADA ya Tanzania kuendelea kufanya vibaya katika mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathoni klabu ya Riadha ya Holili (HYAC) ya mkoani Kilimanjaro imelazimika kuwapeleka wanariadha wake watatu nchini Kenya kwa ajili ya mazoezi ya mbio ndefu za Kilometa 42 .



Hatua hiyo imekuja baada ya wakimbiaji kutoka nchini Kenya kuendelea kuwaburuza wanariadha wa kitanzania katika mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka na kushirikisha mataifa zaidi ya 40 huku zikishirikisha
wakimbiaji zaidi ya 6000.



Akizungumza na Globu ya Jamii mkurugenzi wa Holili Youth Athletics Club ,Domician Genand alisema wanariadha hao ambao wanatarajia kurudi nchini Kesho walienda nchini humo kwa ajili ya kupata uzoefu toka kwa wanariadha wanao shiriki mbio mbalimbali za kimataifa.



“Ninao wanariadha watatu ambao niliamua kuwapeleka nchini Kenya kwa ajili ya kutusaidia ili wafanye mazoezi ya kilometa 42 kutokana na uwepo wa makocha wazuri na wazoefu katika mbio hizo”alisema Genand.



Alisema mbali na wanariadha hao pia wapo wanariadha wengine kutoka katika klabu yake ambao wamekuwa katika mazoezi Mbulu mkoani Arusha na wengine watakao shiriki mbio fupi za Kilometa 21 na kilometa tano wao wamekuwa wakiendelea na mazoezi katika maeneo ya Holili.



Genand alisema klabu yake bado imekuwa na Changamoto mbalimbali licha ya kwamba baadhi ya wafadhili wamejitokeza angalau kupunguza baadhi ya mahitaji kwa wanariadha hao wanaotarajia kushiriki mbio za Kilimanjaro
Marathoni.



“Unapokuwa unaweka mtu kambini kuna mahitaji mengi sana anayokuwa anahitaji,sisi tulijaribu kuandika andiko ambalo linaweza kutubeba katika kipindi hiki cha Kilimanjaro Marathoni na tulikuwa na bajeti ya Sh Mil,5 wapo ambao wametusaidia kama Marenga Investment,Bonite
Bottlers na John Hudson muandaaji wa mbio za Kilimanjaro”alisema
Genand.



Mbio hizo zinadhaniwa kuwa kati ya mbio kubwa zaidi duniani za kitalii na ndio tukio kubwa zaidi la kimichezo Tanzania. Kilimanjaro Marathon ya mwaka huu inatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 wakiwemo
takribani wageni 800 kutoka nchi zaidi ya 40.



Mbio za Kilimanjaro Marathon 2015 zinaratibiwa na Executive Solutions kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Tigo,
GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar,  CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, Kibo Palace Hotel, UNFPA, NSSF, Bodi ya Kahawa Tanzania, na Kilimanjaro Water.

No comments: