Mitaa mbali mbali ya Ilala usafi ukifanywa na wananchi kuunga mkono siku ya uhuru wa vyombo vya habari leo
Na Diana Bisangao wa Francisgodwinblog ,Iringa
WANAHABARI mkoa wa Iringa waungana na wakazi wa kata ya Ilala katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa waadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kufanya usafiri wa mazingira katika kata hiyo ya Ilala inayoongozwa na naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Grevas Ndaki.
Mbali ya wanahabari hao kushiriki kuzoa taka katika eneo hilo la Ilala pia wamefikisha neema kwa wananchi hao wa Ilala baada ya kuwaombea chombo maalum cha kuhifadhia taka (DAMPO) ambacho walikuwa hawana na kulazimika kutupa katakata katika kiwanja cha mkazi mmoja wa eneo hilo.
Wakizungumzia utaratibu huo wa wanahabari Iringa kujitolea kufanya usafi wa mazingira baadhi ya wananchi wa kata hiyo ya Ilala walisema kuwa kilichofanywa na wanahabari hao ni mfano wa kuigwa na kuwa kwani ni kwa mara ya kwanza katika kata hiyo wanashuhudia wanahabari hao wakionyesha mfano wa kushika vifaa vya usafi na kuzoa taka badala ya kuandika pekee.
Alisema Amina Sanga kuwa baada ya kusikia katika vyombo vya habari jana kuwa wanahabari hao wangefika kufanya usafi katika eneo lao wengi wao walikuwa na hamu ya kushuhudia kama ni kweli wanahabari hao watafika kufanya usafi ila baada ya kuwaona wao kama wananchi walifarijika zaidi .
Huku kwa upande wake Husein Ally alisema kuwa changamoto kubwa ya usafi katika eneo hilo ni kukosekana kwa chombo cha kuhifadhia taka na hivyo kuwafanya wananchi kutupa takataka eneo la uwanja wa mtu jambo ambalo kiafya ni hatari zaidi kwani wapo baadhi ya watoto wamekuwa wakishinda katika takataka hizo kuokota uchafu huo na kuchezea.
Hivyo waliomba wanahabari hao kuwasaidia kuwaombea chombo cha kuhifadhia takataka ili kiweke eneo hilo na kila kinapojaa basi gari la kubeba uchafu la Manispaa kufika na kuziondoa mapema.
Katibu mtendaji wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) Bw Francis Godwin alisema kuwa kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Arusha ambapo mwenyekiti wake Frank Leonard amekwenda kuwawakilisha wanahabari wa mkoa wa Iringa ambapo kauli mbinu kwa mwaka huu kitaifa ni Uhuru wa Habari kwa maendeleo na utawala bora .
Godwin alisema kuwa mbali ya kauli mbinu hiyo ya kitaifa mkoa wa Iringa umeongeza kauli mbinu ya pili kwa ajili ya mkoa huo mbali ya ile ya Taifa pia wamejiongezea ile ya uhuru wa vyombo vya habari na usafi wa mazingira ni jukumu letu sote .
Hivyo alisema kuwa kutokana na heshima kubwa ya mkoa wa Iringa iliyopata kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kuwa ya pili kiusafi kitaifa wao wameamua kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhamasisha jamii kufanya usafi katika mji huo .
Pia kujitolea misaada mbali mbali kwa kituo cha Yatima cha DBL Mkimbizi na kuwa suala hilo la usafi katika kata ya Ilala limefanyika kama sehemu ya kuihamasisha jamii kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao .
Aidha aliomba uongozi wa Manispaa kuunga mkono jitihada hizo kwa kuweka Dampo eneo hilo la Ilala ili kuwawezesha wananchi hao kuwa na sehemu ya kuhifadhi takataka.
Afisa msimamizi wa wahudumu wa usafi katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Aron Mafumiko mbali ya kuwapongeza wanahabari hao kufika kufanya usafi pia alikubali kuweka dampo la kudumu eneo hilo la Ilala kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za wanahabari hao mkoa wa Iringa.
|
No comments:
Post a Comment