Hatimaye Wilaya mpya ya chemba Mkoani Dodoma Mwishoni mwa wiki hii imepata Halmashauri yake ya Wilaya iliyoundwa kutoka Halmashauri mama ya Wilaya ya Kondoa iliyoizaa Wilaya hiyo ya Chemba.
Wilaya ya Kondoa iliyokuwa na ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya 13,000 mwaka 2012 iligawanywa na kuizaa wilaya mpya ya chemba ambapo tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo ya chemba chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya Isack Mtinga haikuwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hivyo imekuwa ikihudumiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
Baada ya wilaya ya Kondoa kugawanywa na kuzaa wilaya mpya ya Chemba mwaka 2012, mapema mwezi Mei mwaka huu wilaya hizo (Kondoa na chemba) zilifanya mchakato wa kugawana watumishi, rasilimali na madeni kwenye kikao kilichofanyika chini ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ndg. Rehema Madenge.
Kikao cha mwisho cha pamoja kati ya wilaya hizi mbili Kondoa na chemba kilifanyika mwishoni mwa wiki hii chini ya usimamizi wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi na baada ya kikao hiko kila Halmashauri ya Wilaya sasa imeanza kusimamia nakutekeleza majukumu yake ya msingi.
Akifafanua malengo ya serikali kuigawa wilaya ya Kondoa na Kuanzisha wilaya mpya ya Chemba Mkuu wa Mkoa alisema jambo hilo lilifanyika kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaaisha malengo makubwa ikiwa ni pamoja na kuhimiza na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama na kuwa siyo matarajio ya serikali na wananchi wake kuwa ulinzi na usalama udorore baada ya kuanzisha wilaya mpya.
Vilevile lengo lingine muhimu ni kupeleka madaraka ya kufanya mipango na maamuzi mbalimbali ya maendeleo karibu zaidi na wananchi. Mkuu huyo wa Mkoa alisema anatarajia kuwa Wilaya hizo mbili Kondoa na Chemba sasa zitaongeza zaidi kushirikisha wananchi hasa kwenye masuala ya maendeleo na kwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza demokrasia.
Miongoni mwa masuala ya msingi ambayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi aliwahusia viongozi wa wilaya za Kondoa na Chemba, mabaraza ya madiwani na watendaji wa wilaya hizo ni kuepuka kwa nguvu zote mahusiano ya kuwekana mifukoni baina ya madiwani na wakuu wa Idara za Halmashauri, hii itawafanya washindwe kutekelezwa majukumu yao kwa uhuru, haki na kufuata sheria.
Vilevile Mkuu huyo wa Mkoa allizitaka Halmashauri hizo Mbili za wilaya kuboresha na kuongeza uwezo wa makusanyo ya mapato ya ndani kwa kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato. Aidha kuwajengea wananchi uwezo katika shughuli za uzalishaji ili waweze kuchangia shughuli za maendeleo kama elimu, Afya, maji na sekta zingine.
Alisema kuwa kugawanywa kwa wilaya ya kondoa na kuzaa wilaya ya Chemba kunafanya kondoa kuwa na julma ya wananchi wasiopungua 260,000 na chemba wananchi wasiopungua 230,000 hivyo viongozi na watendaji wahakikishe wanamfikia mwananchi mmojammoja kuhakikisha anaongeza ufanisi katika kilimo na kuacha tabia ya kutegemea chakula cha msaada.
Vilevile kuchangia mfuko wa elimu kwa ajili ya ujenzi wa maabara, madarasa, mabweni na nyumba za walimu. Aidha kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu darasa la saba na kuchaguliwa kwenda kidato cha kwanza wanaripoti shule na kuendelea na masomo ya sekondari.
Mkuu huyo wa Mkoa alimaliza kwa kuzitaka Halmashauri hizo mbili za Wilaya Kondoa na Chemba kuheshimu mgawanyo wa watumishi na rasilimali walizogawana, kuzitunza na pia kuhakikisha wanalipa madeni yote ambayo pia waligawana.
Akiwakilisha madiwani wa wilaya za Chemba na Kondoa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa mheshimiwa Hamis Mwenda alisema mawaidha ya Mkuu wa Mkoa watayachukulia kama dira katika utendaji wao, inawabidi washirikiane viongozi na watendaji ili wapige hatua katika shughuli za maedneleo.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya changamoto hazitakiwi kuwakumba kama vile ukosefu wa chakula na kutegemea chakula cha msaada kwanza ni aibu kwa wilaya za Kondoa na Chemba.
Nae mbunge wa Chemba (CCM) akiwawakilisha wabunge wenzie wa Kondoa na Chemba Mheshimiwa Juma Nkhamia aliomba serikali ya Mkoa kushirikiana na halmashauri hizo mbili kwenye nyanja za usimamizi wa utekelezaji miradi ya maendeleo kama mradi wa maji wa Ntomoko ambao serikali tayari imeshaanza kuutolea fedha za utekelezaji, vilevile alitaka tabia ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ile iliyokwisha kutengewa fedha unaofanywa na baadhi ya watendaji na wasimamizi ikome mara moja.
No comments:
Post a Comment