MKUU WA MKOA
Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu walioko
katika mkoa huo kujihoji nafsi zao na kutathimini matendo yao kama kweli ni ya
kumpendeza Mungu kwa vile ndiyo yanachangia wao kutotambua umuhimu wa nafasi
walizonazo.
Dk. Nchimbi
ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia maelfu ya wanavyuo
waliohudhuria Jumuiko la Wanavyuo wa Dodoma (Dodoma Campus Night)
lililoambatana na mkesha wa kusifu na kuabudu uliofanyika kwenye ukumbi wa
Chimwaga mjini Dodoma.
Jumuiko hilo
lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya 3,500 wa dini mbalimbali kutoka vyuo vikuu
vya Dodoma (UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo
cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu vya Mtumba na Capital.
Dk. Nchimbi
alisema wanavyuo wengi ambao walifaulu kidato cha sita kwa alama za juu (first
class) huwa wanaporomoka kimasomo wanapoingia kwenye vyuo vya elimu ya juu kwa
sababu hawajiweki sawa kwenye mahusiano yao na Mungu aliyewaumba.
“Wanaharibikiwa kwa sababu hawajiweki sawa na Mungu... hawakai pale ambapo
Mungu anataka wawe (their right position),” alisema.
“Tunzeni
nafasi zenu ambazo Mungu amewapatia... wingi wenu huu katika usiku wa leo hauna
maana kama hatutakuwa na uhusiano mwema na Mungu kwani hata shetani ana watu
wake na huwa anawapatia mahitaji yote... kila mmoja wenu aanze upya na Mungu”,
alisema.
“Tumfikirie
Mungu, tuangalie mahusiano yetu na Mungu wetu yakoje na tumuombe atusaidie
katika yote tuyatendayo, naye atatujibu kwa sababu Mungu huwa hawekezi kwa
hasara bali huwekeza kwa faida,” alisema huku akishangiliwa na wanafunzi
waliokuwa wamefurika kwenye ukumbi huo.
Alisema
idadi kubwa ya wanavyuo wakishapata fedha za mkopo hutumbua maisha kwenye
vilabu vya muziki ambavyo ni maarufu mjini humo kama vile Club 84, Club La
Aziz na Maisha Club na hawarudi vyuoni hadi fedha yote imekwisha.
“Mungu alipofanya uumbaji alisema kila alichokifanya ni chema sana. Sasa
kama wewe ni kiumbe chema wa Mungu iweje uende kwenye hizo club kuponda maisha,
iweje unywe pombe, iweje ufanye uzinzi na uasherati badala ya kukaa chuoni
ukasoma, iweje ugome kufanya mtihani hadi upate ‘kibuti’?, alihoji huku
akishangiliwa na wanavyuo hao.
Alisema yeye
kama mzazi analazimika kuyasema hayo kwa sababu anatambua kuwa watoto wa leo
wamezungukwa na mitego mingi. “Hatutaki shetani awachezee, ndiyo maana
tunawaonya,” alisisitiza.
Alisema
katika kundi kubwa kama hilo wamo viongozi wa kesho na kwamba wasipojihadhari
na kuweka mahusiano yao sawa na Mungu kuanzia sasa, watajikuta wanafanana na
baadhi ya viongozi nchini ambao wamekabidhiwa dhamana lakini wanakengeuka na
kufanya kinyume na matarajio ya wengi.
Akitoa mfano
alisema: “Nchi hii wako wasomi wengi lakini wamekaa kiwiziwizi tu, fedha za
barabara zikitolewa haziendi kufanya kazi iliyopangwa, wakurugenzi wakipewa
fedha za kujenga shule, mabweni au nyumba za walimu, unakuta zinakamilika
lakini ziko chini ya kiwango, madaktari nao wanaiba dawa za hospitali kwa kutumia
magari ya kubebea wagonjwa.”
“Kama
viongozi hawa wangesimama kwenye nafasi zao (right position) haya mambo
yangetoka wapi? Mambo ya mikataba mibovu yangetoka wapi? Mnadhani nchi hii
ingekuwa maskini? Haiwezekani!” alisisitiza huku akishangiliwa na wanavyuo hao.
Aliwasihi
wanavyuo wote watambue nafasi zao na wazitunze nafasi hizo ili wasimkosee
Mungu. “Tunzeni nafasi zenu mlizopewa na Mungu na wakati wote jitahidini
kusikiliza sauti yake, muone jinsi atakavyowashindia”, alisema.
Mapema, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa
kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Gerald ole Nguyaine wa Kanisa la ICC
–TAG Dodoma alisema wanafunzi walio katika vyuo hivyo ni wababa na wamama wa
kesho hivyo hawana budi kumtanguliza Mungu katika yote wayafanyayo.
Naye Mchungaji Gavin Walker kutoka
Kanisa la Calvary Christian Fellowship lililoko Columbus, Ohio, Marekani ambaye
alikuwa mnenaji mkuu katika mkesha huo, aliwasihi wanavyuo kutambua makusudi ya
Mungu ambayo ameyaweka juu yao. “Mungu amekuumba wewe kwa kusudi maalum hivyo
ni lazima ujue hilo kusudi”, alisema.
Alisema kwa
kutotambua kusudi la Mungu katika maisha yao, wako watu ambao wamejikuta
wakitaka kufanana na wengine bila kujua ni kwa nini watu hao wamekuwa hivyo.
“Wanatamani nafasi za wengine kwa sababu tu wao ni maarufu, ni waigizaji, ni
wacheza sinema ama wasanii... hapana! Kila mmoja anatakiwa kujua kusudi ka Mungu katika
maisha yake,” alisisitiza.
Alisema duniani kuna wakazi zaidi ya bilioni saba lakini wengi kati ya hao
wanaishi maisha yasiyotimilika kwa sababu hawamjui Mungu. “Hakuna kitu ambacho
Mungu hawezi kukifanya maishani mwetu, tunachotakiwa ni kumuomba tu! Kama ni
masomo soma kwa bidii huku ukimtumaini Mungu, nawe utashinda sababu Mungu yuko
upande wako,” alisisitiza.
Aliwaasa wawe wavumilivu wawapo vyuoni. “Katika maisha ya chuo jifunze kuwa
na saburi. Ukijenga
saburi sasa hivi tangu uko chuoni, itakusaidia kuvumilia mengi katika maisha ya
mbele baada ya kuhitimu Chuo Kikuu au chuo chochote unachosoma sasa,”
alisisitiza.
No comments:
Post a Comment