Wednesday, June 13, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Shirika la Under The Same Sun linasikitika na kufadhaishwa na mauaji ya mwanaume asiyetambuliwa kati ya umri wa miaka 25 hadi 35 mwenye albinism yaliyofanyika katika kijiji cha Nambala, Kata ya Kikwe, Tarafa ya Mbughuni, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha kati ya tarehe 19 na 22 Mei 2012.

Unyama huu umekithiri kiasi kwamba wauaji hata hawakuusetiri huo mwili baada ya kuukata kata na kuondoa viungo vyake mbali mbali. Mwili ulikutwa mtupu na suruali iliyovuliwa hadi kwenye vifundo vya miguu katika mto Nambala kilomita zipatazo 40 hivi kutoka Mererani. Viungo vilivyonyofolewa ni pamoja na mikono yote, masikio, ulimi, ngozi ya usoni, sehemu ya makalio, sehemu yote ya nyeti zake na nywele za kichwani. Mwili huo uliachwa kifudi fudi juu ya jiwe ndani ya mto wenye kina kifupi.
Mtu huyu bado hajaripotiwa na ndugu zake kwamba amepotea na pia hajatambuliwa na mtu yeyote yule. Mabaki ya mwili wake ulioharibika vibaya yamehifadhiwa kwenye hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru. T-Shirt ya rangi ya bluu iliyoiva imekutwa karibu na mwili huo pamoja na sahani nyeupe ya udongo. UTSS inatoa mwito kwa Watanzania wenye ndugu, jamaa na marafiki wenye albinism kuangalia kama wamepotelewa na mpendwa wao.

UTSS inalaani vikali vitendo vya ukatili na vya kinyama vya mauaji na majaribio ya mauaji vinavyofanywa kwa watu wenye albinism nchini. Katika kipindi cha Machi hadi Juni mwaka huu 2012 kumeripotiwa matukio sita ya uhalifu dhidi ya binadamu unaotishia maisha ya wenzetu wenye hali hiyo ya kurithi.

Katika matukio hayo sita yaliyoripotiwa matukio mawili ni vifo, matatu ni majaribio ya mauaji na moja ni utekaji nyara. Hali hii inaashiria kwamba, wimbi la mauaji dhidi ya watu wenye albinism na ukataji viungo vyao nchini Tanzania bado linaendelea na juhudi za makusudi zinahitajika kukabiliana na tatizo hili.
Matukio haya ya kinyama yamesababisha UTSS kuchukua hatua hii ya kutoa taarifa rasmi kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na viongozi wa serikali na wale wa kisiasa, wa kidini na wale wa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kwa pamoja na wa nguvu zetu zote, tukomeshe ukatili huu hapa Tanzania. Shirika linatoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete kulivalia njuga suala hili na kuhakikisha kwa hali hii inakomeshwa kabisa.
UTSS ina wasi wasi kwamba matukio mengi huenda yanatokea bila kuripotiwa na pia watu wanaouawa hawatambuliwi na ndugu zao. Kuna mifano mingi ya aina hii, ikiwa ni pamoja mtu mwenye alibinism ambaye mkono wake uliokotwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi huko Zanzibar na mwanaume mwenye albinism aliyekutwa ameuawa na viungo vyake kunyofolewa huko Lindi.
Tukio la jingine ni lile lililoripotiwa na gazeti la Daily News toleo la Juni 12 2012 ambapo polisi inawashikilia watu wanne tangu tarehe 7 Juni 2012 kwa tuhuma za kufanya jaribio la kutaka kumwuua Harubu Nuru mwenye albinism katia wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera.

Tukio la tatu lililotokea katika kijiji cha Nyamwala, Kata ya Nyakatimbi Karagwe, Mkoani Kagera tarehe 17 Mei, 2012 ambapo mtoto mwenye albinism wa umri wa miezi 21 Agneta Dionizi amenusurika kifo baada ya wauaji wasiyojulikana kuvamia nyumba yao usiku. Katika kiza hicho, wauaji walinyakua na kukimbia na mtoto wa kaka yake Agneta anayeitwa Leti Amenius Dionizi asiye na albinism mwenye umri wa miaka 3 na miezi 8. Mwili wa Leti uligunduliwa tarehe 26 Mei, 2012 na watoto waliokuwa wakitafuta kuni msituni ukiwa umenyofolewa viungo.

Tukio la tano ni jaribio la kutaka kumkata mikono binti mwenye albinism aitwae Beatrice Sospeter Leme, aliyekuwa akisoma kidato cha III shule ya Sekondari ya Busia, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga. Msichana huyo alinusurika kutendewa ukatili huo tarehe 23 Machi, 2012 pale alipokutana na watu wawili wakiwa katika pikipiki ambao walimtaka asimame na asalimishe mikono yake kwao ili waikate na kuipeleka kwa mganga wa kienyeji.

Tukio sita ni la kutekwa nyara kwa mtoto wa kiume mwenye albinism anayedhaniwa kuwa ametokea Tanzania. Mtoto huyo mwenye umri unaokadiriwa kuwa ni miaka mitatu (3) alionekana uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nairobi nchini Kenya akisafirishwa kutoka Tanzania na watu watatu wenye asili ya Kiafrika wanaozungumza Kifaransa wakielekea Burkina Faso.

UTSS inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vyombo vya habari na jamii katika kufichua maovu haya na pia mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinawatia nguvuni wahalifu wanaohusika na ukatili huu.

Tunasikitishwa na maovu haya na hivyo tunaitaka serikali na jamii kwa ujumla wake kushirikiana ili kuhakikisha usalama wa raia zake wote bila kubagua kwa kuwa nchi hii ni nchi yetu wote.

Tunatoa wito kwa polisi wa Mkoa wa Arusha kwenda katika eneo la tukio ambayo mwili wa mtu mwenye ulemavu wa ngozi ulikutwa wakachukue fulana na sahani nyeupe ya udongo vilivyoachwa kwenye eneo la tukio viwe sehemu ya ushahdi wakati wanaendalea na uchunguzi wao katika kuwasaka wauaji. Polisi na viongozi wa serikali wa Arumeru wahakikishe kuwa wananchi wote wanapata taarifa hii na wachukue hatua za makusudi kupitia wajumbe wa nyumba kumi kumi au wenyeviti wa vijiji kuhakikisha kuwa wananchi wao wenye albinism hawajapotea.

Tunachukua fursa hii kuiomba serikali kupitia sekta zake mbalimbali kama vile sekta ya ulinzi na usalama, afya, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii,elimu pamoja na wadau wengine kukaa kwa pamoja na kuweka mpango mkakati madhubuti wa kitaifa ambao utaainisha changamoto na matatizo ambayo watu wenye albinism wanapata na kutoa mwelekeo na njia za kukabiliana na changamoto hizo.

Tunatoa wito kwa ndugu jamaa na marafiki na jamii ambamo watu wenye albinism wanaishi kuwalinda watu hao na kutoa taarifa mapema katika vyombo vya usalama pindi wanapohisi kuna hali ya hatari na vitisho au wanapoona wamepotea au kutoonekana na waachane na dhana potofu kuwa watu wenye albinism huwa hawafi ila wanapotea.

UTSS inatoa changamoto kwa wanasiasa na viongozi wa serikali wote kama kweli hawaamini ushirikina, uchawi na hawaamini na kuwatumia waganga wa kienyeji warejeshe amri ya kupiga marufuku shughuli za waganga hao wengine wanajiita waganga wa jadi, tiba asilia na wa kiutamaduni iliyowekwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Januari mwaka 2009. Baadhi ya hawa waganga wanaendelea kusababisha mauaji ya watu wenye albinism nchini Tanzania.

Swali linaloulizwa na UTSS ni kwa nini mauaji haya na vitendo hivi vya kinyama dhidi ya watu wenye albinism vimeachwa viendelee? Mbona uchunaji ngozi ulikomeshwa? Mbona mauaji ya wenye vipara, wenye mwanya na wasichana bikira waliokuwa wanakatwa sehemu zao za siri na matiti yao yalikomeshwa haraka sana?

Taarifa hii imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Under The Same Sun
Dar es Salaam, 13 Juni 2012

No comments: