Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana kwa siku mbili kuanzia tarehe 23-24 Novemba, 2011 mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na mambo mengine imeazimia yafuatayo:
UNUNUZI WA MAHINDI
I. Halmashauri Kuu ya Taifa imeipongeza Serikali kwa kuwa na mkakati wa kutafuta fedha haraka kwa kuamua kuuza mahindi tani 80,000 kwa UNFP na nchini Kenya ili kwanza, kulipa madeni ya wakulima, na pili, kununua mahindi ya wakulima yaliyopo majumbani na kwenye vituo vya ununuzi kabla ya upandaji wa msimu mpya haujaanza.
II. Imeipongeza pia Serikali kwa kuruhusu uuzaji wa mahindi nje ya nchi, hali ambayo itasaidia mahindi yaliyobaki kwa wakulima kupata soko. Hata hivyo, imesisitiza kuwepo na tahadhari sasa na siku zijazo, ili chakula chote kisiuzwe nje ya nchi na kusababisha tatizo la njaa nchini.
III. Imeitaka Serikali iimarishe Wakala wa Chakula wa Taifa kwa kuuwezesha kwa fedha zaidi na kujenga maghala mengi na makubwa zaidi ili uweze kununua kiasi kikubwa cha mazao.
IV. imeiagiza Serikali ihimize kuundwa kwa Vyama vya Ushirika vya Mazao ya Chakula, ambavyo navyo viwezeshwe kujenga maghala ya kuhifadhi nafaka katika maeneo yao pamoja na kuanzisha mfumo wa ununuzi wa mazao wa stakabadhi ghalani.
MJADALA WA KATIBA
- Halmashauri Kuu ya Taifa imewataka wananchi na wanachama wa CCM kuelewa, kutambua, na kuamini kwamba Katiba mpya pamoja na mchakato wa kuipata, ni kwa manufaa ya nchi. Imewataka Wabunge na viongozi wengine wa ngazi zote nchi nzima kuwaelewesha wananchi si tu maudhui yake, bali hata faida zake.
- Imeiagiza Serikali, pamoja na/au kupitia Tume ya Kukusanya Maoni, iweke msukumo wa kutoa elimu kwa umma wakati wote kuhusu jambo hili na mchakato mzima ili kuzuia upotoshaji unaofanywa kwa wananchi kuhusu mchakato mzima wa kupata Katiba mpya.
- Imeitaka Serikali ihakikishe hakuna Chama chochote cha siasa, mtu, kikundi cha watu au taasisi yoyote ikayotumia mchakato wa kupata Katiba mpya kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani. Vyombo vya Usalama viwe imara katika kuhakikisha kwamba Sheria za nchi zinafuatwa na wanaochochea vurugu wanachukuliwa hatua kali bila kujali nafasi zao.
Aidha, imempongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam kwa ufafanuzi na maelezo fasaha kwa mambo makubwa na ya msingi yanayolikabili taifa letu.
NISHATI YA UMEME NA MAFUTA NCHINI
I. Halmashauri Kuu ya Taifa imeipongeza Serikali kwa kutengeneza mpango wa umeme wa dharura, licha ya gharama kubwa, lakini umesaidia kuleta nafuu katika uzalishaji umeme na kupunguza kero kwa wananchi. imeitaka Serikali kutoa taarifa sahihi kwa wakati kuhusu mgao wa umeme na maeneo yanayoathirika ili kupunguza lawama kwa Serikali.
II. Aidha imeitaka Serikali kuongeza jitihada za kuzalisha umeme kwa vyanzo vingine, hasa makaa ya mawe ambayo yapo nchini na umeme wake ni nafuu.
III. Halmashauri Kuu ya Taifa imepongeza pia jitihada za Serikali kusambaza umeme nchini, ambapo sasa karibu kila Makao Makuu ya Wilaya yana umeme. Hata hivyo, imeitaka Serikali, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), iongeze kasi ya usambazaji umeme vijijini ili kufikia lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM la asilimia 30 ya kaya zote nchini kuwa na umeme ifikapo mwaka 2015.
IV. Imepongeza jitihada za Serikali za kutafuta fedha (dola za Kimarekani takriban bilioni 1) za ujenzi wa bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambalo litawezesha kuongeza uzalishaji wa umeme na kuondokana na matumizi ya mafuta kuzalisha umeme. Aidha, Serikali iharakishe taratibu zote za upatikanaji wa fedha hizo ili utekelezaji wa mradi huo uanze mara moja.
UPANGAJI WA BEI ZA NISHATI YA MAFUTA.
I. Kutokana na umuhimu wa nishati ya mafuta kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu, Halmashauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali kuhakikisha kwamba EWURA inao uwezo, utaalamu na weledi wa kuisimamia sekta hii ipasavyo. Aidha imeipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuwa na hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta, na wa kuanzisha Kampuni ya Mafuta ya Taifa kwa sababu itasaidia kuziba pengo pale linapotokea tatizo la hujuma kwa waagizaji wa sekta binafsi.
UCHANGISHAJI FEDHA KWA AJILI YA KUPITISHA BAJETI
Halmashauri Kuu ya Taifa imeipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuipokea taarifa ya Kamati Teule ya Bunge na kuahidi kuifanyia kazi.
VURUGU KATIKA MIJI NA MAENEO MENGINE NCHINI.
- Kumejitokeza wimbi la vurugu katika maeneo mbalimbali hapa nchini hasa katika majiji yetu. Majiji ambayo hivi karibuni yameripotiwa kutokea vurugu zikifanywa zaidi na vijana ni Mwanza, Mbeya na Arusha. Kutokana na hali hiyo, Halmashauri Kuu ya Taifa, imeitaka dola kuchukua hatua thabiti na za haraka kudhibiti vitendo vya hujuma na uharibifu kwa mali za Watanzania. Imesisitiza kuwa Kusiwepo kabisa na uvumilivu kwenye uvunjaji wa amani kwa kisingizio cha kudai haki. Viongozi wa vyama vya siasa wanaojihusisha na vitendo vya uchochezi na hujuma wachukuliwe hatua za kisheria bila kuogopwa.
- Hata hivyo, Halamshauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali kuharakisha kutatua matatizo yanayowakabili vijana wa mijini, hususan tatizo la ajira na maeneo ya kufanyia biashara zao ndogo ndogo. Imeitaka kuuangalia upya mfumo wa elimu nchini ili vijana wengi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne wawe na stadi za ufundi zitakazowapa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa. Vile vile, mpango wa kujenga shule za ufundi kwenye kila wilaya uliomo kwenye llani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015 utekelezwe haraka.
MIGOGORO VYUO VIKUU NA TAASISI ZA ELIMU YA JUU
I. Halmashauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali ihimize utawala bora katika menejimenti za baadhi ya vyuo vikuu vya umma kama moja ya jawabu la kupunguza malalamiko, migogoro, migomo na vurugu katika baadhi ya vyuo.
II. Imeitaka Serikali kutekeleza Sheria yake ya kupiga marufuku harakati za siasa na uvaaji wa sare za vyama katika maeneo ya vyuo (Campuses). Wafanyakazi wa vyuo na wanavyuo wanaopenda kujihusisha na harakati za siasa basi wafanye hivyo nje ya maeneo ya vyuo. Hii itawafanya jamii ya wanavyuo kutoingilia shughuli za masomo na mipango ya vyuo.
III. Imeiagiza Serikali kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya migogoro na malalamiko hasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma na ichukue hatua muafaka kurekebisha hali hiyo.
MIGOGORO YA ARDHI
I. Halmashauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali ihakikishe kwamba katika uwekezaji unaohusisha umiliki wa maeneo makubwa ya ardhi, wananchi wasiporwe au kudhulumiwa au kushurutishwa kuhama kwenye ardhi yao bila fidia stahiki.
II. Iwahamasishe pia wawekezaji waliopewa maeneo ya kulima mashamba makubwa kusaidia wakulima wadogo walio karibu na mashamba hayo makubwa kuinua kilimo chao.
III. Kuhakikisha uongozi wa Serikali katika ngazi zote kushughulikia kwa haraka migogoro ya ardhi nchini ili kupunguza kero kwa wananchi.
IV. Imeipongeza Serikali kwa kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, ambayo kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo imesisitiza jitihada ziendelezwe serikali katika kupanga matumizi ya ardhi, hasa kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji ili kuepusha muingiliano ambao husababisha migogoro.
KUZAMA KWA MELI YA MV SPICE ISLANDER I TAREHE 10/09/2011
I. Kutokana na maafa yaliyotokea tarehe 10 Septemba, 2011 ya kuzama kwa meli ya Spice Islander I, Halmashauri Kuu ya Taifa imezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua thabiti na za haraka ilizochukua katika kipindi chote cha maafa na msiba huo na hata baada.
II. Imewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dr. Ali Mohammed Shein kwa kutoa uongozi thabiti na kuongoza katika kuwafariji na kuwatuliza wananchi wa visiwa vya Zanzibari na Watanzania kwa jumla katika kipindi chote cha msiba huu.
III. Halmashauri Kuu ya Taifa, pia imewashukuru watu binafsi na taasisi mbalimbali zilizoshiriki kwenye zoezi la uokoaji na zilizochangia kwa hali na mali, kwa fedha na vifaa, katika msiba huu. Vilevile, imewashukuru na kuwapongeza wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba waliojitolea kushiriki kwenye zoezi la uokoaji.
IV. Kwa kuwa tayari Tume imeundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi, Halmashauri Kuu ya Taifa imewataka wananchi wasubiri na waiache ifanye kazi yake kwa uadilifu na kwa muda uliopangwa na kuhakikisha kuwa mapendekezo ya tume hiyo yanafanyiwa kazi.
V. Imeiagiza pia Serikali kuendelea na jitihada zake za kurahisisha usafiri wa abiria kati ya Unguja na Pemba na kati ya visiwa hivyo na Tanzania Bara ikiwemo nia yake ya kununua meli zake.
UTEKELEZAJI WA MAAMUZI YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA KUHUSU VIONGOZI WANAOTUHUMIWA.
Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya kuyatafsiri maazimio yake 27 ya tarehe 10-11 Aprili 2011, na kupokea taarifa ya utekelezaji wa azimio la “Viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama, wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa”.
Katika kutekeleza sehemu ya pili ya uamuzi huo, Halmashauri Kuu ya Taifa imeiagiza Kamati Kuu pamoja na kamati za siasa za ngazi zote za chama chetu, kupitia kamati za usalama na maadili za ngazi zao, kuanza mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu zinazohusika za chama, na kwamba zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa.
Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, taarifa za utekelezaji zipelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya chama.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Wilson C. Mukama
KATIBU MKUU WA CCM
1 comment:
KUZAMA KWA MELI YA MV SPICE ISLANDER hakuna preventive measures ya kuzuia isitokee tena ikiwamo kuwawajibisha wakuu wa wizara husika na kufanya jitihada za kukagua vyombo vyote vya usafiri majini.
CCM iko tayari kwa tukio jingine kama hili na maoni yatakuwa hayahaya milele na tutazidi kufa milele
Post a Comment