Saturday, September 29, 2018

VODACOM WASAINI MKATABA KUTUMIA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILINO









Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania, Ndugu Hisham Hendi (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Ndugu Waziri Kindamba (wa pili kulia) wakisaini mkataba wa kibiashara leo Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam. Katika makubaliano hayo Vodacom watatumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika huduza za data na sauti maeneo mbalimbali kuboresha mawasiliano. Nyuma ni wanasheria wa makampuni hayo wakishuhudia.










Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania, Ndugu Hisham Hendi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Ndugu Waziri Kindamba (kulia) wakipongezana mara baada ya kubadilishana nakala za mkataba wa kibiashara leo Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam. Katika makubaliano hayo Vodacom watatumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika huduza za data na sauti maeneo mbalimbali kuboresha mawasiliano. Wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Jim James Yonazi akishuhudia tukio hilo pamoja na Ofisa Msimamizi wa Mkongo wa Taifa.




Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Jim James Yonazi (katikati) akizungumzia tukio hilo kwenye hafla hiyo ya kusaini mkataba wa kibiashara kati ya Vodacom na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Kushoto ni Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania, Ndugu Hisham Hendi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Ndugu Waziri Kindamba (kulia) kabla ya tukio la kusaini mkataba wa biashara na Vodacom ya kutumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania, Ndugu Hisham Hendi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Ndugu Waziri Kindamba wakionesha mikataba hiyo mara baada ya kusainishana.
Mh. Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Jim James Yonazi (wa pili kushoto) akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Ndugu Waziri Kindamba (wa pili kulia) mara baada ya kusaini mkataba wa biashara na Vodacom ya kutumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania, Ndugu Hisham Hendi.





Na Joachim Mushi, Dar es Salaam


KAMPUNI ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania leo imesaini mkataba wa kibiashara na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) wa kutumia Huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) utakaowezesha mkongo kusambaza huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini.

Hafla ya makubaliano hayo ya kibiashara imefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo TTCL Corporation imewakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ndugu Waziri Kindamba na Vodacom ikiwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Hisham Hendi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kindamba alisema Vodacom amekuwa mteja wa Mkongo wa Taifa tangu Mei Mosi, 2013 na hadi sasa anatumia huduma za ukubwa wa STM-4 (Jumla 7) na STM-16 (Jumla 9), huku akiongeza kuwa Mkataba mpya uliosainiwa unaongeza viwango vya matumizi ya Mkongo kwa Vodacom kwa STM-16 (Jumla 2) na STM-64 (Jumla 1) wenye thamani ya Shilingi bilioni 25.6 bila VAT.

“..Mkataba wa leo unatufanya sisi NICTBB na TTCL kutambua uzito wa majukumu tuliyokabidhiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa huduma za Mkongo zinaimarishwa ili watoa huduma za Mawasiliano hapa nchini waboreshe huduma zao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema.

“Mkataba wa leo unatufanya sisi NICTBB na TTCL kutambua uzito wa majukumu tuliyokabidhiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa huduma za Mkongo zinaimarishwa ili watoa huduma za Mawasiliano hapa nchini waboreshe huduma zao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” aliongeza Kindamba.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ndugu Hisham Hendi akizungumza katika hafla hiyo alisema unalenga kuboresha huduma za mawasiliano za sauti na data kanda ya ziwa kati kaskazini na mikoa ya kusini ya Tanzania kwa kuwezesha kuleta maendeleo kupitia huduma teknolojia ya mawasiliano.

Alisema Vodacom inatumia mkongo kwa takribani zaidi ya miaka 5 na kwa mwaka huu Vodacom inakodisha mkongo huo ambao miundombinu yake imesambaa kwa urefu wa kilomita zipatazo 7,560 nchini kote kwa kipindi cha miaka 10 kwa thamani ya dola za Kimarekani USD11.2 milioni bila VAT.

“miundombinu ya mkongo wa taifa wa mawasiliano imesambaa katika eneo kubwa kwa urefu na unao uwezo mkubwa wa kuwezesha kurusha mawasiliano ya data kwa ufanisi mkubwa, teknolojia hii itawezesha wateja wa Vodacom kupata mawasiliano mazuri zaidi nchini kote,” alisisitiza Ndugu Hisham Hendi.

Hadi sasa wateja wanaohudumiwa na mkongo wa Taifa wa mawasiliano ni pamoja na kampuni ya TTCL, Vodacom, Tigo, Viettel, Airtel, Simbanet, Zantel, Raha, Smile, Sasakwa, eGA na ISP wengine yanatumia Mkongo wa Taifa kufikisha huduma zao kwa wateja. Mkongo wa Taifa hutumiwa pia na nchi za Afrika Mashariki na eneo la Maziwa makuu yaani Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia na hivyo kuufanya Mkongo huu kuwa na umuhimu wa kipekee kwa mawasiliano.

NAFASI ART SPACE KUSHEHEREKEA MIAKA 10 TANGU KUANZISHWA KWAKE, WAANDAA TAMASHA MATATA DAR

 *Ni leo Septemba 29 ,kufanyika katika ukumbi wao uliopo Mikocheni B kuanzia saa tisa alasiri
*Wasanii maarufu ndani na nje ya nchi kutoa burudani

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
 NAFASI Art Space katika kusheherekea miaka 10 tangu kuanzisha kwake wanatarajia kufanya tamasha kubwa na la aina yake leo kuanzia saa tisa alasiri ambapo wasanii maarufu katika uchoraji, uimbaji na waimbaji wa muziki wa dansi wafanya show kwa mashabiki na wapenzi wa Sanaa ndani na nje ya nchi.
Tamasha hilo linatafanyika katika Ukumbi wa Nafasi Art Space uliopo Michokeni B jijini Dar es Salaam na kwamba hakutakuwa na kiingilio chochote na lengo la kufanya hivyo ni kutoa nafasi kwa mashabiki na wapenzi wa sanaa kufika kwa wingi.
 Akizungumza na Michuzi Blog jana kuhusu Tamasha hilo ambalo limepewa jina la Sanaa Yetu Festival, Ofisa Maendeleo Biashara na Masoko wa Nafasi Art Space Agnes-Senga Tupper amesema katika kusheherekea miaka 10 ya Nafasi Art Space wanatarajia kufanya show hiyo matata ambayo itagusa sanaa za aina zote nchini Tanzania.
Amesema zaidi ya wasanii 19 wa uchoraji, uimbaji , wanamuziki wa dansi ni miongoni mwa watakaotoa burudani kwa mashabiki wao ambao kwa kipindi cha miaka 10 wamekuwa wakiwaunga mkono.
Tupper amefafanua kwamba “Mwaka 2008 kikundi kidogo cha wasanii wa Tanzania walijikusanya na kuanzisha Nafasi Art Space kwa ajili ya wasanii nchini kuwa na sehemu ya kufanya kazi zao, pamoja na msaada kutoka Denmark Embassy, Nafasi Art Space ilianzishwa.Tangu wakati huo, Nafasi imeweza kusaidia wasanii zaidi ya 100 nchini Tanzania kuendeleza na kukuza vipaji vyao .
 “Hii imewapatia wapenzi wa sanaa fursa ya kuona, kujifunza na kufahamu sanaa na utamaduni jijini Dar es Salaam pamoja na nje ya nchi. Hivyo kwa mwezi huu wa Septemba, Nafasi Art Space imekuwa ikisherehekea miaka 10 kwa kufanya matukio mbalimbali ya kisanaa kwa ajili ya umma,”amesema Senga.
 Ametaja baadhi ya matukio ambayo wameyafanya kama sehemu ya kusheherekea miaka 10 ambayo kesho ndio kilele chake ni pamoja na kufanya mkutano na waandishi wa vyombo vya habari, uzinduzi kwa kuchora live soko la Karume, kutembelea Wodi ya Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wameshiriki kwenye kipindi cha Jukwaa la Sanaa pamoja na Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA).
Pia wameshiriki Siku ya Usafi Dunaini kwa kusafisha eneo la Coco Beach, kufanya warsha ya sanaa katika Shule ya Mgulani na Chang’ombe za jijini Dar es Salaam pamoja na uchoraji Graffiti Live Nafasi Art Space.
Senga amesisitiza “Kwa kumalizia tunafanya bonge moja la Festival –Sanaa Yetu Festival .Hivyo Septemba 29 (Jumamosi)  wakati wa Festival hiyo ikiendelea kutakuwa na nafasi ya kuchora T-shirt kwa mashabiki watakao hitaji. Pia kutakuwa na maonesho, uuzaji wa sanaa za uchoraji kutoka kwa wasanii mashuhuri dunia nzima ambao ni wanachama wa Nafasi,”amesema Senga.
Pia amesema baada ya hapo itafuata Show ya wasanii kama vile Muda Africa,  Wamwiduka Band, Wahapahapa Band, Bagamoyo Players, Fashion Show ya Makeke International.Kisha watamaliza na Mfalme wa Kisengeli Mfalme Ninja Na DJ Frank.
“Septemba hii ni fursa kwa Nafasi kusherehekea mafanikio ya sanaa ya kisasa nchini Tanzania kwa kutoa shukrani kwa wafadhili na mashabiki wetu, na kuleta jamii pamoja katika ujenzi wa kizazi kijacho cha wasanii na wapenzi wa sanaa.  Nisisitize hakuna kiingilio na watu wa rika zote wanakaribishwa.Lakini Michango ya tunapokea,”amesema Senga.
Kuhusu mgeni rasmi amesema wanatarjia kuwa na mgeni rasmi katika tamasha hilo ambaye atatoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania hasa kwa kuzingatia ndio wafadhili wakuu wa Nafas Art Space.
Baadhi ya matukio ambayo wameyafanya kama sehemu ya kusheherekea miaka 10 ambayo leo ndio kilele chake ni pamoja na kufanya mkutano na waandishi wa vyombo vya habari, uzinduzi kwa kuchora live soko la Karume, kutembelea Wodi ya Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wameshiriki kwenye kipindi cha Jukwaa la Sanaa pamoja na Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA).
 Michoro mbalimbali ilichorwa na vijana wenye vipaji ikiwa ni sehemu ya maandalizi
 Vikundi mbalimbali vilishiriki kuelekea kilele cha  NAFASI Art Space ambapo leo inatimiza miaka 10 tangu kuanzisha kwake 

Friday, September 28, 2018

SHEREHE ZA KUMUAGA KAMISHNA JENERALI MSTAAFU WA MAGEREZA, DKT. JUMA ALI MALEWA, UKONGA JIJINI DAR ES SALAAM

Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa akiwa kwenye gari maalum akipita katikati ya Gwaride likiwa katika umbo la OMEGA ikiwa ni ishara ya kumuaga rasmi baada ya kustaafu utumishi wake Jeshini tangu Julai 1, 2018. Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Ukonga jijini Dar es salaam leo Septemba 28, 2018.
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa akiwasili katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Ukonga jijini Dar es salaam leo Septemba 28, 2018 kwenye Sherehe za kumuaga rasmi baada ya kustaafu utumishi wake Jeshi tangu julai 1, 2018.
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akipokea salaam ya heshima kutoka kwa Gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake katika Sherehe za kumuaga zilizoandaliwa kwenye Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Ukonga jijini Dar es salaam leo Septemba 28, 2018.
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kumuaga.
Kikosi cha bendera kikipita mbele ya jukwaa kwa mwendo wa pole.
Gadi ya wanaume iliyoundwa na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakipita mbele ya jukwaa kwa mwendo wa pole.
Gadi ya wanawake iliyoundwa na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wakipita mbele ya jukwaa kwa mwendo wa haraka.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, CGP – Phaustine Kasike akiwa na baadhi ya Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wageni mbalimbali waliofika katika Sherehe hizo. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye na katikati ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala.
Askari wa vyeo mbalimbali wakipunga mikono ikiwa ni ishara ya kumuaga na kumtakia kheri Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa(hayupo pichani) katika hafla ya kumuaga iliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Ukonga jijini Dar es salaam Septemba 28, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, Phaustine Kasike (kulia) akimpongeza Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa mara baada ya gwaride rasmi la kumuaga lililofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Ukonga jijini Dar es salaam.
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wakuu wa Magereza Mikoa nchini (wa pili kulia) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi pamoja na familia ya Kamishna Jenerali Mstaafu wa Magereza(Picha zote na Jeshi la Magereza).

RAIS MSTAAFU JK ASHIRIKI MKUTANO WA TOKOMEZA MALARIA DUNIANI

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya  Kikwete ameshiriki katika mkutano wa Baraza la Kutokomeza Malaria Duniani (End Malaria Council) uliofanyika tarehe 26 Septemba, 2018 mjini New York Marekani.
Baraza la Kutokomeza Malaria linaundwa na Wajumbe 9 ambao ni watu mashuhuri katika sekta ya umma na sekta binafsi chini uenyekiti wa Bill Gates. 


Lengo la Baraza hilo ni kuunganisha nguvu za wadau na mataifa duniani kukabiliana na hatimaye kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2030.

MAGAZETI YA LEO IJUMAA SEPTEMBA 28, 2018





















Thursday, September 27, 2018

RAIS MAGUFULI AZINDUA FLYOVER YA MFUGALE ENEO LA TAZARA JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Septemba, 2018 amefungua barabara za juu katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara Jijini Dar es Salaam (Mfugale Flyover) ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo, ikiwemo kwenda na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Mfugale Flyover imejengwa na kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd ya Japan kwa gharama ya shilingi Bilioni 106.7.

Ujenzi wa Mfugale Flyover umehusisha njia 4 za barabara zenye urefu wa kilometa 1, ina uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja, imesanifiwa kuishi kwa miaka 100, ina barabara za pembeni (access roads), njia za waenda kwa miguu, mfumo wa mifereji ya maji ya mvua, taa za kuongozea magari na umezingatia mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuacha eneo la meta 12 katikati ya barabara hizo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa Mfugale Flyover ulioanza tarehe 01 Desemba, 2015 umekamilika mapema kabla ya tarehe iliyopangwa ambayo ni 31 Oktoba, 2018 na kwamba katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari Serikali itajenga Flyover nyingine eneo la Chang’ombe katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.

Kufuatia uamuzi wa Mhe. Rais Magufuli kuwa Flyover ya makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela iitwe Mfugale Flyover, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amesoma wasifu wa Mhandisi Patrick Aron Lipilima Mfugale na kueleza kuwa ameitumikia nchi akiwa Mhandisi kwa miaka 41 ambapo katika kipindi hicho ameongoza katika kubuni na kusimamia ujenzi wa barabara kilometa 36,258 zikiwemo kilometa 9,951 za lami na amebuni na kusimamia ujenzi wa madaraja makubwa na madogo 1,400 yakiwemo madaraja makubwa ya Mkapa (Rufiji), Umoja (Ruvuma), Rusumo (Mara), Kikwete (Malagarasi), Nyerere (Kigamboni, Dar es Salaam), Magufuli (Kilombero) na Sibiti (Simiyu/Singida).

Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa Mfugale Flyover, amewapongeza wakandarasi kwa kumaliza kazi mapema, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa usimamizi wake wa karibu na kwa namna ya kipekee amempongeza Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Flyover hiyo, madaraja na barabara mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Wahandisi wengine na wataalamu mbalimbali hapa nchini kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale wa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa, badala ya kuwa kikwazo kwa kukosa uaminifu na uadilifu ama kutoa ushauri usio na manufaa kwa Taifa.

Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam kama ilivyoahidi, na kubainisha kuwa pamoja na kujenga Flyover nyingine katika eneo la Chang’ombe pia inajenga barabara za juu katika eneo la Ubungo (Ubungo Interchange), inajenga barabara ya njia 8 ya Kimara – Kibaha (Kilometa 19.2) na ameagiza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara uitwao DMDP na ambao umetengewa Shilingi Bilioni 660 uhamishiwe Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA).

Ametoa wito kwa watumiaji wa Mfugale Flyover kuwa makini ili kuepuka ajali zisizo za lazima na ameagiza zifungwe kamera za kurekodi magari katika Flyover hiyo na nyingine zitakazojengwa Jijini Dar es Salaam.

Sherehe ya Ufunguzi wa Mfugale Flyover imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara, Balozi wa Japan hapa nchini anayemaliza muda wake Mhe. Masaharu Yoshida, Wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Seleman Kakoso, viongozi wa dini, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Paul Makonda.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshida ambaye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mzuri alioupata kwa kipindi cha miaka 3 na nusu aliyokuwepo hapa nchini.

Mhe. Masaharu Yoshida amepongeza uongozi mzuri wa Mhe. Rais Magufuli na juhudi kubwa anazozifanya katika kujenga uchumi wa Tanzania na ameahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Septemba, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia  wakati akizindua rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida akipena mikono na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa  baada ya kuzindua rasmi  Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa akimpongeza   Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale  baada ya kuzindua rasmi  Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018. 
Mke wa Rais Dkt. Magufuli, Mama Janeth Magufuli, akiongozana na Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na mwakilishi wa BAKWATA Sheikh Alhad Mussa Salum wakielekea kushuhudia uzinduzi rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida wakisalimia mamia ya wananchi waliofurika kushuhudia uzinduzi rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
 Msafara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  ukipita katika Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam baada ya uzinduzi rasmi leo Septemba 27, 2018.