Tuesday, February 28, 2017

HALMASHAURI YA KAKONKO SHULE ZA KATA ZANG’ARA MATOKEO KIDATO CHA NNE

Lusubilo Joel Ded Kakonko
Na Judith Mhina –MAELEZO
Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko yafaulisha wanafunzi 743 kati ya watahiniwa 784 na kushika nafasi ya Tatu Kitaifa kati ya Halmashauri 178hapaTanzania.
Katika mahojiano maalum na Idara ya Habari MAELEZO Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko Bw Lusubilo Joel Mwakabibi amesema: “Shule za serikali zimeanza kurudisha heshima ya kufaulu kama ilivyokuwa miaka ya 1970 na 1980, mara baada ya matokeo ya kidato cha Nne mapema mwezi huu”.
Mwakabibi ameeleza kuwa Halmashauri hiyo inajumla ya shule           za sekondari 14, kati ya hizo 11 ni za Serikali na 3   za binafsi. Matokeo ya kidato cha nne mwaka huu
Yanaonesha daraja  la  kwanza shule za binafsi ni 10,  pili  35, tatu 40, nne 41 na zilizopata ziro ni 13. Kwa upande wa Shule za Serikali daraja la kwanza 6, pili 47, tatu 149, nne 400 na ziro 38.
 “Siri ya mafanikio yetu ni usimamizi wa karibu na ufuatiliaji shuleni, umoja na mshikamano kati ya Walimu, wazazi, Viongozi wa Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa wilaya; walimu wetu tupo pamoja nao, tunawatia moyo katika kazi ya kufundisha”. Anafafanua Mkurugenzi huyo.
Aidha, Mkurugenzi Mwakabibi amesema mwaka 2016 Halmashauri imeshika na fasiyatatu, Kitaifa katika Halmashauri 178 Tanzania, kwani matokeo ya kidato cha Nne na Pili mwaka 2015, Halmashauri yetu, ilikuwa ya kwanza kitaifa na kuzawadiwa ngao ya ushindi toka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia. Hata hivyo ameeleza kuwa mikakati ya Halmashauri yake ni kurudi namba moja, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote watakao sajiliwa kufanya mtihani wa kufaulu kwa viwango vya juu na kufuta kabisa aibu ya kufeli..
Bw Mwakabibi amesema kati ya watahiniwa 794 wa Kidato cha Nne 743 wamefaulu na wanafunzi 51 tu ndio waliofeli. Shule ambayo imeongoza matokeo ya kidato cha nne ni ya binafsi ya Mtakatifu Thomas More Kibogora iliyotahini wanafunzi 30, mbili za binafsi matokeo yake ya kosa wana shule zetu za serikali na idadi ya wanafunzi ni 55.  Huu niuthibitisho dhahiri kuwa shule za Sekondari za Serikali zenye watahiniwa 709 ambazo ni Kata zimefanya vizuri kama shule za binafsi.
Kuhusu masomo waliyofaulu, Mwakabibi amesema kuwa watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya Uraia (Civics), Historia, Biolojia, Kingereza, Jiografia, na Kiswahili na kubainisha kuwa ufaulu ni matokeo ya uwepo wa walimu wakutosha na wenye uwezo mkubwa wa ufundishaji na kufanya kazi kwa bidii na kujituma
“Ili tuendelee kuwa namba moja, Halmashauri inasimamia walimu katika kazi zao, inawahudumia na kujali mahitaji yao.  Pia, inashirikiana na shule, wazazi, wadau wengine iliwanafunzi wajifunze kwa bidii na vitendo iliwapate maarifa na kutumia elimu yao katika maisha ya kila siku, vilevile halmashauri ipate matokeo bora zaidi”. Amesema Mwakabibi
Mwakabibi alisisitiza kuwa “Mafanikio yetu ya mechangiwa na wazazi, walimu, Ofisi ya Mkurugenzi, Waheshimiwa Madiwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wadau mbalimbali kama Mpango wa Ubora wa Elimu Tanzania EQUIP-T , kwa kuunda Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (Parent Teachers Participation).
“Ushirikiano huu, umesaidia kuwatia hamasa wazazi kushirikiana vizuri na walimu katika zoezi zima la kuchangia chakula, kwa kutoa mahindi kilo tano kila mzazi kwa muhula mmoja”. Alifafanua Mkurugnezi huyo na kuongeza kuwa hatua hiyo imewezesha watoto kuwa na usikivu wakati wa ufundishaji na ujifunzaji  na kuongeza ufaulu”.
Akichangia utoaji wa chakula shuleni Afisa Elimu Sekondari Bw Joseph Mutahaba amesema “Kakonko imefanikiwa kutoa chakula au uji katika shule za Msingi 59 zaserikali”. Huu ni utekelezaji wa agizo la Serikali la wanafunzi kupata chakula wawapo shuleni. Zoezi hili limefanikiwa baada ya kuhamasisha na kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa kuchangia chakula au uji kupitia vikao mbalimbali.
Bwana
Mutahab Alitoa Wito kwa Halmashaurinyinginekuhakikishakuwazianakuwana:“Usimamiziwakaribuwataalumashuleni, kuwajali walimu, kuwapa moyo, kuwasikiliza shida zao, kuwahamasisha wafundishe kwa bidii, ushirikiano wa karibu wa wazazi, walimu na wadau wengine wa Elimu katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji” na kusisitiza kuwa “Haya ni mambo ya msingi sana”.
Tofauti na Halmashauri nyingine ambazo zina shule nyingi za binafsi ambazo hunyanyua viwango vya ufaulu wa Halmashauri hizo lakini kwa upande wa  Kakonko ambayo ina idadi ndogo ya shule za binafsi, shule za Serikali zimesaidia kunyanyua kiwango cha ufaulu hadi kushika nafasi ya tatu Kitaifa katika Halmashauri. Ulinganisho huo umefanywa kwa kupata maelezo ya:
Afisa Elimu Mkoa wa Njombe Bw Halfan Omary Masukira amesema: “Halmashauri ya Mji Njombe shule za binafsi zilizotahiniwa 16; daraja la kwanza 58, pili167,tatu 162, nne 168 naziro 12. Shule zaserikalizipo15 daraja la kwanza 11, pili 61,tatu146,nne584 naziro 105 jumlawatahiniwa 1538” 
Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Kagera Bw Wandare Lwakatare amesema: Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba shule za binafsi zilizotahiniwa 13; daraja la kwanza 133, pili 209, tatu 171, nne 188 na ziro 16. Kwa upande wa Shule za serikali ni 16; daraja la kwanza 24, pili 97, tatu 167, nne 550 na ziro 190 jumla watahiniwa 1757. 
Ukiangalia takwimu za Halmashauri hizo tatu utagundua kuwa shule za Kata za Kakonko zimefanya vizuri kuliko za Kata za Halmashauri ya kwanza na ya pili.  Halmashauri ya kwanza Tanzania katika ufaulu wakidato cha nne ni Manispaa ya Bukoba; kati yawatahiniwa 1757 waliofaulu ni 1542, waliofeli 215 na kupata GPA ya 3. 5414 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Njombe ambayo ilikuwa na watahiniwa 1538 na walifaulu 1418, waliofeli 120 na kupata GPA 3.6453. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ndio iliyoshika nafasi ya tatu ambayo ilikuwa na watahiniwa 794 kati yao watahiniwa waliofaulu ni 743 na waliofeli ni 51 na kupata GPA ya 3.6716. Kakonko ndio Halmashauri yenye wanafunzi watahiniwa wachache zaidi katika Halmashauri kumi bora.
New Picture

WAZIRI MKUU ANUSA MADUDU MINADA YA MADINI

 Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akisisitiza jambo katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo ,kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017. 
 Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo,kwenye makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifafanua jambo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam Februari 27, 2017, kwa ajili ya kujadili masuala ya madini. Watatu kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na  ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Bendera.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Amuagiza Kamishna wa Madini aende Mererani
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini inayofanyika nchini kwa sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.

Amesema ukiukwaji huo unachangia kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada hata kama kuna vito viliyokakatwa au havijakatwa.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 27, 2017) wakati akihitimisha kikao alichokiitisha kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam kilichojumuisha Mawaziri wa Fedha pamoja na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo. 

Alisema licha ya kuwa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili Serikali iweze kunufainika na madini hayo.

“Uzoefu wa kwenye minada ya korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima. Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,” alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa madini na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa bei inapaswa kuwa juu ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.

Amemuagiza Kaimu Kamishna wa Madini, Bw. Benjamini Mchwampaka (ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Madini) aende Mererani na kufuatilia utendaji kazi wa mgodi wa Tanzanite One na suala zima la teknolojia zinazotumika kiwandani hapo.

Waziri mkuu aliitisha kikao hicho kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mererani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara Februari 16, 2017 kwamba akimaliza ziara ya mkoa huo ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite One baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi sasa.

Ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini unaongezeka, Waziri Mkuu amemwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa ndege vya Arusha na Kilimanjaro (KIA),

“Kamishna wa TRA na watu wako inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi zinafanyika kwenye sekta ya madini wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo. Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri waje kuwaletea malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija wakakuta mmetoka ofisini je?” Alihoji Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu uelewa wa sheria miongoni mwa wachimbaji wadogo, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Kamishna wa Madini wanapaswa kutoa elimu na uelewa wa kisheria kwa wachimbaji hao ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kwenye maeneo mengi nchini.

“STAMICO na Kamishna wa Madini fanyeni kazi pamoja, waelewesheni wachimbaji wadogo kuwa uwepo wa vitalu maana yake kuna mipaka ambayo pia inajumisha utoaji wa leseni kwa wenye vitalu hivyo. Kwa hiyo, waelimisheni kuwa mtu hapaswi kwenda upande wa pili wa mtu mwenye leseni, akifanya hivyo atakuwa anavunja sheria.” 

“Ninyi ni wadau wakubwa wa sekta hii kwa hiyo mnapaswa kushiriki katika zoezi la kutoa elimu. Mnayo maeneo mengi ya uchimbaji lakini yana migogoro, mfano ni kule Ngaka na Kiwira. Maeneo yote haya yanahitaji usimamizi mzuri. Mnayo Bodi, Mwenyekiti yupo kwa hiyo mnatosha kuifanya kazi hii,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One waboreshe mahusiano yao na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo. “Kuweni karibu na wananchi ili wajue umuhimu wenu na uwepo wenu na waweze kusaidia kulinda mali zenu. Shirikianeni na Halmashauri na Baraza la Madiwani, tangazeni kazi zenu za CSR ili wananchi wajue mmechangia nini katika kusaidia maendeleo yao,” alisema.

Kuhusu suala la watumishi waliofukuzwa kazi kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu (OWM-Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Erick Shitindi asimamie suala lao na kuwapatia majibu kuhusu hatma ya suala hilo.



Watumishi hao walikuwa wanawakilisha wenzao 201 ambao walifukuzwa kazi Februari 8, 2016 kwa sababu ya kufuatilia maslahi yao vikiwemo malipo ya saa za kazi za ziada (overtime), mishahara ya miezi miwili, malipo ya NSSF, vitendea kazi na usalama wa kazi migodini.

MWAKIFAMBA AKANUSHA UJUMBE ULIONEZWA MITANDAONI

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba amekana kuhusika na utumaji wa ujumbe katika mitandao ya kijamii juu ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari. 

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujumbe huo uliokuwa ukisambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kumuhusisha Rais wa Shirikisho hilo. 

Mwakifamba amesema kuwa ujumbe huo umeeleza kuwa Rais wa shirikisho hilo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaohusu wasanii waliokipigia kampeni Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutolipwa fedha zao pamoja na kuunga mkono jitihada za msanii Wema Sepetu kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Kiukweli sikushiriki kwa namna yoyote katika kuuandika ujumbe huo na nimesikitishwa kuona kwamba huo ujumbe unasambazwa ukiwa na jina langu hivyo umeniletea picha mbaya kwani ni kinyume na taratibu na sheria za Shirikisho,”alisema Mwakifamba.

Amefafanua kuwa Shirikisho hilo sio chama cha siasa na hawajasajiliwa na msajili wa vyama vya siasa bali wamejisajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kazi zote zinafanyika kwa Sheria Na. 4 ya mwaka 1976 ambayo iko chini ya Bodi ya Filamu Tanzania.

Ameongeza kuwa mwanachama wa shirikisho hilo hafungwi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa lakini kwa mujibu wa katiba ya vyama na shirikisho ni marufuku siasa kuletwa katika shirikisho au vyama vyake.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Chama cha Waigizaji, Saimon Mwapagaja ametoa rai kwa wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa lengo la kuchafua majina ya watu kuacha tabia hiyo kwani inashusha hadhi ya mtu husika na sio utaratibu mzuri.

“Changamoto tulizonazo katika tasnia ya filamu ni nyingi sana hivyo ifike wakati wasanii tuanze kuangalia vitu vya msingi na vyenye tija vitakavyomaliza changamoto hizo, pia wananchi wapunguze kujiamulia kufanya mambo ambayo baadae yanaweza kumsababishia muhusika matatizo mabukwa,” alisema Mwapagaja.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU VIFUNGASHIO VYA POMBE KALI – VOROBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Mamkamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, alipozungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.
Katikati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, kulia ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Profesa Faustin Kamuzora na Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira, Waziri Makamba alizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.




Mtakumbuka tarehe 20 Februari 2017 Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la Serikali la utaratibu utakaotumika kutekeleza agizo la kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba)kuanzia tarehe 1 Machi 2017. Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo, na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012.

Napenda kusisitiza na kuujulisha umma wa Tanzania kuwa utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali kuhusu usitishaji uingizaji, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki vya kufungia pombe kali utaanza rasmi tarehe 01 Machi, 2017, katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. 

Operesheni ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe 2 Machi 2017 kwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa. Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mnamo terehe 24 Februari 2017, kiliitishwa kikao cha Mawaziri na viongozi wa taasisi za Serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hili. Katika kikao hicho, Wizara na taasisi za Serikali zilipewa majukumu mbalimbali, kama ifuatavyo: 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki. Aidha, Mamlaka itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa. 

Wazalishaji na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale tu ambao wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu (3) ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa. Uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali ambao hawajasajiliwa itakuwa ni kosa la jinai kulingana na Sheria. 

Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani, atasajili makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani nchini ikiwa ni pamoja na Ethanol. Msajili atawajibika kutoa taarifa sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi na taasisi zinazohusika, kiasi kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na madhumuni ya matumizi. 

Kulingana na sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka 2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika operesheni hii itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. 

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama vimekidhi viwango vya kitaifa Ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali. 

Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha bidhaa zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa ufafanuzi wa hatima ya mitambo hiyo. Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia vifungashio vya plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashtakiwa. 

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mabwana afya katika operesheni hii watatoa elimu kwa umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza vileo vya aina zote, na kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume cha sheria na kanuni. 

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili. 
Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia. 

Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni. 


Kama tangazo letu la tarehe 20/2/2017 lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji muda mchache kufanya hivyo, na ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata kibali maalum kabla ya tarehe 28/2/2017. Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya wazalishaji 9. Tutangaza kesho iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au la. Kanuni za upigaji marufuku pombe hizi zipo tayari.

Pia tumepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hili limekuja ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala. Ukweli ni kwamba Serikali ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei 2016, na mara kadhaa baada ya hapo, na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi. Vilevile, taarifa ya Serikali iliyotangaza kupiga marufuku pombe za viroba ziliripotiwa kwa ukubwa stahiki kwenye vyombo vya habari, ikiwemo kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi, mwezi Agosti 2016. Katika taarifa zote za nyuma, Serikali ilitangaza kwamba hatua hiyo itaanza tarehe 1 Januari 2017. Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili. Iwapo, baada ya taarifa hizo za Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au kutengeneza au kuhifadhi pombe za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo, atakuwa amefanya hivyo akijua madhara yake.

Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.


OFISI YA MAKAMU WA RAIS

28/02/2017

NHIF YATOA ELIMU KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MKINGA


 Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Ally Mwakababu akizungumza wakati wa kikao cha pamoja baina yao na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga,kushoto ni Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Ally Mwakababu kulia ni Mratibu wa CHF wilaya ya Mkinga,Rashid Gembe
 Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga (NHIF) Ally Mwakababu kushoto akifuarahia jambo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga,Rashid Gembe mara baada ya kufungua kikao cha pamoja baina ya Mfuko huo na watumishi wa Halmashauri hiyo kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huo ili kuweza kunufaika na huduma zinazotolewa.
Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga (NHIF) Miraji Kisile akieleza umuhimu wa watumishi wa halmashauri hiyo kujiunga  na mfuko huo ili kuweza kunufaika na huduma zinazotolewa wakati wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Kutoka kushoto ni Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga (NHIF) Ally Mwakababu akiteta jambo na Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga,Miraji Kisile katikati kushoto ni Mratibu wa CHF wilaya ya Mkinga Elizaberth Dickson kabla ya kuanza semina hiyo ya uhamasishaji wa watumishi kujiunga na mfuko huo
Daktari akiwapima baadhi ya watumishi wa halmashauri huo
 Daktari akiwapima baadhi ya watumishi wa halmashauri huo
Afisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Juliana Mathias wa pili kulia akiwapima baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo uzito wakati wa uhamasishaji huo 
 Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga wakifuatilia kikao hicho
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga wakifuatilia kikao hicho
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha

MEYA ILALA AFUNGUA RASMI DARAJA LA BONYOKWA-KINYEREZI

 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, akihutubia wananchi baada ya kufungua rasmi  daraja linalounganisha Kata ya Bonyokwa na Kata ya Kinyerezi katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es salaam.
 Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonesti (Chadema) akihutubia wakati wa ufunguzi wa daraja hilo
 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, akikiwa amekata utepe ikiwa ni ishara ya  kufungua rasmi  daraja linalounganisha Kata ya Bonyokwa na Kata ya Kinyerezi katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es salaam.

Mwandishi wetu
MSTAHIKI MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko jana alifungua rasmi daraja linalounganisha Kata ya Bonyokwa na Kata ya Kinyerezi katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es salaam.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mhandisi wa Manispaa ya Ilala ndugu Benjamin Maziku alisema  daraja hili limejengwa kwa takribani mwaka mmoja na kugharimu Tsh.million  478 hadi kukamilika kwake leo hii. Ujenzi wa daraja hili umesua sua kwa siku nyingi kutokana na sababu mbali mbali lakini kutokana na usimamizi imara wa Mstahiki Meya wa Ilala Mhe. Charles Kuyeko sasa historia imebadilika.

Meya Kuyeko akizungumza na umati wa wananchi waliokusanyika kushuhudia ufunguzi huo amewasitiza kulilinda na kulitunza vyema daraja hilo kwani limejengwa kwa kodi zao.

Awali, Meya akitoa historia ya daraja hilo amesema kuwa, waliokuwa wanatakiwa kujenga daraja hilo ni wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) lakini kutokana na kusuasua kwao, Mimi (Meya)  niamua kuingilia kati kwa Manispaa kutenga Fedha kujenga daraja la muda ili kuwasaidia wananchi wa Bonyokwa kuondokana na atha ya kuwa Kisiwa hususani wakati wa Mvua.

Kuyeko ambaye pia ni Diwani wa kata ya bonyokwa amewaambia wananchi hao waliofurika kwenye uzifunguzi huo kuwa huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa ahadi zake katika kutatua kero za wananchi na wapiga kura wake. "Nawahakikishia kuwa hamtajutia kunipa kura zenu kwani daraja hili imekuwa kero ya miaka nenda rudi lakini Mimi nimeimaliza kwa muda mfupi kwa kushirikiana na watendaji wangu hivyo mtarajie mengi kabla mwaka huu kuisha hata daladala zitakuwa zinafika hadi kisiwani".

Mbali na hayo,Meya amewaahidi wananchi hao muda mfupi ujao atatatua kero ya maji na barabara kama ambavyo aliahidi kutekeleza wakati wa kampeni.

Ufunguzi huo ulihudhuliwa na viongozi mbali mbali wa kiserikali na kisiasa akiwemo mbunge wa Viti Maalum Mhe. Anatropia Theonest, madiwani wa kata mbalimbali na viongozi wa vyama vya siasa.

Akitoa salam kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa, Dk.Makongoro Milton Mahanga mbunge wa zamani jimbo la Segerea ambaye kwa sasa ni, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Ilala alisema, "Tangu niwe kiongozi sijawahi kuona kiongozi mahiri kama Meya Kuyeko. 

Ameweza kuwaunganisha viongozi wa Manispaa yake na kuwa kitu kimoja, na hadi sasa ameshafanya vitu vingi ambavyo awali vilishindikana nakupongeza sana Meya Kuyeko.

Dkt. Mahanga  aliwasisitiza wananchi kuwaamini viongozi wanaotokana na UKAWA kwani ni wazuri jifunzeni kwa Kuyeko mambo makubwa anayoyafanya. Kwa niaba ya Chadema nampongeza sana Meya Kuyeko kwa kukiwakirisha vyema  chama kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea ndugu Gango Kidera aliwataka wananchi wa Bonyokwa  waendelee kumwamini na kumuunga mkono Meya Kuyeko, Baraza lake la Madiwani kwani amekuwa mfano bora kwa kutekeleza ahadi zake zinazotokana na ilani na Sera za Chadema/UKAWA. 

Chadema imemtuma Kuyeko kuwatumikia wananchi wa Bonyokwa na Manispaa nzima ya Ilala kwa kuhakikisha anatatua kero zao kwa spidi ya mwendokasi na leo tumeona anatenda kwa maslahi ya wananchi. Nakupongeza sana Meya Kuyeko, alisema Kidera

Viongozi wengine waliozungumza katika ufunguzi huo ni Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Anatropia Theonest ambaye aliwapongeza wananchi wa Bonyokwa kwa kumchagua Kuyeko, wananchi wa Bonyokwa mlifanya maamuzi sahihi kuchagua Chadema kwa sababu bila Chadema Meya Kuyeko tusingempata. 

Anatropia pia alimpongeza Meya Kuyeko kwa kuendelea kutatua kero za wapiga kura wa Bonyokwa siku hadi siku na Ilala kwa ujumla. UKAWA kwa Manispaa ya Ilala chini ya Meya Kuyeko imeleta matumaini makubwa kwani wakazi wa Manispaa wapatao 1,415,443 walikuwa wamekata tamaa kabisa kwani viongozi waliopita walishindwa kutatua kero za wananchi, hivyo UKAWA chini ya Meya Kuyeko ni mfariji mkuu wa wananchi, alisema Anatropia.

Diwani wa Buguruni Mhe. Penza wa CUF akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa Ilala alisema ilani ya UKAWA imeweka vipaumbele kwenye Barabara, maji, afya, elimu, na masoko na mitaji hivi vyote vinafanyika.

Meya Kuyeko aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kumwamini na kumpa ushirikiano wa karibu hali ambayo inampa ari ya kuwatumikia kwa nguvu zake zote. Pia amekishukuru chama chake Chadema, viongozi, Madiwani na watendaji wote wa Manispaa ya Ilala wakiongozwa na Mkurugenzi kwa kumpa ushirikiano wa hali na Mali katika kuwatumikia wananchi.

MAKALA: WIKI YA SHERIA NA SIKU YA SHERIA NCHINI, 2017

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akikagua gwaride maalum lililoandaliwa, ukaguzi wa gwaride hili huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika.

Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania

Nchi yoyote yenye kuzingatia misingi ya Utawala wa Sheria, huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta amani na Maendeleo ya kiuchumi katika taifa husika.

Hii inajidhihirisha kupitia Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini, 2017 ambayo ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’

Kauli mbiu hii ina maana ya kuwa kukamilishwa mapema kwa mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.
Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania iliadhimisha Siku ya Sheria nchini, ambayo huashiria kuanza rasmi kwa mwaka wa Mahakama ambapo shughuli za usikilizaji wa Mashauri huanza rasmi.

Kwa mwaka huu, sherehe za Siku ya Sheria nchini ziliadhimishwa rasmi tarehe 02.02.2017, ambapo kila Mkoa uliadhimisha, kwa upande wa Dar es Salaam, Sherehe hizi zilifanyika katika Kiwanja cha Mahakama kilichopo Chimala karibu na Hospitali ya ‘Ocean road’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia watumishi na wageni waalikwa katika Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02, 2017.

Aidha; Sherehe za Kilele cha Siku ya Sheria nchini zilitanguliwa na Maonyesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza rasmi Januari, 28 hadi Februari 01, 2017, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika nchi nzima lengo kuu likiwa ni kutoa elimu ya Sheria kwa Wananchi juu ya huduma na taratibu mbalimbali za Kisheria.

Kwa upande wa Dar es Salaam, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo, Wadau walioshiriki ni pamoja Mahakama yenyewe kama mwenyeji, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi wa Mahakama IJA, Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Huria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wengine ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal Aid), TAKUKURU (PCCB), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya Ardhi,  Chama  cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tume ya Kurekebisha Sheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA, Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA),  Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Sekretarieti ya Msaada wa Sheria, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ‘Tanzania Network of Legal Aid Provider (TANLAPS),’ Legal Aid and Human Centre na NHIF.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma akisoma risala yake ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02, 2017, waliopo nyuma ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ni baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Tanzania.

Katika maonesho hayo kulikuwa na uwakilishi wa ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufaa ambapo taratibu/huduma mbalimbali za Kimahakama zilitolewa kwa wananchi waliopata fursa ya kutembelea mabanda ya Maonesaho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Lengo la kufanyika kwa Maonesho hayo ilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi kufahamu shughuli za Mahakama pamoja na Wadau wa Sekta Sheria kwa ujumla, vilevile kuwawezesha wananchi kupata elimu juu ya taratibu mbalimbali Mahakama katika upatikanaji wa haki.

Aidha, Sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Wageni mbalimbali akiwepo Spika wa Bunge la Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Mwendesha Mashtaka (DPP), TLS, Majaji Wastaafu,  Mabalozi, Viongozi wa dini mbalimbali n.k.

Aidha katika Sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumzia masuala kadhaa ambayo ni pamoja na:-
Kutoa pongezi kwa kasi nzuri ya Uondoshaji wa Mashauri, ambapo katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa ‘Pamoja na changamoto inayotukabili ya uwiano usio sawa wa idadi ya Majaji na Mahakimu na Watumishi wengine kama Wasaidizi wa Kumbukumbu; wastani wa jumla ya umalizaji wa mashauri upo wa asilimia 101 (101%), yaani kwa tafsiri ya kila mashauri mia moja (100) yanayosajiliwa uwezo wa kuyamaliza ni asilimia 101 (101%).
Kwa mwaka wa Mahakama ulioisha Desemba, 2016, jumla ya mashauri 276,147 yalisajiliwa na mashauri yaliyosikilizwa na kukamilika yalikuwa ni 279,331.
Viongozi wanaoiwakilisha Mihimili mitatu ya Dola wakiwa katika picha ya pamoja katika Siku ya Sheria nchini, wa pili kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wa kwanza kushoto ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji, Prof. Ibrahim Juma, wa pili kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na wa kwanza kulia, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali.

Mashauri ambayo yapo bado Mahakamani ilipofika Desemba, 2016 ni jumla 56,531 na kati ya hayo, yenye sifa ya kuitwa ya zamani (backlogs) ni mashauri 3,618 na ambayo ni sawa na wastani wa  asilimia sita (6%) tu.

Mhe. Prof. Jaji Juma aliongeza kuwa kati ya mashauri 249 yaliyosajiliwa Mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ambapo ya Ubunge yalikuwa 53 na Udiwani 196. Hadi kufikia Desemba 30, 2016 mashauri 52 yaliyohusu ubunge yaliamuliwa, hivyo kubaki na shauri moja (1) tu. Mashauri ya udiwani yalisikilizwa na kuamuliwa yote. Mashauri ya uchaguzi wa Ubunge yalisikilizwa mfululizo kuanzia mwezi Juni mpaka Oktoba, 2016 yakijumuisha Majaji 29 kwa yale ya Ubunge; na Mahakimu kwa mashauri ya Udiwani.

Ari hii ya Kasi ya usikilizwaji wa Mashauri mbalimbali, ilimfurahisha Mhe. Rais na kupelekea kutoa pongezi kwa Mahakama kwa kazi nzuri waliofanya katika mwaka wa Mahakama uliopita.

Mbali na pongezi, Mhe. Rais alitoa changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na ‘Mashauri ya kodi na fedha zilizokwama kutokana na wadaawa na masjala za Mahakama kufanya mchezo maarufu wa ‘Parking’ kuzuia mashauri yasimalizike na kuikosesha serikali mapato.’ Katika hili Mhe. Rais aliiomba Mahakama kutilia mkazo katika mashauri haya ili kuingizia Serikali mapato.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama na Wageni wengine waalikwa wakiwa katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika Februari 02, 2017.

Hata hivyo; Mahakama pamoja na jukumu lake kuu la kutoa haki,imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inajenga na kuweka mazingira bora ya biashara shindani ili kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini, alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imedhamiria kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha wadaawa wanapata nakala ya hukumu ndani ya siku 21 na mwenendo wa shauri ndani ya siku 30 tangu hukumu iliposomwa.

“Wananchi wanastahili kupata nakala za hukumu kwa wakati. Sheria inataka kila Jaji au Hakimu asome hukumu ndani ya siku 90 tangu kesi ilipomalizika kusikilizwa,” alisisitiza Kaimu Jaji Mkuu.

Miongoni mwa masuala ambayo Kaimu Jaji Mkuu aliyatilia msisitizo/mkazo katika hotuba yake pia ni pamoja na matumizi ya TEHAMA Mahakamani ili kurahisisha taratibu mbalimbali za Mahakama.

“Ifikapo Desemba, 2018, kulingana na ramani (Road map) ya matumizi ya TEHAMA, kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (E-govt Agency), tuweze kuanza matumizi kamili ya TEHAMA kwenye kazi za Kimahakama na Kiutawala,” alisema Jaji Juma.

Aliongeza kuwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa ya Mahakama pia unaenda sanjari na matumizi ya hatua kwa hatua ya TEHAMA, vilevile kuhakikisha taratibu za masuala ya fedha ndani ya Mahakama zinaendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA mpaka kwenye ngazi ya Mikoa/Wilaya.

Alienda mbali na kuongeza kuwa Mfumo wa TEHAMA wa ukusanyaji wa Takwimu za Mashauri (JSDS) utaboreshwa kuwa sehemu ya mfumo wa kisasa. Matumizi makubwa ya Watanzania ya simu za kisasa (smart phone) yanarahisisha sana azma hii ya kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji kazi wa kizamani na wenye tija hafifu.

Jitihada mbalimbali zifanywazo na Mahakama kwa sasa kama ujenzi na ukarabati wa miundombinu, matumizi ya TEHAMA n.k zinalenga katika kuboresha na kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini aliitaka Mahakama kukamilisha mapema mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.

“Majaji, Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na wadau wengine wa Mahakama, ikiwemo vyombo vya upelelezi wa jinai, Rushwa na Uhujumu uchumi, Mabaraza ya kodi, Ardhi, Ushindani na mengineyo wazingatie matakwa ya Katiba ya nchi, Sheria na Kanuni katika utoaji haki kwa wakati,” alieleza Masaju.

Siku ya Sheria nchini, hutoa nafasi kwa Mahakama pamoja na wadau wake wakuu ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika kutoa hotuba juu ya Mafanikio na changamoto zinazoikabili Sekta ya Sheria katika mwaka husika.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Bw. John Seka aliihakikishia Mahakama kupitia hotuba yake kuwa Chama hicho kipo tayari wakati wowote kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha kuwa utoaji haki unatamalaki.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hutumika kama njia mojawapo ya kukutana na Wadau ili kupata michango/maoni mbalimbali ya Wadau na wananchi kwa ujumla yote yakitumika na Mahakama kujitathmini na kuona wapi imepwaya ili kuendelea kufanya maboresho katika suala zima la utoaji haki nchini.

Akiongea na Mwandishi wa Makala hii, Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati alisema kwa mwaka huu mpya wa Sheria, Mahakama imejipanga kuhakikisha inaendelea kushughulikia mlundikano wa kesi/mashauri ya muda mrefu ‘case backlog’.

“Kama unavyojua kwa sasa, Mahakama imejikita katika kufanya maboresho kadhaa wa kadhaa, miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na kushughulikia mashauri ya muda mrefu, na jitihada hizi zimezaa matunda hata kwa mwaka jana ambapo hadi tunamaliza mwaka tulikuwa mlundikano sifuri (zero cases) katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na za Wilaya,hivyo jitihada hizi zinaendelea hata kwa sasa,” alieleza Mhe. Revocati.

Msajili Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa Mahakama imejiwekea muda maalum wa kushughulikia kesi hadi kumalizika kwake, ambapo alieleza kuwa kwa ngazi ya Mahakama za Mwanzo kesi inabidi iwe imekamilika kwa kipindi cha miezi sita, Mahakama za Wilaya/Hakimu Mkazi, mwaka mmoja na kwa upande wa Mahakama Kuu/Rufani miaka miwili (2), na suala hili tunalisimamia kwani pia Mpango Mkakati wetu wa Mahakama kupitia moja ya nguzo zake inaelekeza kuboresha suala zima la utoaji haki nchini.

Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria nchini ndani ya wiki ya kwanza wa mwezi Februari kila mwaka, siku hii huashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika, maudhui ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’

Kwa mara ya kwanza, Mahakama ya Tanzania iliadhimisha rasmi Siku ya Sheria nchini mwaka 1997 ambapo Viongozi wa Dini walitoa dua ya kuombea Majaji, Mahakimu na Wanasheria ili watimize wajibu wao mzito wa utoaji haki nchini. Hata hivyo mnamo Machi 1, 1996 kulifanyika ibada maalum ya kuwaombea Majaji na Mahakimu ili wasikilize vyema mashauri yoyote na hasahasa ya uchaguzi Mkuu uliofanyika 1995. Huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na hivyo kulikuwa na mashauri mengi ya uchaguzi.

Aidha; mnamo mwaka 2007, Sherehe za Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza na Mheshimiwa Rais alipata nafasi ya kutoa hotuba na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgeni rasmi kutoa hotuba.