Tuesday, December 26, 2017

MAASKOFU WAFUNGUKA, WATOA YA MOYONI

*MMOJA ATAKA WATANZANIA KUACHA KULALAMA VYUMA KUKAZA


Na Said Mwishehe,Blogu ya Jamii

MAASKOFU mbalimbali nchini wameitumia Sikukuu ya Krismasi kuelezea mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

Huku baadhi yao wakimpongeza Rais,Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuachia baadhi ya wafungwa waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa na wale wa vifungo vya maisha jela.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustine Shao, amempongeza Rais kuwaachia huru wafungwa hao kwani inaonesha wazi anaamini waliopo magerezani wakiwemo vijana wataendelea kujirekebisha na kuwa na tabia njema inayompendeza Mungu na jamii nzima.

Pia amewataka waumini wa Kikristo kujitakasa upya hasa katika Sikukuu ya Krismasi . “Ni vema pia Watanzania kila mmoja wetu akaheshimu mawazo ya mwenzake hata kama yanatofautiana”.


Askofu Pengo ahimiza mema

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesisitiza umuhimu wa Watanzania kutenda matendo mema na kuongozwa na hofu ya Mungu.

Askofu Pengo amesema hayo kwenye Misa ya pili ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Amesema maendeleo hayawezi kuja kama Watanzania wenyewe hawana maadili au hofu ya Mungu.“Kila mmoja wetu awe mwananchi au kiongozi, anapaswa kuwa na hofu ya Mungu itakayomuongoza katika kufanikisha mipango iliyokusudiwa au aliyoikusudia.

“Pia Watanzania wanapaswa kukubali kuongozwa na kuwaombea viongozi wao ili jitihada zinazofanywa zizae matunda mema kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake,” amesema Askofu Pengo.

ASKOFU Amani azungumzia utekaji nyara



Wakati huo huo Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, mkoani Kilimanjaro Isack Amani, amekemea vitendo vya ukatili vikiwamo vya utekaji nyara na mauaji ya kinyama yanayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

Amesema matukio hayo yanatishia kutoweka kwa amani iliyopiganiwa na waasisi wa Taifa kwa miaka mingi.

Akihubiri kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme Moshi, Askofu Amani alisema katika kipindi cha muda mfupi kumeibuka matukio yanayohatarisha amani ya nchi yetu.





Askofu Malasusa ahimiza upatanisho

Kwa upande wake Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, amewataka Watanzania kutumia Sikukuu ya Krismasi kupatana na kuwa wamoja.

Amesema hayo akiwa katika ibada ya Krismasi iliyofanyika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam.Amefafanua kuna watu wengi wanaishi bila kupatana hata ndani ya Kanisa.

“Neema inatuagiza kukataa dhambi na inatukumbusha kuwa watu wa kutafuta amani na upatanisho,”amesema.



Askofu Mwenda ataka waumini kujiimarisha

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Ruvuma, Amon Mwenda, amewataka waumini wa kanisa hilo kujiimarisha katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya kiuchumi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya kidunia.

Ametoa salamu hizo leo katika salamu za Sikukuu ya Krismasi na kuongeza waumini wanatakiwa kutambua dunia ya sasa imebadilika, hivyo ni vyema wakajifunza kwenda na wakati na kujiimarisha kiuchumi.



Askofu Gavile ataka Watanzania kuacha kulalama

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile, amewataka Watanzania kuacha kulalamika kuhusu vyuma kukaza na badala yake kumrejea Mungu awapiganie ili wafanikiwe kimaisha.

Akizungumza mara baada ya ibada katika Usharika wa Kanisa Kuu, Askofu Gavile amesema kuwa Wakristo hawana sababu ya kuungana na wanaolalamika vyuma kukaza bali wanapaswa kufanya kazi na kumtanguliza Mungu kwa kila jambo. 

.

Askofu Mtokambali atahadharisha

Askofu Mkuu wa Makanisa ya Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnabasi Mtokambali amewataka viongozi wa dini nchini kuzingatia wajibu wao katika kutoa huduma za kiroho na kuacha kuingiza siasa katika nyumba za ibada.

Amesema hayo katika maadhimisho ya miaka 43 ya kanisa hilo yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Amesema viongozi wa dini wanaaminiwa na kundi kubwa la watu lakini baadhi yao wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa jambo ambalo si nzuri.

1 comment:

Anonymous said...

Mbona hujaandika ya askofu Kakobe au kwa vile amemsema Magufuli? Mbona upo biased sana ndugu yangu Michuzi? Si kuripoti tu kwani wewe ndiye uliyesema?