Wednesday, January 11, 2017

TTCL YAZINDUA HUDUMA YA 4G ZANZIBAR

Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa TTCL na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu baada ya uzinduzi wa huduma ya 4G Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.
Na Khadija Khamis, 
MAELEZO Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Issa Haji Ussi Gavu amewataka wananchi kujiunga na huduma ya mawasiliano ya 4G LTE Zanzibar ambayo inauwezo mkubwa wa mawasiliano ya haraka .
Akizundua huduma  za 4G LTE  katika ofisi za Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) , Waziri Gavu alisema kwamba ukuaji wa teknolojia unawalazimu watumiaji wa simu za mkononi kuwa na mawasiliano ya uhakika.
Waziri Gavu alisema kwamba huduma hiyo itawarahisishia wananchi wa Zanzibar  mawasiliano katika kazi zao za kilimo, biashara ufugaji pamoja na  wafanyakazi wa serikalini  na sekta binafsi.
“Teknolojia inaendelea kukua na kuja na ugunduzi mpya, nakuombeni wananchi wenzangu tutumie teknolojia hizi katika kuharakisha maendeleo yetu maana huduma za mawasiliano ni sehemu muhimu katika kuchapuza maendeleo” Alisema Waziri Gavu.
Alisema anaimani kuwa kuanza kutumia teknolojia hizo za 4G LTE kutawezesha sasa kuwaunganisha wananchi katika maeneo mbalimbali kimawasiliano ikiwa pamoja na kutumia huduma hizo katika kukuza biashara ya mtu mmoja mmoja au kikundi.
Waziri Gavu  alisema kwamba Aidha  sekta za serikali na binafsi zitaimarishwa kwa kupata huduma nzuri kutokana na mawasiliano ya  4G ambayo yamejipanga kwa mwaka mmoja tu kuenea kwa Tanzania nzima.
Nae Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu  wa TTCL, Waziri Kindamba  alisema  huduma ya mawasiliano ya 4G  ina gharama nafuu  kwa wateja wake,lakini pia mawasiliano yake ni ya uhakika zaidi.

“Mheshimiwa Waziri gharama za 4G ni shilingi  moja kwa sekunde kwa mtumiaji, kiwango cha tozo hiki ni nafuu sana   kulinganisha na kampuni nyengine  hapa nchini.”Alieleza.
Kaimu  Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL alisema kwamba kuzinduliwa kwa huduma hizo wakati huu wa kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar ni kielelezo tosha cha namna TTCL inavyoenzi kwa vitendo Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo yaliwakomboa wananchi wa Visiwa hivi katika ukoloni mkongwe wa Kisultan.

 “katika kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuweza  kuungana na wenzetu kwa pamoja  kitu kizuri cha kuwapa kama ni zawadi  ni 4G ni mawasiliano yaliobora na  ya  kisasa “alisema Kindamba .
Aidha alisema huduma hizo ni kiungo muhimu katika kustawisha maendeleo ya jamii kupitia katika Nyanja zote ikiwemo kiuchumi kisiasa na  kijamii.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, kauli mbiu yetu ya kutambulisha huduma za 4G LTE Zanzibar ni “Chei chei Zanzibar tumefanikisha” alisema Kindamba.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiunga na huduma za 4G LTE ikiwa ni kampuni ya kizalendo ya hapa Tanzania.
Alisema kuwa lengo kuu la kampuni hiyo ni kuifanya kampuni  kuwa namba moja kwa Tanzania  ambayo itatoa huduma ya simu ya mezani na mkononi  na kurudi katika ubora wake wa awali   na pia ni mdau wa TEHAMA.

No comments:

Post a Comment