Wednesday, January 11, 2017

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kituo cha Zimamoto na Uokozi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba uzembe wa aina yoyote  unaoweza kufanywa  na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi wakati inapotokea dharura kwa bahati mbaya unaweza kukimbiza huduma za ndege za Kimataifa zinazotumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Alisema  umuhimu wa Kikosi hicho kuwepo katika maeneo ya Viwanja vya ndege hata Bandarini kwa ajili ya kutoa huduma za uokozi wa masuala ya dharura ni muhimi na mkubwa kwa Uchumi wa Taifa hili.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokozi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Balozi Seif alisema  Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada mbali mbali za kukiimarisha Kikosi hicho cha Zimamoto ili kiende sambamba  na Teknalojia  ya kisasa pamoja na kufikia  kutoa huduma zenye viwango vya  Kimataifa.
Alisema Idara ya  Zimamoto na uokozi  ni nyenzo muhimu katika Taifa lolote Duniani, hivyo ni vyema kwa watendaji wa Taasisi hiyo   wakaandaliwa utaratibu muwafaka wa kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara  ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa watendaji wa Kikosi hicho kutoa mafunzo maalum kwa watendaji wa Serikali, Taasisi za Umma na hata zile binafsi katika kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea katika maeneo yao ya kazi.
Aidha Balozi Seif  aliuomba Uongozi wa Taasisi hiyo kushirikiana na Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar katika kutoa mafunzo maskulini juu ya suala zima la Zimamoto na Uokozi ili kutengeneza jamii yenye ufahamu na utayari katika  kukabiliana na majanga wakati yanapotokezea.
Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Makamanda na wapiganaji wa vikosi vya ulin zi na usalama hapa Nchini kwa jitihada mbali mbali wanazochukuwa  katika kukabiliana na maafa katika sehemu mbali mbali hapa Nchini.
Alieleza kwamba Wananchi wengi hivi sasa wamejenga imani kubwa kwa Vikosi hicho, hivyo ni vyema  wakaendelea kujiaminisha  kwa Jamii iliyowazunguuka  wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Akitoa Taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho,  Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Kamishna Ali Abdulla Malimus  alisema kituo cha Zimamoto  na Uokozi kiliopo  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amain Karume  kimejengwa kwa kuzingatia vigezo vya Kimataifa kufuatia  agizo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Kamishna Ali  Abdulla alisema askari wa Kikosi hicho wameonyesha faraja yao kutokana na jitihada kubwa  zilizochukuliwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha miundombinu na Vifaa vya kisasa  kwa kikosi chao vinavyolingana na uwezo wa huduma zinazohitajika kutolewa kwenye Viwanja vya ndege.
Alieleza kwamba kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Aman Karume Zanzibar hivi sasa kimekuwa na harakati kubwa za kuhudumia ndege kubwa za Kimataifa kutoka  Mataifa mbali mbali Duniani.
Kamishna wa Zimamoto na Uokozi Zanzibar alisema  Kikosi hicho tayari kimeshapokea magari makubwa ya Kisasa Mawili kati ya Manne yaliyonunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kuitia Mradi salama ambao kila gari Moja lina uwezo wa kutoa Lita 9,000 kwa dakika moja wakati wa kutoa huduma za dharura.
Hata hivyo Kamishna huyo alieleza changamoto ya sasa inayokikabili Kikosi hicho kuwa ni uhaba wa watendaji wenye elimu na Taaluma Maalum inayoweza  kukidhi mahitaji ya kupambana na Majanga makubwa kama ajali za Ndege kubwa zinazoruka na kutua.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ  Bibi Radhia  Rashid  Haroub alisema ujenzi wa Kituo hicho cha Zimamoto na Uokozi kwenye  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Zanzibar uliojumuisha Taasisi tofauti za Umma umeigharimu Serikali Kuu jumla  ya Shilingi Milioni 234,000,000/-.
Bibi Radhia alisema Kituo hicho kina sehemu maalum ya maegesho ya Magari ya Kikosi hicho, Ofisi ya Mkuu wa Kituo, Chumba cha Mawasiliano  pamoja na Vyumba wa Askari wanawake na wanaume.
Akimkaribisha Balozi Seif kwenye hafla hiyo ya Uzinduzi wa Jengo la Kituo cha Zimamoto Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali ya Mitaa na Idara Maalum za SMZ  Mh. Shamata Shaame  Khamis alisema Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kimeongezewa nguvu ya utekelezaji wa majukumu yake iliyopangiwa kila siku.
Mheshimiwa Shamata alisema  nguvu hizo za miundombinu na vifaa ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuzipatia uwezo Taasisi zake ikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua patia kuashiria kuzindua rasmi Jengo la Kituo cha kikosi cha zimamoto na uokozi cha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Muonekano wa Jengo Jipya la Kikosi cha Zimamoto na Uokozi liliopo kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wa Abeid Aman Karume lililojengwa na Serikali kwa agizo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment