Friday, September 6, 2013

MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA OKTOBA - DISEMBA 2013 NCHINI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za masika (Machi - Mei) 2013 na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi  cha Oktoba hadi Disemba, 2013.

1.0 TATHMINI YA MVUA KIPINDI CHA MACHI – MEI, 2013
Katika msimu uliopita wa mvua za masika 2013, maeneo mengi ya  nchi yalipata mvua za wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tabora, Rukwa, Mara na Singida  ambayo ilipata mvua juu ya wastani. Wakati huo huo baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa, Ruvuma, Kilimanjaro na maeneo mengi ya mwambao wa pwani yalipata mvua chini ya  wastani.

Vifuatavyo ni viwango vya mvua pamoja na asilimia ya mvua zilizonyesha ikilinganishwa na wastani wa muda mrefu katika baadhi ya vituo nchini:
1.1 Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka
Kanda ya Ziwa Victoria: Bukoba milimeta 984.9 (110.9%), Mwanza 385.0mm (101.1%), Musoma milimeta 516.4 (127.5%), Ukiriguru milimeta 363.4 (107.5%) na Shinyanga milimeta 307.7 (61.1.0%).
Nyanda za juu kaskazini mashariki: Arusha milimeta 368.8 (84.4%), Moshi milimeta 472.9 (77.9%), Lyamungo milimeta 655.5 (65.3%), Kilimanjaro milimeta 291.6 (95.5%) na Same milimeta 291.3 (111.8%).
Pwani ya kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba: Zanzibar milimeta 534.3 (62.0%), Amani milimeta 484.0 (63.0%), Kizimbani milimeta 667.7 (75.2%), Dar es Salaam milimeta 458.8 (77.7%), Morogoro milimeta 227.8 (55.1%), Tanga milimeta 586.7 (91.4%) na Pemba milimeta 884.0 (85.7%).

1.2 Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Nyanda za juu kusini magharibi: Mbeya milimeta 254.8 (85.7%), Sumbawanga milimeta 275.0 (126.2%), Mahenge milimeta 1215.5 (118.2%) na Tukuyu milimeta 1094.2 (96.7%).
Kanda ya magharibi: Tabora milimeta 296.4 (135.2%), Kibondo milimeta 418.2 (94.0%) na Kigoma milimeta 318.7 (94.6%).

Pwani ya kusini: Kilwa milimeta 346.4 (68.3%), Mtwara milimeta 404.2 (86.0%) na Naliendele milimeta 350.5 (79.4%).

Kanda ya kati: Singida milimeta 410.0 (198.9%), Dodoma milimeta 145.1 (82.0%) na Hombolo milimeta 101.0 (52.9%).

Kanda ya kusini: Songea  milimeta 247.9 (67.5%)
Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani, wakati viwango vya kati ya asilimia 75 na 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.

2.0 MWELEKEO WA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA 2013

2.1 Utangulizi
Wanasayansi kutoka taasisi za hali ya hewa kwenye nchi za Pembe ya Afrika, Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, na taasisi za kikanda na kimataifa walikutana Nairobi na baaadae Eldoret, Kenya kuanzia tarehe 12 hadi 23 Agosti, 2013 kufanya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu. Aidha, mkutano kama huo ulifanyika pia kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) huko Harare, Zimbabwe kuanzia tarehe 19 hadi 31 Agosti, 2013 ambapo Tanzania  ilishiriki. Mikutano hiyo ilikuwa inafanyika sambamba na mkutano wa wataalam na wachambuzi wa masuala ya hali ya hewa na klimatolojia katika Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambapo  tathmini ya kina katika mifumo ya hali ya hewa na athari zake  kwa msimu ujao wa mvua nchini ilifanyika.Viashiria vikuu vilivyotumika ni pamoja na  hali ya joto la Bahari katika maeneo ya bahari ya Hindi, Atlantiki pamoja na yale ya tropikali ya bahari ya Pasifiki.

2.2 Mifumo ya hali ya hewa
Joto la Bahari lililopo na linalotarajiwa katika maeneo ya tropikali ya bahari za Pasifiki, Atlantiki pamoja na Hindi lilichambuliwa. Viashiria vingine ikiwemo mifumo na mwelekeo wa upepo ambayo huleta unyevunyevu katika nchi yetu pia ilizingatiwa. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2013 joto la wastani hadi chini ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya tropikali ya bahari ya Pasifiki.

Hali ya joto la bahari inatarajiwa kuwa juu kidogo ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Indonesia) katika miezi ya Oktoba hadi Novemba 2013, ikiambatana na hali ya joto la bahari chini kidogo ya wastani katika maeneo ya  magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki).  Hali hiyo inatarajiwa kusababisha upepo wenye  unyevunyevu hafifu kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika maeneo mengi ya pwani ya Afrika mashariki. Aidha, upepo kutoka magharibi katika misitu ya Kongo unatarajiwa kuwa hafifu na hivyo kupunguza kiwango cha unyevunyevu angani katika maeneo ya magharibi mwa nchi.

Hata hivyo, katika kipindi cha  mwishoni mwa miezi Novemba hadi Desemba, 2013 kunatarajiwa kuwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la  magharibi mwa Bahari ya Hindi hali hii inatarajiwa kusababisha ongezeka kiasi la unyevunyevu katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki.
Ongezeko kiasi la joto la bahari kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi katika kipindi cha Novemba na Disemba, 2013 linatarajiwa kusababisha kuwepo kwa matukio ya vimbunga katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli, na hivyo kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini katika vipindi vifupi.

2.3 Mwelekeo wa Mvua Oktoba - Disemba 2013 Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa kama ilivyoelezewa hapo juu, mvua za kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2013 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
(i)    Mvua za Vuli (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini, kanda ya Ziwa Victoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Mwaka huu mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), mikoa ya Mwanza, Simiyu  na Shinyanga,  maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita na Mara), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma pamoja na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani.


Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Septemba, 2013 katika mkoa wa Kagera na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu katika wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2013. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Katika mikoa mingine ya ukanda wa Ziwa Victoria (Mwanza, Shinyanga, na Simiyu) mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi wa Oktoba, 2013. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za chini wastani katika maeneo mengi.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara): Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2013 na zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Arusha. Hata hivyo kaskazini mwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika baadhi ya maeneo.

(ii)     Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kati, nyanda za juu kusini-magharibi, kusini mwa nchi na pwani ya kusini. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2013 maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani.

Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2013 katika mkoa wa Kigoma na wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2013 katika mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo ya kusini mwa mkoa wa Tabora na maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Rukwa. Mikoa ya Katavi, kusini mwa mkoa wa Kigoma, magharibi mwa mkoa wa Rukwa na kaskazini mwa mkoa wa Tabora,  mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Disemba, 2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo ya kusini na uwezekano mkubwa wa kuwa na mvua chini ya wastani katika maeneo ya kaskazini mwa mikoa hiyo.

Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba, 2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi.

Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)

Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba, 2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani na upo uwezekano wa baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Lindi kuwa na mvua chini ya  wastani. 

No comments:

Post a Comment