Thursday, December 6, 2018

MJANE WA DAUD BALALI AINGIA KWENYE MGOGORO WA ARDHI MBWENI MAPUTO

*Wanaoishi maeneo hayo wamuangukia Waziri William Lukuvi, wamuomba aingilie kati *Diwani ajitosa kuzungumzia ukweli eneo hilo...adai wananchi wamevamia, waondoke

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WANANCHI wa Mtaa wa Mbweni Maputo jijini Dar es Salaam wapatao 270 wamemuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuingilia kati mgogoro wa ardhi wa eneo ambalo linadaiwa kuwa ni mali ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Daud Balali(sasa marehemu) ambalo baada ya kuwa pori na kichaka cha uhalifu waliamua kusafisha eneo hilo na kisha kuweka makazi yao.

Wakizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari leo katika eneo hilo la mtaa wa Mbweni Matupo jijini Dar es Salaam wananchi hao ambao wanadaiwa kuwa ni wavamizi wameeleza wazi kuwa ni kweli wao waliamua kusafisha eneo hilo baada ya kuwa kero kwa wananchi wa maeneo hayo ya Mbweni na walifanya hivyo baada ya kuona limekaa muda mrefu bila kuendelezwa huku wakidai wamefuatilia wizarani na kubaini halina mwenyewe kwani ni eneo ambalo halijapimwa ila wanachokiona kuna watu wameamua kutengeneza hati ili kujionesha kama wao ndio wamiliki.

Wamewaambia waandishi wa habari kutambua kuwa katika eneo hilo hadi sasa kuna watu karibu watano wamekwenda na kila mmoja anasema la kwake.Hata hivyo wananchi hao wakiomba kuoneshwa hati hakuna mwenye hati miliki huku wakidai kuwa kwa kuwa wao wanyongwe watu wenye uwezo wa kifedha wanatumia kama fimbo ya kuwanyanyasa na kutishia kwamba waondoke na kinyume na hapo nyumba zao zitabomolewa.

Akizungumza na kwa niaba ya wananchi wenzake ambao wapo eneo hilo Raphael Joseph amesema kuwa hawana tatizo iwapo sheria itawataka kuondoka eneo hilo lakini kwa haki ila kinachowasumbua ni namna ambavyo watu ambao hawana hati ya umiliki wa eneo hilo wanavyoamua kutumia utajiri wao wa fedha kuwanyanyasa na kuwatishia kuwa makazi yao yatabolewa.

"Hatuko juu ya sheria lakini tunaomba ifahamike ili eneo lilikuwa pori, hivyo likawa linatishia uhai wa wananchi wa eneo hili la Mbweni Maputo.Wananchi tukaamua kusafisha eneo hili na baadae tukaanzisha makazi kama ambavyo mnaona.Hatuko juu ya sheria lakini tunaomba haki ifuatwe.Tulienda kufungua kesi mahakamani ambayo ipo Mahakama Kuu , sasa kabla ya kesi kutolewa huku tunambiwa tuondoke.Tunakwenda wap? Hivyo tunamuomba Rais wetu mpendwa anayejali wanyonge atusaidie.Pia tunamuomba Waziri wa Aridhi atusaidie ili haki itendeke.Eneo hili lote halijapimwa lakini tunashangaa baadhi ya watu wanakuja na hati,"amesisitiza.

Ameongeza kuwa wamefuatilia historia ya eneo hilo na kubaini kuwa Daud Balali enzi za uhai wake aliomba eneo hilo kwa moja ya wazee wa Mbweni ambapo alipewa kipande kidogo kwa ajili ya kujenga hoteli ya kitalii lakini hata hivyo hakuendeleza na kubaki pori kwa muda mrefu

MJUMBE SERIKALI YA MTAA

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mbweni Maputo Costantine Malifa amekiri kuutambua mgogoro wa ardhi ya eneo hilo huku akifafanua wananchi hao wapo eneo hilo kwa zaidi ya miaka sita sasa ila kinachoshangaza ni idadi ya watu wanaofika eneo hilo na kudai ni mali yao.

Hata hivyo amesema kwa sasa amejitokeza mke wa Daud Balali aliyemtaja kwa jina la Anna Muganda ambaye anasema ni eneo lake na hivyo amewataka wananchi hao waondoke na tayari amepeleka kampuni ya udalali ya Suma JKT kwa ili wabomoe makazi ya watu."Eneo hilo lilikuwa pori la muda mrefu , hivyo wananchi zaidi ya 270 waliamua kwenda kuanzisha makazi yao kama ambavyo
mmeona.Leo hii anakuja mtu anasema ni eneo lake.Bila kujali ya uamuzi wa Mahakama Kuu anataka watu waondoke,"amesema.

Amefafanua wananchi hao wanachotaka ni kujua ukweli wa eneo hilo na kutaka isitambulike kuwa wamevamia bali waliamua kuweka makazi baada ya kuona eneo hilo haliendelezwi na kubaki pori ambalo lilikuwa linatishia usalama wa maisha ya watu huku akisisitiza Mahakama Kuu ikitoa hukumu ya kuwataka wananchi waondoke basi wataondoka na kama atatakiwa kupewa Muganda ambaye anatajwa kama mkewe marehemu Daud Balali basi atapewa.

DIWANI AVUNJA UKIMYA...ATOA UFAFANUZI

Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mbweni jijini Dar es salaam Hashim Mbonde amesema kuwa analifahamu vema eneo hilo na ukweli ni kwamba mmiliki halali ni Anna Muganda ambaye ni mkewe Daud Balali, hivyo wananchi hao wamevamia na ni vema wakaondoka.Amesema awali kuna wananchi walitoka eneo la Bunju na kuvamia eneo hilo ambao walikuwa 100 lakini yeye kama
kiongozi wa wananchi aliamua kuwaondoa lakini baadae wamekuja wengine na kuvamia eneo hilo lenye heka 12 na lina umiliki halali wa Muganda.

Amesema kutokana na Muganda kulimiliki kihalali alikwenda Manispaa ya Kinondoni kuomba kibali kwa ajili ya ujenzi na baada ya kutaka kuanza ujenzi wananchi hao waliamua kuwatimua, hivyo akalazimika kuomba ulinzi ambapo kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya."Nimekuwa diwani wa eneo hili kwa muda mrefu na mchakato wote wa ununuzi wa Balali eneo hilo nilikuwepo, hivyo naufahamu vema na unaponiuliza nani mmiliki halali jibu langu ni kwamba mkewe marehemu Daud Balali ndio mmiliki.Hivyo niwaombe wananchi waheshimu sheria na wapishe eneo hilo kwani si la kwao,"

Ametumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Maputo ambavyo wanapotosha ukweli wa eneo hilo na kuwataka kuwa wa kweli kwani mwenye eneo hilo ni Anna Muganda ambalo amelirithi kutoka kwa mumewe.Amefafanua kuwa yeye anamtambua mjane wa Daud Balali ambaye ni Anna Muganda kuwa ndio mwenye eneo hilo kwa kuwa na hati zote na hati yake ya umiliki haina shaka hata kidogo lakini kinachoshangaza wananchi hao ambao wamewaita wavamizi wanamzuia asifike kwenye eneo lake kwa ajili ya kuliendelea huku akisistiza umuhimu wa wananchi kufuata sheria.

Kuhusu haki za binadamu amesema wanatambua hilo na ndio maana wananchi walioko eneo hilo wamepewa notisi ya siku 14 ili waondoke kwa hiyari yao.

BARUA YA NOTISI YABANDIKWA MTAANI

Wakati hayo yakiendelea Kampuni ya Udalali ya Suma JKT nayo imefika eneo hilo na kisha kubandika barua ya notisi inayowataka wananchi walioko ndani ya eneo hilo waondoke.Hata hivyo Mjumbe wa Serikali ya Mtaa aligoma kuitambua barua hiyo ya notisi wala kwenda kuonesha eneo lenye mgogoro ambapo amesema hawezi kwenda kuonesha eneo bila ya kuona barua ya nakala ambayo
imetoka Mahakama Kuu kwani kesi bado iko mahakamani ya kutafuta uhalali wa nani mmiliki sahihi wa eneo hilo.

MJANE WA DAUD BALALI AOMBA ULINZI ....

Pamoja na yote hayo aliyekuwa mkewe Daud Balali Anna Muganda Julai 26 mwaka huu wa 2018 aliamua kuomba ulinzi katika mchakato wa kuwatoa wananchi hao ambao amewaita wavamizi wa eneo lake.Kupitia barua yake ya tarehe hiyo kwenda kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni amesema yeye Anna Muganda Balali mwenye eneo Mbweni Ploti namba 1007 Block B lenye
ukubwa wa wa 36,197 Sqm ambalo limepimwa na kupewa hati namba 155638.

Hata hivyo anasikitishwa na kutendo cha wananchi kuamia eneo hilo na kwenye barua hiyo anaonesha kuwa aliwahi kuomba ulinzi ili

aweze kuwaondoa wavamizi hao katika eneo hilo.
 Baadhi ya wananchi wa Mbweni Maputo jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye kikao cha kuangalia namna ya kuomba msaada wa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuingilia kati kwani kwa sasa wanaishi maisha ya hofu
 Mkazi wa Mtaa wa Mbweni Maputo jijini Dar es Salaam Raphael Joseph akizungumzia mgogoro wa eneo ambalo wao wameamua kufanya makazi baada ya mrefu kudai lilikuwa pori ambapo wanamuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati ili haki itendeke kwani kuna watu wanawatishia kuwaondoa  kwa nguvu
 Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mbweni Maputo Costantine Malifa akionesha barua ya kampuni ya udalali ya Sums JKT ambayo inawataka wananchi hao kuondoka ndani ya siku 14 kuanzia jana.Hata hivyo amekataa kuitambua hiyo kwa mdaia suala la eneo hilo liko mahakamani ,hivyo hawezi kutoa usharikiano kwenye jambo analoona linakwenda kinyume na sheria
 Diwani wa Kata ya Mbweni Hashimu Mbonde(kulia)akitoa ufafanuzi kuhusu eneo hilo ambalo amedai mmiliki halali ni Anna Muganda ambaye ni mke wa aliyekuwa Havana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Daud Balali ambaye kwa sasa ni marehemu
 Mkazi wa Mtaa wa Mbweni Maputo John Julius akitoa ufafanuzi namna ambavyo wamefika eneo hilo na kuweka makazi yao huku akiiomba Serikali kuingilia  kati eneo hilo ili haki ipatikane

 

No comments:

Post a Comment