Thursday, December 6, 2018

MBOWE , ESTER MATIKO 'MAMBO MAGUMU' , WARUDISHWA TENA MAHABUSU


*Kuna kila dalili Sikukuu ya Krismass, Mwaka mpya wakasheherekea wakiwa ndani

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

KESI ya tuhuma za uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko na wenzao saba inayounguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepigwa kalenda hadi Desemba 21 mwaka huu.

Aidha Mahakama hiyo imetoa ruhusa kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuendelea kuhudhuria michezo ya Afrika Mashariki nchini Burundi na pia imeruhusu Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, kumuuguza mkewe ambaye amejifungua kwa upasuaji hivi karibuni.

Mbowe na Matiko wataendelea kukaa mahabusu kwa muda usiojulikana pengine hadi mwakani, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusimamisha usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na washitakiwa hao kupinga maamuzi ya Mahakama ya Kisutu ya kuwafutia dhamana.

Hatua hiyo imetokana na upande wa Serikali kukata rufaa kupinga uamuzi ya Jaji Sam Rumanyika aliyesema kuwa rufaa ya kina Mbowe ipo mahakamani hapo kisheria na kwa maana hiyo, haina mamlaka ya kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Akitoa uamuzi huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Jaji Rumanyika alisema DPP anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo ambao haumalizi kesi chini ya kifungu cha sita cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa na kwamba kunapokuwepo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.

Mapema leo,Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi amedai mbele ya Hakimu Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba washitakiwa Mdee na Heche hawapo mahakamani.Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa Heche alitolewa 

taarifa kuhusu kufanyiwa upasuaji mdogo kwa mke wake lakini afya ya mtoto sio nzuri sana na kwa upande wa Mdee yupo nchini Burundi kushiriki mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki.Mdhamini wa Mdee, Fares Robinson aliieleza mahakama hiyo kuwa Mdee yupo safarini kwenda Burundi kwa safari za kibunge na kwamba Katibu wa Bunge aliandika barua kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama kumtaarifu kuwa mshitakiwa huyo atakuwa nje kwa shughuli za kibunge na kwamba atarudi Desemba 20, mwaka huu.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Nchimbi alidai walipokea hati ya wito ikiambatanishwa na maombi ya ruhusa ya kupitia Mdee kupitia kwa Katibu wa Bunge.Alidai kwa mantiki hiyo wanaona washitakiwa wanafuata taratibu na hawana pingamizi na hilo na kuhusu Heche anayemuuguza 

mkewe pia hawana pingamizi ikizingatiwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa.Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mashauri alisema kuwa walipokea barua kutoka kwa Katibu wa Bunge kuomba ruhusa ya Mdee kwenda Burundi kuhudhuria michezo ya EAC na kwamba pande zote za utetezi na mashitaka walikuwa Mahakama Kuu kwa kesi nyingine.

"Mahakama inamruhusu mshitakiwa kuhudhuria michezo na ruhusa ya Heche ya kumuuguza mkewe imekubaliwa lakini wazingatie kuwepo mahakamani siku ya kutajwa kesi hiyo Desemba 21, mwaka huu, " alisema Hakimu Mashauri.Muda wote wakati kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi ambapo uliwazuia baadhi ya wafuasi wa chama hicho kuingia mahakamani na badala yake waliwaruhusu viongozi wa chama hicho pekee.

Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu 
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment