Friday, December 14, 2018

MAWAKILI 800 WASHINDWA KUJIELEZA KWA LUGHA YA KINGEREZA, JAJI MKUU ATOA NENO

Karama Kenyunko, Globu ya jamii

 MAWAKILI zaidi ya 800 ambao wamehojiwa kuhusu masuala mbalimbali ya sheria wameshindwa kujieleza kwa lugha ya Kingereza kwa ufasaha.

Imeelezwa kuwa mawakili waliowengi bado wana changamoto licha ya sheria kutumia zaidi lugha ya Kingereza.

Hayo yamesemwa leo  na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma ameyasema hayo leo Desemba 14.2018 wakati wa hafla ya kuwakubali mawakili wapya 909 iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo.

Jaji Juma amesema, amegundua changamoto hiyo baada ya kupata nafasi ya kukutana ana kwa ana na waombaji wa uwakili wapatao 824 kwa mujibu wa kifungu 8 (3) cha Sheria ya Mawakili.

Miongoni mwa mawakili hao 909  waliokubaliwa kupata uwakili saba ni majaji, aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola na  Msajili wa Mahakama ya Rufani John Kahyoza.

Wengine ni  Balozi mstaafu na mwanadiplomasia  wa Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba, maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, mapadre, mashekhe na watu wengine.

Akizungumza wakati hafla hiyo, Jaji Juma amesema,  lengo la kuwahoji ni kutaka kujiridhisha na ufahamu na matumizi ya lugha ya Kiingereza kwa mambo yanayozunguka sheria kwa Tanzania na dunia.

"Changamoto ya kujieleza inatakiwa kufanyiwa kazi na mfumo wa elimu pamoja na Baraza la Sheria Tanzania chini ya Jaji Kiongozi.
"Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka Kiingereza ni 'Kiswahili cha Dunia'.

 Hivyo, kwa wakili anayetaka kujifunza na kujiendeleza katika ushindani wa karne ya 21, hawezi kukwepa umuhimu wa kuwa na ufasaha katika lugha ya hiyo," amefafanua Jaji Profesa Juma.

Ameeleza mawakili hao wanaweza kutoa huduma zenye ubora na ushindani kama watajisomea maeneo mapya na kujiendeleza kitaaluna kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Amesema katika kujiendeleza, mawakili hao wanapaswa kuelewa changamoto zinazoikabili nchi ya Tanzania na namna gani sheria unaweza kukabiliana na changamoto zilizipo.

Pia Jaji Juma amesisitiza kuwa mawakili wanapaswa kujitayarisha na mabadiliko ya sheria na kanuni za uendeshaji wa mashauri ziboreshwe na zieleweke kwa urahisi na ziharakishe utoaji wa haki.

Aidha amewataka mawakili hao kubaki ndani ya misingi ya maadili na uwakili bora kwa kuzingatia Kanuni za Kimaadili, 
"Wakili ni ofisa wa mahakama mwenye tabia njema isiyo na dosari, ukweli na kufanya kazi kwa kuheshimu misingi ya haki. Wakili anatakiwa kuheshimu wateja wake, wananchi na mawakili wenzake  pia kuheshimu wataalamu kutoka fani nyingine bila kusahau kuheshimu mahakama na mfumo wa sheria na utoaji haji," amesisitiza.

Pia amesema kanuni zimeainisha mifano ya wakili ambaye atachukuliwa kuwa amekosa uadilifu na tabia njema endapo atakiuka sheria za nchi, kuficha ukweli kwa wateja, matusina kutoa taarifa za uongo au maneno ya kudhalilisha maofisa mwengine wa mahakama.

Hata hivyo, amesema kanuni zimetoa mifano ya huduma mbovu zinazoweza kusababisha mawakili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kusimamishwa uwakili kama vile kushindwa kumpa mteja  taarifa muhimu za maswala yanayomuhusu, kushindwa kutoa taarifa kwa mteja zinapohitajika na kushindwa kutoa huduma kwa sababu ya ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

Pia amesema kutoa huduma mbovu kwa mfano ubovu wa hati za kimahakama kwa niaba ya mteja wake na kusababisha kuchelewa kwa shauri au kusababisha gharama zisizo za lazima dhidi ya mteja.

Jaji Profesa Juma alieleza sababu nyingine za zitakazosababisha mawakili kusimamishwa ni kutoa huduma mbovu, kutayarisha hati za kimahakama zisizoeleweka na makosa ya kiufundi katika hati za kimahakama.

"Kushindwa kuwa na ofisi ambazo wateja, mawakili wenzako na mahakama zinazoweza kukufikia na kuwasilisha taarifa. Hivi karibuni tutamtaka kila wakili ajisajili eneo ilipo ofisi yake, mtaa na postikodi ili aweze kufikiwa," ameongeza.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amesema mawakili wanatakiwa kuzingatia sheria kwa kutotenda makosa ya jinai, kuzingatia maslahi ya mteja dhisi ya maslahi hao binafsi na kuisaidia mahakama kupata haki.

Ameongeza, mawakili watakaochaguliwa kufanya kazi za utumishi wa umma wanapaswa kuchagua suala moja kwa sababu ni ukiukwaji wa maadili wakili kunufaika mara mbili.
Naye, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema, kazi ya mawakili ni kusaidia mahakama kupata haki na kwamba hakuna haki bila hekima.

No comments:

Post a Comment