Saturday, September 1, 2018

Matumizi ya ARV hupunguza maambukizi kwa mtu mwingine

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu  akiendelea na matembezi katika moja ya banda lililokuwa katika viwanja vya maji maji Songea mkoa wa Ruvuma wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha yangu Mkoa wa Ruvuma.

Na WAMJW-SONGEA,RUVUMA

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa mtu akitumia ARV kwa usahihi na kikamilifu anapunguza ewezekano wa kuambukiza VVU kwa mtu mwingine  kwa takribani Asilimia 60.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo wakati akizindua Kampeni ya FURAHA YANGU, PIMA, JITAMBUE, ISHI katika  viwanja vya Majimaji Songea Mkoa wa Ruvuma. 

“Kwa mujibu wa Wataalamu wa Afya ikiwemo Wanasayansi imedhihirika kwamba mtu akianza mapema kutumia Dawa anapunguza uwezekano wa kupata magonjwa nyemelezi, pia anaongeza muda wa kuishi na anapunguza uwezekano wa kuwaambukiza watu wengine”  alisema Waziri Ummy Mwalimu.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu aliselebuka na kikundi cha Bendi cha JKT Mlale wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha Yangu mkoa wa Ruvuma katika viwanja vya maji maji Songea.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa mtu akigundulika kuwa na maambukizi ya VVU na UKIMWI ataanzishiwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi mara moja badala ya kusubiri hali yake kuwa mbaya zaidi. 

Waziri Ummy alisema kuwa wakati Takwimu za Kitaifa zikionesha maambukizi ya VVU yamepungua kutoka Asilimia 5.7 hadi Asilimia 4.7, bado maambukizi mapya yameendelea kuwepo, takribani vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 sawa na Asilimia 40 wanaambukizwa VVU.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Asilimia 52 ya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wanajifahamu kuwa wana VVU,  katika kila watu 100 Watu 48 wenye maambukizi ya VVU hawajui kuwa wana VVU jambo ambalo ni hatari kwenye kaya zao na Taifa kwa ujumla .

Mbali ya yote Waziri Ummy aliwaagiza watoa huduma  kupitia Kampeni hiyo kwamba  watu wote wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU vizuri kwa kuzingatia masharti wapewe dawa za miezi mitatu badala ya mwezi mmoja kama inavyofanywa sasa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (wapili Kushoto) akiendelea na matembezi katika viwanja vya maji maji wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha yangu mkoa wa Ruvuma.Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi Christina Mndeme.

“Watu wote wanaotumia Dawa vizuri kwa kuzingatia masharti, wapewe dawa za miezi mitatu badala ya kila mwezi kwenda kuchukua dawa katika vituo vya kutoa huduma za afya, tunaamini kwamba hatua hii itachochea watu wengi zaidi kwenda kupima na kujiandikisha kupata huduma za dawa” alisema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy  amewaagiza Waganga Wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha kwamba  vituo vya Afya vyote nchi ambavyo vimesajiliwa na kutambulika na Wizara ya Afya  kutoa huduma za kupima VVU, kutoa ushauri nasaa na kutoa dawa

“Maelekezo ambayo tumetoa Serikali, hatuoni ni kwanini katika kila kituo cha Afya kisitoe huduma za kupima VVU, zakutoa Ushaurinasaa na kutoa huduma za dawa kama ameambukizwa” alisema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya maji maji katika kampeni ya Furaha yangu mkoa wa Ruvuma

Sambamba na hayo Waziri Ummy alisema kuwa  katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini Tanzania ,Watoto 11 walikuwa wanazaliwa na maambukizi ya VVU,  ndani ya mika miwili maambukizi ya VVU yamepungua kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hadi kuwa chini ya Asilimia 5 kutoka Asilimia 11.

Aliendelea kusema kuwa  katika kila watoto 11 wanaozaliwa na VVU ni takribani watoto 5 ndio wanazaliwa na maambukizi ya VVU, inawezekana kabisa kuwa na mtoto  asilimia 0 ambae anazaliwa na maambukizi ya VVU.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Mndeme alisema kuwa kwa upande wa 909090 hali ya hali ya Mkoa wa Ruvuma takwimu zinaonesha kuwa 90 ya kwanza imefikia Asilimia 71.3 sawa na watu 41,789 wanaokadiliwa kuishi na maambukizi ya VVU imefikiwa kati ya watu wanaokadiliwa 58,534 wanaishi na VVU katika MKoa wa Ruvuma, huku 90 ya pili Asilimia 78 ambayo ni sawa na watu 41,141 ya watu waliotambuliwa hali zao za maambukizi ya VVU na tayari wamekwisha anzishiwa dawa.

Aidha, Bi. Mndeme aliendelea kusema kuwa vituo vya kutolea huduma za upimaji wa VVU vimeongezeka mkoani Ruvuma kutoka vituo 240 kwa mwaka 2016 hadi kufikia vituo 293 kufikia mwezi juni 2018, Mkoa wa Ruvuma Tayari una vituo 303, huku vituo 293 vikiwa Tayari vimekwishafikiwa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akipata huduma ya kupima maambukizi ya VVU wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha yangu katika viwanja vya maji maji Songea mkoa wa Ruvuma.
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi Christina Mndeme akipata huduma ya kupima maambukizi ya VVU wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha yangu katika viwanja vya maji maji Songea mkoa wa Ruvuma.
Picha ya pamoja ikiongonzwa na Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Mndeme wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Furaha yangu mkoa wa Ruvuma katika viwanja vya maji maji Songea.

No comments:

Post a Comment