Thursday, June 28, 2018

TANZANIA NI KIMBILIO KWA WALIOKOSA AMANI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa tuzo ya Balozi wa Amani na Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Wabunge Wapenda Amani, Dk Thomas Walsh katika hafla ya kuzindua tawi la Tanzania la Wabunge wapenda amani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, jijini Dodoma Juni 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika hafla ya kuzindua tawi la Tanzania la Wabunge wapenda amani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, jijini Dodoma Juni 28, 2018
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipeana mkono na Mbunge wa Tabora Mussa Ntimizi katika hafla ya kuzindua tawi la Tanzania la Wabunge wapenda amani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, jijini Dodoma Juni 28, 2018 katikati ni Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Wabunge Wapenda Amani, Dk Thomas Walsh. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Wabunge Wapenda Amani, Dk Thomas Walsh, katika hafla ya kuzindua tawi la Tanzania la Wabunge wapenda amani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, jijini Dodoma Juni 28, 2018.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kunakolifanya Taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na kimbilio la wale waliovurugikiwa na amani katika nchi zao. 

Kadhalika, uwepo wa amani nchini si tu unatoa fursa ya kutekeleza majukumu ya kiuchumi na kijamii bila hofu bali pia ni sababu muhimu ya wenzetu wengine kutoka nje kuona fursa ya kuwekeza na kushirikiana nasi katika kujenga maendeleo ya nchini. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 28, 2018) wakati akizindua Umoja wa Kimataifa wa Wabunge Wapenda Amani tawi la Tanzania (IAPP), kwenye mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa Bungeni, jijini Dodoma.

Amesema amani na utulivu ni tunu kubwa sana katika jamii yoyote ile Duniani na Tanzania muda wote imeendelea kuenzi tunu hiyo iliyojengwa kwenye misingi imara kupitia waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Shirikisho la Amani kwa Wote (Universal Peace Federation (UPF), ambalo lilianzishwa kwa lengo la kumkomboa binadamu kutoka katika udhalili wa kukosa mahitaji muhimu. 

“Hili linadhihirika kupitia mipango ya shirikisho hilo ya kushirikiana na jamii nyingine katika kuimarisha sekta zenye kugusa maisha ya watu wengi kama vile kilimo, mazingira, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mipango hiyo utategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu katika jamii husika, ambapo amewahakikishia kwamba Serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana nao katika nyanja hizo za kijamii na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda maslahi ya pande zote mbili na kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nitoe rai kwa Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika kwamba hakikisheni mnaanzisha mazungumzo na wawakilishi wa UFP nchini kwa lengo la kuona namna nzuri ya kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia shirikisho hilo hususan katika sekta za kilimo, elimu, afya, mazingira na miundombinu,” amesema. 

Awali, Mwenyekiti Mwanzilishi wa IAPP, Bw. Mussa Ntimizi amesema Shirikisho la Amani kwa Wote litasaidia nchi kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo kama ya kilimo, afya kwa sababu hakuwezi kuwa na amani bila maendeleo.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. William Ngeleja amesema Shirikisho la Amani kwa wote limetenga dola bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya katika nchi 10 za Bara la Afrika na Tanzania ikiwemo.

Katika hafla hiyo Waziri Mkuu amepewa tuzo ya Balozi wa Amani na Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh. Viongozi wengine walipewa tuzo hiyo ni pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo,Bw. William Ngeleja Katibu Msaidizi wa umoja huo Bibi Anna Lupembe, Mweka hazina Bibi Ritta Kabati.

Baada ya kukabidhi tuzo hizo, Dkt. Walsh shirikisho lao linahitaji kufanya kazi nna Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia kwa ajili ya kuboresha maendeleo na amani. Amesema katika Taifa kukiwa na maendeleo amani lazima itakuwepo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh, Katibu wa Shirikisho la Amani kwa Wote Kanda ya Afrika (UPF_Afrika), Bw. Adama Doumbia, Katibu wa Shirikisho la Amani kwa Wote Tanzania (UPF_Tanzania), Bw Stylos Simbamwene, 


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 28, 2018.

No comments:

Post a Comment