Tuesday, June 5, 2018

MAPACHA WALIOUNGANA MARIA NA CONCOSALATA KUZIKWA KATIKA KABURI MOJA

*Tayari maandalizi ya jeneza la kipekee na kaburi kubwa yakamilika, kaburi lao kuzungukwa na makaburi ya mapadre, masista

 Na Ripota Wetu,Iringa

Tayari Maandalizi ya kuipumzisha Miili ya mapachaa hao yamekamilika baada ya jeneza la kipekee na kaburi kubwa lililochimbwa katika makaburi wanayozikwa masista na mapadre pamoja na viongozi wa kanisa Katoliki, Tosamaganga kukamilika. 

Maria na Consolata wanazikwa kesho baada ya ukamilisho wa ibada ya kuwaaga itakayofanyika kwenye viwanja vya Rucu kabla ya kuanza msafara wa kuelekea Tosamaganga watakakozikwa. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Shule ya Seminari ndogo ya Tosamaganga Padre Benedict Chavala amesema uamuzi wa mapacha hao kuzikwa Tosamaganga, kutawasaidia kuendelee kuwaombea. Awali kulikuwa na msuguano wa eneo watakalozikwa mapacha hao uliohitimishwa na Mkuu wa Masista wa Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi kudai walichagua kuzikwa wanakozikwa viongozi wa kanisa hilo. 

Msuguano huo pia ulitokana na hatua bibi wa marehemu upande mama yake, kudai miili hiyo isafirishwe kwa ajili ya maziko Bukoba jirani na alipozikwa marehemu mama yao. Alipoulizwa endapo kama itatokea wakasema miili hiyo izikwe Bukoba wakati tayari Iringa wameshachimba kaburi Padre Chavala alisema kuwa itategemea watu hawa wana hoja nzito kiasi gani. 

“Muda mwingi wamechukuliwa ni watoto wetu nahivyo tunapenda watuelewe kwamba tangu mwanzo kama kanisa liliamua kuwachukua kutokana na mazingira waliokuwa nayo na kuwalea tunasikia ni wanetu na kama ni wanetu basi tubaki nao hapa ambapo wapo mama na bibi zao ambao ni masista ili tuweze kuwakumbuka muda wote.”alisema Padre Chavala na kuongeza: 

“Wanaendelea kuwa karibu nasi kuliko kupelekwa huko hata pengine hawajawahi kufika,kila mmoja atawashangaa inakuwaje hawa watu wanakuja wakiwa wamefariki wakati wakiwa wazima hawajawahi kufika,na kilio ni kilio,msiba ni msiba wakubali tu wazikwe hapa ni pazuri zaidi hata wao wenyewe waje tulie pamoja.”alisema Padre Chavala 

Alisema masista walio walea kwa muda mrefu tayari ni wazee kuwapeleka hukombali hao masista watajisikia wapweke zaidi kwa sababu wameachana na wapendwa wao halafu kuwapeleka mbali ambapo wao hawawaoni. “Jambo lote hili lina uzito wake,kule nako wakipelekwa kuna uzito wake lakini hapa pia pana uzito zaidi.”alisema Padre Chavala 

Chavala akizungumzia utofauti wa kaburi la maria na Consolata alisema kuwa wanaweka pana kwasababu wapo watu wawili,lazima ukubwa wake utofautiane na kaburi linalozikwa mtu mmojammoja. “Wapo watu wawili,tumeamua kuwaweka mahali pamoja lakini upekee wa kaburi ni kwamba watu hawa tunaendelea kuwalea katika vituo vyetu,ni wenzetu,tunawaweka hapa ambapo wanalala Masista,Mapadre,Mabrother na hata walei sasa hawa wamepata upekee sana kwa sababu wamebaki wakilelewa na masista.”alisema Chavala 

Naye sista Calista Ludega ambaye ni mkuu wa shirika la mtakatifu Theresa wa mototo Yesu jimbo katoliki la Iringa alisema kuwa wanawazika Maria na Consolata mahala wanapolala masista wa consolata kwa ajili ya kuwaenzi masista wa mishionari wa consolata kwa kuwa wao wamechukuwa sehemu kubwa ya malezi tangu walipozaliwa watoto hao hadi wanapomaliza maisha yao hapa duniani. 

Maria na Consolata wanazungukwa na makaburi ya masista ambao walikwisha fariki Maraia Lorenta,Masweta Pagosi na Maria Saglio. Maria na Consolata walifariki dunia June 2 mwaka huu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa ambapo walikuwa wakipatiwa matibabu. 

Vifo vya mapacha hao vimeleta simanzi na huzuni kubwa kwa Watanzania walio wengi akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk.John Pombe Magufuli ambapo baada ya kupata taarifa za vifo hivyo alisema na hapa namkunukuu “Nimesikitishwa na kifo cha maria na Consolata .Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa.Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa .Poleni familia , masista wa maria Consolata na wote walioguswa , pumzikeni mahali pema wanangu .Bwana alitoa na bwana ametwaaa.Jina la bwana lihimidiwe.
 Baadhi ya Ndugu na Jamaa wakishiriki kuchimba kaburi ambalo Mapacha walioungana Maria na Consolata wanatarajiwa kuzikwa hapo kesho 
 Sehemu ya Makaburi yaliyolizunguka kaburi la Mapacha walioungana ,Marehemu Maria na Consolata,ambapo Masista na Mapadre wamezikwa
 Baadhi ya Ndugu na Jamaa wakiendelea kushiriki kuchimba kaburi ambalo Mapacha walioungana,Marehemu Maria na Consolata wanatarajiwa kuzikwa hapo kesho .


Zoezi la uchimbaji wa kaburi kwa ajili ya maziko ya mapacha walioungana, marehemu Maria na Consolata linaendelea katika Makaburi ya Masista wa Shirika la Bikira Maria wa Consolata Tosamaganga,  Jimbo Katoliki la Iringa.

No comments:

Post a Comment