Monday, May 7, 2018

MKURUGENZI MTENDAJI TIC:UKUAJI WA KASI WA UCHUMI WA TANZANIA KIVUTIO KWA WAWEKEZAJI

*Azungumzia miradi mipya 109 waliyoisajili kwa kipindi cha miezi minne,fursa za ajira

Na Said Mwishehe,Globu

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe ametoa hakikisho kwa wawekezaji na Watanzania kwa ujumla kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa na kwa sasa nchi yetu inashika nafasi ya tano kati ya mataifa 10 duniani ambayo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Amesema kuimarika kwa uchumi huo wa Tanzania na kukuwa kwa kasi, maana yake inatoa usalama kwa anayetaka kuwekeza nchini kuwa na uhakika wa mtaji wake huku akielezea mafanikio ya TIC katika kuhamasisha uwekezaji nchini ambapo kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu wamefanikisha kuandikisha miradi mipya 109 inayotarajia kutoa fursa ya ajira 18,172.

Mwambe amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anatoa mafanikio ya TIC kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu ambapo amefafanua kutokana na matokeo hayo ya haraka ya ukuaji wa uchumi yametokana na jitihada za Serikali  chini ya Rais Dk.John Magufuli katika kupambana na rushwa , kuondoa urasimu kwa kutengeneza mazingira wezeshi ya usajili wa biashara na leseni kwa wawekezaji wa nfani na nje.

Akifafanua zaidi mambo mengine ambayo yamefanyika katika kuwahudumia wawekezaji kwa haraka ni pamoja na kuboresha mfumo wa huduma mahala pamoja ndani ya TIC ambapo kwa sasa kuna maofisa zaidi  10 wanaotoka kwenye wizara,idara na taasisi za Serikali kwa ajili ya kutoa huduma za kusajili kampuni.

Pia usaidizi wa kupata ardhi ya uwekezaji ,leseni mbalimbali ,kusajili VAT ,TIN na ushauri wa kitaalam kuhusu kodi,vivutio vya uwekezaji , vibali vya kazi na kutathimini masuala ya mazingira.Mwambe amesema kituo kimefanikisha uanzishaji wa kamati ya Taifa ya huduma kwa wawekezaji  ili kujadili mikakati ya kutatua changamoto za uwekezaji kabla na baada ya uwekezaji.

Kuhusu maeneo ambayo uwekezaji unafanyika zaidi ni sekta ya ujenzi, uzalishaji viwandani , usafirishaji wa mizigo, kilimo na miundombinu na kati ya miradi  mipya 109 , miradi 28 ambayo sawa na asilimia 34.86 inamilikiwa na wageni , miradi mitatu  ni ya ubia na miradi 68 inamilikiwa na Watanzania.

Akizungumzia uchumi wa Tanzania , Mwambe amesema  kituo kinawajibika kuishauri Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ambapo kulingana na na takwimu za Benki ya Rand Merchant (RMB) zilizotolewa  mwaka 2015 ,Tanzania inashika nafasi ya 9 kati ya nchi 10 za  Afrika zenye ushawishi wa kumvutia mwekezaji .

Pia amesema kwa ujumla uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi kubwa ambapo kwa sasa nchi inashika nafasi hiyo ya tano  na kwa mujibu wa Taasisi ya utafiti ya the Centre for International Development (CID) ya Chuo Kikuu cha Havard ni kwamba Tanzania inatarajia kuwa nchi ya nne duniani na ya tatu kwa Afrika katika ukuaji wa uchumi wake.Mwambe amesema katika kipindi cha mwaka 2016 Tanzania iliendelea kubaki nafasi ya 9 kabla ya kupanda hasi nafasi ya saba mwaka 2017 kati ya nchi 10 za Afrika zenye ushawishi wa kumvutia mwekezaji  kuwekeza.

"Kwa kiasi kikubwa matokeo ya ukuaji wa kasi ya uchumi imekuwa sababu kubwa ya kuvutia wawekezaji kuwekeza.Amani na utulivu wa nchi yetu nayo imekuwa chachu ya nchi yetu kuwa kimbilio la uwekezaji na jukumu letu TIC ni kuhamasisha uwekezaji, hivyo tutaendelea kuifanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake,"amefafanua Mwambe.

Pia amesema katika kufanikisha mambo yake TIC imetumia njia mbalimbali kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi kama sehemu bora ya kuwekeza.Ametaja njia hizo ni pamoja na kushiriki makongamano ya biashara nje na kupokea ujumbe wa wafanyabishara na wawakilishi wa Serikali kutoka nje.

Mwambe ametoa shukrani kwa viongozi wa ngazi mbalimbali za wilaya mpaka Taifa kwa juhudi zinazofanyika katika kufanikisha uwekezaji nchini huku akitoa mwito kwa wakuu wa mikoa ,wilaya na watendaji wa taasisi  zote za Serikali  kuongeza kasi za uboreshaji  wa huduma zao kwa wawekezaji.

"Juhudi hizi  zikifanyika kwa nguvu na kasi kubwa kwa pamoja basi Tazania chini ya Rais Magufuli  itaendelea kupaa, kuvutia uwekezaji , kuibua fursa za ajira kwa vijana, kupanua wigo wa walipa kodi na hatimaye kuongeza uzalishaji  na kufikia uchumi wa kati,"amesema Mwambe.

No comments:

Post a Comment