Friday, March 23, 2018

HOSPITALI DAR ZABAINIKA KUWA NA WAGONJWA WENGI WALIOKUFA KWA VIFO VYA MALARIA, UKIMWI


Mganga Mkuu wa Serikali, Prof Muhammad Bakari Kambi akizungumza wakati akifungua mdaharo uliowahusisha wataalamu mbali mbali kujadili ni kitu gani kinasababisha vifo katika hospitali, kufuatia utafiti uliofanywa na  Taasisi ya Taifa Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMRI). Kupitia matokeo ili kutoa ushauri wa kisera ili serikali iweze kutilia mkazo ambapo Prof. Kambi amesema changamoto inazikumba hospitali nyingi ni magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni changamoto kubwa inayopelekea kuzigharimu sana. Kaimu Mkurugenzi wa NIMRI akimkaribisha mgeni rasmi. 
 Washiriki kutoka taasisi mbali mbali za serikali na hospitali za mikoa wakifuatilia kwa makini.
 Mgeni rasmi akiwa na Washiriki kutoka taasisi mbali mbali za serikali na hospitali za mikoa.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG. 

 HOSPITALI za Mkoa wa Dar es Salaam zimebainika zilikuwa na wagonjwa wengi ambao walikufa kutokana na malaria, Ukimwi , ajali, maambukizi ya bakteria kwenye damu, upungufu wa damu, saratani na kifua kikuu(TB) ukifuatiwa na mkoa wa Morogoro. Imefahamika malaria na upungufu wa damu ulichangia vifo vingi kwenye kundi la watoto chini ya miaka mitano na vifo kutokana na Ukimwi na Kifua Kikuu viliathiri zaidi kundi la watu wazima, vifo vinavyotokana na ajali viliathiri zaidi kundi kubwa la vijana wakati saratani ziliathiri makundi ya umri wote. 

 Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR) wakati ikielezea matokeo ya utafiti wa vifoo vinavyotokea katika hospitali za Tanzania. Imeelezwa na NIMR taarifa za vifo ni moja ya vyanzo muhimu vya takwimu katika kupanga mipango na kuandaa sera ya afya ambapo uchambuzi wa takwimu katika makundi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na kundi la ajali na majeraha ulionesha tofati kubwa kati ya mikoa na mikoa. 

 Utafiti huo umebaini mikoa ya Pwani, Geita na Katavi imeonekana kuathirika zaidi na magonjwa ya kuambukiza na utapia mlo. Wakati vifo kutokana na ajali na majeraha viliathiri zaidi mikoa ya Rukwa, Tabora, Singida na Kigoma. Kundi la magonjwa yasiyoambukiza limeathiri zaidi mikoa ya Ruvuma, Manyara, Dar es Salaam na Mwanza.

 "Kati ya mwaka 2006 na mwaka 2015, mikoa ya Kanda ya Kati (Dodoma, Singida, Manyara) mikoa ya kaskazini (Arusha na Kilimanjaro) ndiyo iliyobeba mzigo mkubwa wa vifo vilivyosababishwa na maradhi ya mifumo ya kupumua, upungufu wa damu uliathiri zaidi mikoa ya Dodoma, Simiyu na Mtwara,"imesema. Imeeleza utafiti umeanisha changamoto katika ukusanyaji, uchanganuzi na matumizi ya takwimu katika hospitali zilizopo nchini na kumekuwa na matumizi hafifu ya majina rasmi ya magonjwa kwa kutumia mwongozo wa kimataifa. 

 "Vyanzo vikuu vya vifo hospitalini nchini Tanzania ni pamoja na malaria, maradhi yanayoathiri mfumo wa kupumua, Ukimwi, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo. "Kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya watoto wachanga na magonjwa ya mfumo wa kupumua katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. 

 Mapendekezo ya utafiti huo Serikali kuandaa mwongozo thabiti wa ukusanyaji, matumizi, utunzaji na uhifadhi bora ya takwimu za afya,"amesema NIMR. Pia pendekezo lingine ni kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika uchanganuzi na matumizi ya takwimu, kuimarisha mfumo wa takwimu wa kielektroniki na kuimarisha mafunzo ya madaktari katika utumiaji wa mwongozo wa kimataifa wa kuainisha vyazo rasmi vya maradhi na vya vifo. Imefafanua zaidi kuhusu utafiti huo amesema kuanisha vyanzo vya vifo katika hospitali zetu ni muhimu kufuatilia matukio ya vifo, kutathimini ubora wa huduma zinazotolewa na kuanisha vipaumbele katika huduma za afya.

 "Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuanisha matukio ya vifo katika hospitali za Tanzania ili kutambua maradhi yanayoathiri jamii yetu. Utafiti pia ulichunguza uwepo,upatikanaji, utunzaji na ubora wa takwimu za vifo hospitalini,"imeongeza. Kuhusu mbinu za utafiti huo, inaeleza ulifanyika kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2016 na ulihusisha hospitali 39. Hospitali hizo ni pamoja na hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa, Hospital Maalum na hospitali za Wilaya.

 "Taarifa za vifo vilivyotokea kuanzia mwaka 2006 had mwaka 2015 zilikusanywa.Takwimu hizo zilipatikana kutoka kwenye rejesta za hospitali na vibali vya mazishi kutoka kwa Wakala wa Vizazi na Vifo katika ofisi za Wilaya. "Taarifa zilizokusanywa zilihusu jinsia ya mgonjwa, tarehe ya kulazwa hospitali, tarehe ya kufariki na sababu za kifo. Vyanzo vya vifo viliwekwa katika makundi 45 kulingana na utaratibu wa makundi ya magonjwa wa Shirika la Afya Duniani,"imesema. 

 Kuhusu matokeo, amesema jumla ya hospitali 39 zilishiriki katika utafiti huu. Kwa ujumla kulikuwa na ugumu katika upatikanaji wa takwimu na utunzaji wa takwimu katika hospitali nyingi ulikuwa una mapungufu makubwa. "Baadhi ya takwimu hazikupatikana katika baadhi ya hospitali au katika baadhi ya miaka.Utunzaji wa takwimu ulikuwa mzuri kiasi katika hospitali za rufaa za kanda kuliko za mikoa na wilaya.

 "Matumizi ya majina ya magonjwa kwa kufuata mwongozo wa kimataifa yalikuwa hafifu. Baadhi ya dalili za ugonjwa ziliandikwa kama ndiyo sababu za kifo. Jumla ya vifo 247,976 vilitolewa taarifa katika kipindi cha miaka 10 (2006-2015). Kulikuwa na tofauti kubwa katika idadi ya vifo kati ya jinsia ya kiume na ya kike,"imesema NIMR wakati inaelezea utafiti huo.

No comments:

Post a Comment