Thursday, January 4, 2018

WAZIRI MWIJAGE: NJIA NZURI YA KUFIKIA UCHUMI WA KATI NI UCHUMI WA VIWANDA


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akifungua Ofisi ya Muda ya Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) iliyoko Mtaa wa Malambo mjini Bariadi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu. 

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe..Charles Mwijage akizungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Ziara yake Mkoani humo 
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage(kulia) akisaini Kitabu cha wageni katika Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika hapo wakati wa ziara yake Mkoani humo (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka. 
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akizungumza na wadau mara baada ya kutembelea eneo itakapojengwa Ofisi Mpya ya SIDO Isanga Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. 

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wadau wa viwanda Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake mkoani humo.




Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema njia nzuri ya kufikia Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 ni kupitia Uchumi wa Viwanda jumuishi.

Waziri Mwijage ameyasema hayo alipozungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake Mkoani humo, ambapo alisisitiza juu ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ulio imara, shindani na endelevu, utakayozingatia mambo muhimu matatu ambayo ni soko, malighafi na teknolojia.

Amesema lengo la Serikali ni kuhamasisha ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Jumuishi ambao unawahusisha watu wengi kupitia viwanda vidogo na vya kati,vitakavyotumia malighafi zitakozozalishwa hapa nchini vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwepo mkoa wa Simiyu ambao umeonekana kufanya vizuri katika eneo hilo.

“Safari ya Simiyu imeanza vizuri na lengo la safari ni kuhamasisha Watanzania kujenga uchumi wa viwanda jumuishi, viwanda ambayo malighafi yake inazalishwa na wananchi wenyewe, vitatoa ajira kwa wananchi walio wengi, vitatumia malighafi asilia na kutoa mazao yenye matumizi makubwa” alisema Mwijage.

Waziri Mwijage amepongeza juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Simiyu katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kupitia Falsafa ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo sasa umejipanga kuelekea kwenye “Kijiji Kimoja Bidhaa Moja”.

Ameongeza kuwa mwaka 2018/2019 Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) litawasaidia wananchi kupata mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji na uchakataji, ambapo ameuhakikishia Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Ujenzi wa Ofisi ya SIDO ya Mkoa huo eneo la Isanga Mjini Bariadi utakamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka 2018, kwa kuwa fedha za ujenzi zipo.

Sanjali na hilo Waziri Mwijage amewataka Maafisa Ushirika kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kukopeshwa mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo na Serikali pamoja na Taasisi nyingine za Kifedha kwa kuwa ni rahisi zaidi vikudi kufikiwa kuliko mtu mmoja mmoja.

Wakati huo huo Mwijage amewataka watendaji wote wa Serikali kuondoa vikwazo na kuacha urasimu unaoweza kuwakwamisha wawekezaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuweza kuufikia Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Akiwasilisha tarifa ya Mkoa, Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amesema ili kuandaa mazingira mazuri yatakayowawezesha wawekezaji kuvutiwa na kuwekeza mkoani humo, wametenga maeneo ya uwekezaji na madawati ya uwekezaji kwa kila Halmashauri na timu mahsusi ya Mkoa ya kuanzisha na kuendeleza dhana ya Simiyu ya Viwanda inayoongozwa na Katibu Tawala Mkoa.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, Njalu Silanga amesema wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kwa vitendo katika Ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati na akaomba Meneja wa SIDO Mkoa atembelee viwanda vilivyopo ili aweze kutoa ushauri juu kuboresha uendeshaji wa viwanda hivyo katika tija.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema kupitia SIDO mkoa huo unaweza kufikia Uchumi wa Kati. “Tungehitaji kuwa ni Mkoa ambao value addition(kuongeza thamani) itafanyika kupitia SIDO, mahali ambapo mtu mwenye milioni tatu wakiungana kikundi cha walima alizeti wanaprocess(wanachaka) wenyewe mafuta” alisema Mtaka.

Pamoja na kuzungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu, Waziri Mwijage alifungua Jengo la muda la Ofisi ya SIDO Mkoa wa Simiyu lililopo Mtaa wa Malambo Mjini Bariadi na kukagua eneo la ujenzi wa Ofisi mpya ya SIDO itakayojengwa na SUMA JKT, ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment