Thursday, January 4, 2018

WANANCHI WAFURIKA USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA MKOANI RUVUMA


Wananchi wakazi wa Kata ya Ndilima Mtaa wa Makambi Ndilima Wilaya ya Songea, wakikagua fomu zao kabla ya kwenda kwenye maalumu cha uchukuaji taarifa kwa maana ya kupigwa picha, uchuaji alama za kibaiolojia na saini ya Kielekrtoniki. Waliopo pichani ni Bi. Hadija Yahaya (mwenye gauni la Pinki kushoto) na Bwana Hussein Nyoni (Mwenye kofia kichwani) wote wakazi wa Mtaa wa Makambi Songea. 
Hawa ni baadhi tu ya wakazi wa Kata ya Ndilima Wilaya ya Songea wakisubiri huduma ya Usajili Vitambulisho vya Taifa unaoendelea kwenye shule ya msingi ya Matogo na kuhusisha wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Kwa Wilaya ya Songea Kata zilizoanza zoezi ni Kata ya Ndilima na Seed-farm zoezi ambalo litafanyika wa siku saba tu kabla ya kuhamia Kata zingine za Wilaya hiyio.

Akionekana mwenye furaha ni Bi Haruna Thabiti Majwila wa Mtaa wa Makambi Ndilima mara baada ya kukamilisha hatua za usajili kwa maana kupigwa picha na kuchukuliwa alama za Kibaiolojia. Na hapa ya akiangalia muonekano wa Kitambulisho chake utakavyokua na kukagua picha yake kujiridhisha endapo picha yake imetoka vizuri. Kulia ni Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Bwana Agaton Magnus Komba. 
Pichani ni Bwana Hausi Rashid Mamba akiweka saini yake ya Kielektroniki kwenye mashine maalumu ya uchukuaji alama za kibaiolojia( alama za vidole), picha na saini ya kielektroniki wakati wa zoezi la Usajili wananchi Vitambulisho vya Taifa linaloendelea katika Kata ya Ndilima wilaya ya Songea mkoani Ruvuma. 
Bwana Michael Komba akikagua kwa makini (aliyevaa jezi) akikagua kwa makini taarifa zake zilizojazwa kwenye fomu ya maombi ya usajili kabda la kuingia kwenye chumba cha Usajili Vitambulisho vya Taifa. Zoezi la Usajili Mkoa wa Ruvuma limeanza rasmi tangu tarehe 02/02/2018 na linahusisha wananchi wote wa mkoa huo wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.


Mamia ya Wananchi wa Wilaya za mkoa wa Ruvuma wamejitokeza kwa wingi kwenye vituo vya Usajili zoezi la Vitambulisho vya Taifa huku baadhi wakiwataka viongozi kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali la usajili Vitambulisho vya Taifa kuwa ni bure.

Wito huo umetolewa na wananchi wa Wilaya ya Songea wakidai kutozwa kiasi cha shs.2000/ za picha za kubandika kwenye kwenye fomu za utambulisho za Serikali za Mitaa wanakoishi na kudai gharama hizo ni kubwa kulinganisha na hali halisi ya maisha.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Makambi Bwana Anuari Methodi Nyoni ametolea ufafanuzi suala hilo na kueleza wananchi wanaoagizwa kuleta picha picha ndogo za passport size ni wale ambao wamekosa viambatisho muhimu vya kuwatambulisha na hivyo ili kujiridhisha kuwa mwananchi wanayemthibitisha kuwa ni mkazi wa eneo lao basi ni vema kuwa na picha yenye taswira yake ili kuepuka matumizi mabaya ya fomu za kuwatambulisha zinazotolewa na Serikali ya Mtaa.

Aidha amesisitiza Serikali yake ya Mtaa kusimamia na kutekeleza agizo la Serikali la kwamba zoezi la Vitambulisho vya Taifa ni bure na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa Serikali inaposema zoezi ni bure haina maana kwamba Serikali itafanya kila kitu; ikutolee copy viambatisho vyako au kukulipia gharama za picha hilo haliwezekani. Amesema wao kama wasimamizi wa zoezi hilo wanasisitiza mwananchi kufika kwenye kituo na picha yake au nakala ya viambatisho vyake na huduma nyingine zote mwananchi atazifuata mtaani zinazkotolewa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati Bi. Rose Joseph amesema Mamlaka ina mashine zake za kuwapiga picha wananchi na kwamba mwananchi anayefika kusajiliwa hapaswi kuja na picha ya passport size kama inavyoelezwa; ila changamoto kubwa ni kwa wale wananchi ambao hawana viambatisho vyovyote vya kuwatambulisha na wanahitaji kupata barua ya utambulisho wa Serikali za Mitaa wanakoishi. Hawa sasa kwa utaratibu waliojiwekea wenyewe barua za utambulisho zinazotoka kwenye Serikali za Mitaa na kugongwa muhuri wa Mtendaji au Mwenyekiti wa Mtaa wamekuwa na utaratibu wa kuweka picha ya mwananchi ili kujiridhisha na yule wanayemtambulisha kwetu.

Bi Rose amewasisitiza wananchi kujitahidi kuwa na viambatisho muhimu vinavyowatambulisha kuepukana na gharama zizisokuwa za lazima kwani mwananchi anayekuja kusajiliwa akiwa na cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule, Kadi ya kupigia kura, TIN namba, Leseni ya Udereva, Pasi ya kusafiria(Passport), Kadi ya Bima ya AFYA, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii au Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi; vichache kati ya hivyo huyu mtu hahitaji barua ya utambulisho ya Serikali ya Mtaa kwani viambatisho vyake vinatosha kumtambulisha” alisisitiza

Amesema ni vema wafanyabiashara kutotumia Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kama sehemu ya kujinufaisha na badala yake kutambua si wananchi wote wenye uwezo wa kulipa gharama za huduma wanazotoa na kuomba Mamlaka mbalimbali za Serikali kuangalia namna zinavyoweza kudhibiti changamoto hiyo ili wananchi wengi wajitokeze kwenye zoezi la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwani zoezi hilo ni bure nala muhimu kwa kila mwananchi kushiriki.

Zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa limeanza mkoani Ruvuma kwa Wilaya za Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru na linatazamiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa tatu mwaka huu.

No comments:

Post a Comment