Friday, December 29, 2017

UHAMIAJI TANGA YAWAONYA VIONGOZI WA VITONGOJI NA VIJIJI VILIVYOPO MIPAKANI WANAOUZA ARDHI KWA WAGENI


VIONGOZI wa Vitongoji na Vijiji vilivyopo kwenye mipaka mkoani Tanga wameonywa kuacha tabia ya kuuza ardhi kwa wageni wanaofika kwenye maeneo yao badala yake hakikishe wanatoa taarifa wanapowaona watu wasiowajua ili kuweza kukomesha vitendo vya wahamiaji haramu.


Hayo yalisemwa na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga Crispian Ngony’ani wakati akizungumza na vyombo habari ambapo alisema viongozi hao wamekuwa ni tatizo kubwa badala ya kukemea vitendo vya wahamiaji haramu lakini wamekuwa wakiwakumbatia kwa kuwapatia ardhi jambo ambalo ni kosa kisheria.

Alisema utafiti walioufanya mpakani mwa Kenya na Tanzania Horohoro wamebaini idadi kubwa ya wakenywa wameuziwa ardhi katika maeneo hayo na wanaishi nchini kinyume cha sheria huku akiwataka viongozi hao kuachana na vitendo hivyo kabla hawajakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya dola.

“Tatizo kubwa viongozi wa vitongoji na vijiji badala ya kumemea uuzaji wa ardhi kinyemele hivyo napenda kutoa onyo kwao kuacha tabia hiyo kwani sisi kama idara ya uhamiaji tupo macho kuhakikisha wale wote wanaohusika na vitendo hivyo tunawachukulia hatua “Alisema.

Alisema viongozi hao badala ya kukemea uzaji wa haramu ardhi kwa wageni wao wamekuwa mstari wa mbele kuwakarabisha kwenye maeneo hayo bila kutambua kufanya hivyo ni makosa kisheria hivyo kuwaonya kuacha vitendo vya namna hiyo mara moja.

“Pindi wanapomuona mgeni au raia anauza ardhi watoe taarifa kwenye vyombo vinavyo husika ikiwemo idara ya uhamiaji tukishirikiana kwa mtindi huo tutaweza  kukomesha vitendo vya watu kuvamia ardhi yetu na kuishi kinyume cha sheria tu “Alisema Ofisa Uhamiaji huyo.

Wakati huo huo,Ofisa Uhamiaji huo alisema katika kipindi cha mwaka 2017 wamekamatwa watanzania 61 kwa kuvunja sheria za uhamiaji ambapo kosa kubwa ni kushiriki vitendo viovu vya kuwasafirisha wahamiaji hao katika maeneo mbalimbali na kuwaingiza nchini.

Alisema hasa wahamiaji ambao ni raia kutoka nchini Ethiophia
wanaonekana wana biashara kubwa sana kwa baadhi ya watu mkoani Tanga kwa kwenda nchini Kenya  kuwachukua kwa kufanya udalali na kuwapitisha kwenye njia za panya hadi kwenye maeneo wanayotaka kufika.

Aidha alisema kutokana na hali hiyo idara hiyo imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha wanakomesha vitendo vya namna hiyo kwa kuongeza udhibiti wa watu wanaoingia nchini kwa kushirikiana na vyombo vya vyengine vya dola.


Hata hivyo alisema katika kipindi hicho kesi 28 zimefunguliwa ambazo zilikuwa zinawahusu watanzania na zilizokuwa zikiendelea ni 10,nne zilikwisha,mbili zilifutwa na moja iko kwa wakili wa serikali na nyengine moja ipo uhamiaji.(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)

No comments:

Post a Comment