Friday, December 29, 2017

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA ‘DOLA’ KUANZIA JANUARI 1 MWAKA 2018

* WATALII KURUHUSIWA KWA KIBALI MAALUMU


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 ambapo alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata wanaowalazimisha watanzania kufanya malipo kwa Dola badala ya Shilingi, mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.


Na Said Mwishehe,Blogu ya  Jamii
SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni ikiwamo ‘dola’ kuanzia Januari 1 mwaka 2018, na kueleza bei zote za huduma na bidhaa zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango wakati anaelezea mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Dk.Mpango kabla ya kutoa agizo hilo,amefafanua suala la matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania nchini linasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa fedha za kigeni ya mwaka 1992, sheria ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT) ya mwaka 2006, na tamko la Serikali ya mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.

Amesema matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania wakati wa kufanya miamala mbalimbali yanaweza kuwa na athari kiuchumi ikiwa pamoja na kudhoofisha thamani ya shilingi.

“Sheria iliyopo kwa sasa haikatazi jambo hili bali inasisitiza sarafu ya Tanzania ndio fedha halali na mtu au taasisi yoyote itakayekataa kuupokea malipo ya shilingi yetu tutachukua hatua za kisheria.

“Hata hivyo suala hili limeendelea kuwa kero kwa wananchi kutokana na ugumu wa kusimamia matakwa ya sheria.Inafahamika kuwa baadhi ya wateja wanapewa kiwango cha thamani  ya kubadilisha fedha ambacho kiko juu kuliko thamani halisi iliyoko kwenye soko,”amesema.

Ameongeza hali hiyo inaumiza zaidi mteja husika. Hivyo suala hilo linahitaji kufanyiwa marekebisho ya sheria.”Ili kukabiliana na hali kero kama hizo wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea ,Serikali inaagiza yafuatayo kuaniza Januari 1,mwaka 2018.”
Kwa mujibu wa Dk.Mpango maagizo hayo ni bei zote nchini kutangazwa kwa Shilingi.Bei hizo zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi.

Pia bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kieletroniki.

Amesema vyombo vya dola vihakikishe vinasimamia maagizo hayo na watakaoendelea kutoza huduma na bidhaa kwa fedha za kigeni wachukuliwe hatua.

Ameongeza kwa bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

“Bei hizo zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nje ya nchi kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nje ya nchi, gharama za viwanja ndege na visa kwa wageni.

“Na gharama za hotelikwa watalii kutoka nje ya nchi.Hata hivyo walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi ya kusafiria na nyaraka za usajili kwa kampuni.

“Viwango vya kubadilisha fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katikka sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko.

“Ifahamike kuwa ni benki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa  kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni kupanga viwango vya kubadilisha fedha, amesema Dk.Mpango.

Ametumia nafasi hiyo kueleza mkazi yoyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni na vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo hayo ya Serikali.

No comments:

Post a Comment