Monday, September 4, 2017

Waziri Mkuu awapongeza NSSF, PPF na magereza mradi wa kiwanda cha sukari cha Mbigiri mkoani Morogoro

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepongeza hatua ya mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda huku akitoa wito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaonyesha uzalendo kwa kujitolea kwa vitendo kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kutatua tatizo la ajira na kuinua uchumi wa taifa.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro mara tu baada ya kuongoza zoezi la upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara alipotembelea shamba la kubwa la miwa linaloandaliwa ikiwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro.

"Pamoja na kutoa pongezi kwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa kuitikia vema wito wa serikali ya awamu ya tano katika uwekezaji wa viwanda vyenye tija kwa taifa, kipekee nitoe wito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaunga mkono jitahada hizi kwa kujitolea ujuzi na maarifa katika kufanikisha adhma hii ya serikali inayolenga kuwanasua kutoka kwenye uhaba wa ajira,'' alitoa wito.

Wito huo wa Waziri Mkuu ulikuja kufuatia kuguswa na uzalendo ulioonyeshwa na vijana wasomi sita kutoka mikoa mbalimbali walioamua kuweka kambi kwenye eneo hilo Mbigiri wakilala chini ya miti lengo likiwa ni kuunga mkono jitiahada za ujenzi wa kiwanda hicho kwa kushiriki bila malipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwanda hicho ikiwemo kubuni mchoro uliotumika katika moja ya jengo litakalotumika kujengwa kiwanda.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio wakati wa ziara hiyo.

"Vijana hawa ambao kwa sasa wamepatiwa maturubai ya kujihifadhi wamekuwa mfano wa kuigwa na wenzao nchi nzima na nitazifikisha salamu zao kwa muheshimiwa Rais ajue jitiahada zake zinatafsiriwa vyema sana na vijana wazalendo wa taifa hili,'' alisisitiza.

Akizungumzia mradi huo Waziri Mkuu alisema pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa sukari hapa nchini, pia utapunguza tatizo la ajira sambamba na kukuza uchumi wa nchi. 

Ili kuhakikisha wananchi wanakuwa kwenye nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuzalisha malighafi kwa ajili ya kiwanda hicho Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa mkoa huo kuhakakikisha wanapita wilaya nzima ya Kilosa unapotekelezwa mradi huo kuhakikisha hakuna mashamba pori zoezi litakaloambatana na unyang'anyaji wa mashamba yasiyoendelezwa kutoka kwa wamiliki wake na kisha kukabidhiwa kwa wananchi wayatumie kwa kilimo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) pamoja na Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama (katikati) wakiongoza zoezi la upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro. Kulia, akishirikiana nao ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe.

"Na kwa wale wananchi wanaolima kwenye eneo la magereza utumike utaratibu mzuri waweze kupata mashamba kwenye eneo la magereza waendelee na kilimo hiki cha miwa ili kulisha kiwanda licha ya kuwa umiliki wa ardhi utabaki kuwa ni wa jeshi la magereza,'' alifafanua.

Mradi huo unaolenga kuzalisha tani 50 za sukari kwa mwaka ni sehemu ya mradi mkubwa unaotekelezwa na mifuko hiyo katika eneo la Ngerengere, Wilaya ya Morogoro Vijijini unaofahamika kama Mkulazi I ambao unaolenga kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka sambamba na kutoa ajira zaidi ya 100,000 katika hatua ya awali.

Kwa upande wake Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama  alisema mifuko ya Hifadhi ya Jamii hapa nchini kwa sasa inatekeleza miradi ya viwanda ipatayo 28 ambayo ipo katika hatua mbalimbali kiutekelezaji lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kuwekeza katika uchumi wa viwanda.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (alieshika jembe) akiongoza zoezi la upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro. Miongoni mwa wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Phillip Mpango (alievaa suti nyeupe).

Akionyesha kuguswa na ushiriki wa wananchi katika mradi huo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Phillip Mpango alimuahidi Waziri Mkuu kuwa anakwenda kutoa maelekezo kwa Benki ya Kilimo nchini kuhakikisha inafika maeneo yote ya mradi huo ili kuangalia namna benki hiyo inavyoweza kuwasaidia wananchi kushiriki kikamilifu katika kilimo cha miwa.

Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji , Charles Mwijage alisema lengo la serikali ni kuhakikisha taifa linazalisha sukari tani milioni mbili ili lijitosheleze na kuunza nje ya nchi ambapo kwa sasa licha ya mahitaji ya sukari kuwa ni tani 600,000 taifa linazalisha takribani laki tatu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio, walihakikishia serikali, wananchama na wadau wote wa mifuko hiyo kuwa utekelezaji wa mpango huo pamoja na mambo mengine unalenga kuongeza ajira na kupunguza kabisa kasi ya mfumuko wa bei kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (mwenye miwani) akisikiliza kwa umakini maelezo kuhusu ubunifu wa michoro ya miradi mbalimbali kutoka kwa vijana wasomi sita kutoka mikoa mbalimbali walioamua kuweka kambi kwenye eneo hilo Mbigiri wakilala chini ya miti lengo likiwa ni kuunga mkono jitiahada za ujenzi wa kiwanda hicho kwa kushiriki bila malipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwanda hicho ikiwemo kubuni mchoro uliotumika katika moja ya jengo litakalotumika kujengwa kiwanda.

"Tayari mkandarasi wa kufunga kiwanda hiki ameshapatikana wakati zoezi la upandaji wa miwa likiendelea. Lengo ni kupanda ekari 3000  za miwa ifikapo Disemba mwaka huu zoezi ambalo tayari limetoa ajira zaidi 150 kwa wakazi jirani na eneo hili la Mbigiri na wengine kutoka mikoa jirani,'' alisema Prof Kahyarara huku akiongeza mkuwa mradi huo pia utazalisha umeme Megawatt 8 .

Naye Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa alisema ufufuaji wa kiwanda hicho kilichosimamisha uzalishaji wake katikati ya miaka 1990 mbali na kuwa mchango mkubwa kwa jeshi hilo pia utatoa fursa kwa wafungwa watakaoonyesha uwezo mkubwa katika utekelezaji wa mradi kuweza kupewa nafasi ya kutumikia kiwanda hicho hata baada ya kumaliza vifungo vyao.

" Kabla hakijasimamisha uzalishaji wake kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo uduni wa teknolojia na ukosefu wa vipuri kiwanda hiki kilikuwa kinazalisha tani 8 hadi 10 za sukari kwa mwaka sasa kinakwenda kuzalisha tani zipatazo 50 kwa kipindi hicho...kiukweli tunawashukuru sana NSSF, PPF na serikali ya awamu ya tano,'' alipongeza.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifuatilia kwa umakini maelezo kutoka kwa meneja wa shamba hilo namna ambavyo miwa inapandwa kitalaam. Wengine ni pamoja na Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama (kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe (mwenye suti nyeusi).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akimshudia Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango akishiriki kwenye zoezi hilo.
Kisha kazi ikaendelea…! Lengo ni kupanda ekari 3000 za miwa ifikapo Disemba mwaka huu zoezi ambalo tayari limetoa ajira zaidi 150 kwa wakazi jirani na eneo hili la Mbigiri na wengine kutoka mikoa jirani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine walipata fursa ya kusherehekea na wenyeji kupitia ngoma za asili.

No comments:

Post a Comment