Friday, June 9, 2017

SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA (NIC) IMETOA GAWIWO LA SHILINGI BILIONI 1.7 KWA SERIKALI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Bw. Sam Kamanga, akizungumza jambo wakati wa tukio la Shirika hilo kukabidhi gawiwo kwa Serikali, kiasi cha Sh. Bil. 1.7, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha, mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, katika hafla ya makabidhiano ya gawiwo la Sh. Bil.1.7 liyofanyika mjini Dodoma.
Viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakishiriki tukio la Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuikabidhi Serikali gawiwo la Sh. Bil. 1.7 baada ya Shirika hilo kufanya vizuri kibiashara katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, tukio lililofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, mjini Dodom
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Doroth Mwanyika, akifurahia jambo wakati wa tukio la Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuikabidhi Serikali gawiwo la Sh. Bil. 1.7 baada ya Shirika hilo kupata faida katika mwaka wa fedha 2016/2017
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akisisitiza jambo wakati wa tukio la Shirika la Bima la Taifa (NIC) kukabidhi Serikalini gawiwo la Sh. bil. 1.7, baada ya Shirika hilo kupata faida kibiashara katika mwaka wa Fedha 2016/2017, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Mjini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akitoa neno la Shukrani kwa uongozi Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa ubunifu na uwajibikaji wao ulioliwezesha Shirika hilo kupata faida na kutoa gawiwo kwa Serikali, Mjini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

……………………….

Na Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma

SERIKALI imeendelea kupata neema kutokana na uwekezaji wake kwenye mashirika na taasisi mbalimbali yanayojiendesha kibiashara nchini ambapo leo Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa gawiwo la Shilingi bilioni 1.707 baada ya kupata faida kiabishara mwaka 2016/2017.

Kwa nyakati tofauti mwaka huu, Serikali ilipokea kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kufuatiwa na NMB Bank Plc, iliyotoa kiasi cha Shilingi bilioni 16.5 hivi karibuni.

Akipokea Hundi kifani ya kiasi hicho cha Shilingi 1.707 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa, Bw. Sam Kamanga, Waziri wa Fedha na Mipango, amelipongeza shirika hilo kwa kuonesha maendeleo makubwa katika kipindi kifupi tangu azindue Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo mwishoni mwa mwaka uliopita.

“Nilipozindua Bodi yenu ya Wakurugenzi uliniahidi Mkurugenzi Mtendaji kuwa mtafanyakazi kwa bidii na kuanza kutoa gawiwo Serikalini, ninajisikia furaha sana kwa niaba ya watanzania kuona kuwa mnatimiza ahadi hiyo kwa kutoa asilimia 15 ya pato ghafi la mapato yenu. Nawapongezeni sana” alisisitiza Dkt. Mpango.

Alizitaka taasisi nyingine za umma zilizochini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina zinazofikia 260 kuanza kutumia huduma za bima kupitia Shirika la Bima la Taifa.

Alisema anafahamu kwamba kuna taasisi nyingine zina mikataba na mashirika mengine ya bima lakini akatoa wito kwa taasisi hizo kwamba baada ya kumaliza mikataba yao, waanze kupata huduma kupitia NIC ambalo manufaa yake yameanza kuonekana baada ya kuanza kurejesha sehemu ya faida yake kwa Serikali.

Hata hivyo Dkt. Mpango aliitaka NIC lisibweteke badala yake liboreshe huduma zake ili kuweza kujiongezea soko kwani mashirika ya bima yamekuwa na ushindani mkubwa.

Alilitaka Shirika hilo kutoa elimu kwa Umma wakiwemo wakulima, wafugaji na wananchi wengine kuhusu umuhimu wa kukatia bima mifugo, mazao, nyumba na vyombo vya moto ili kujiepusha na hasara zinazoweza kutokea wakati wa majanga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwa Shirika hilo kutoa gawiwo kwa Serikali tangu lianzishwe miaka 54 iliyopita na kuzitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara kuiga mfano wa NIC.

“Naamini leo ndiyo mmezaliwa na mna miaka mingine 100 mbele ya kutenda kwa ajili ya watanzania” Alisisitiza Dkt. KIjaji

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Dotto James alilipongeza Shirika hilo na kusisitiza kuwa Wizara ipo bega kwa bega kushirikiana nao ili kuhakikisha Shirika hilo linapiga hatua zaidi kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi kifani, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzihamasisha Taasisi za Umma kukata bima NIC, na kwamba hatua hiyo ndiyo imeliwezesha shirika kutengeneza faida na kutoa gawiwo kwa Serikali.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuyahamasisha mashirika zaidi ya 200 yaliyochini ya Msajili wa Hazina kutumia huduma za Taasisi yake ili kuongeza wigo wa mapato na kuleta faida zaidi kwa wabia wa Shirika hilo

“Ni Taasisi 15 tu ndizo zilizoitikia wito wa Serikali wa kutumia huduma za bima kupitia NIC lakini mashirika na taasisi nyingine bado hivyo ninaiomba Serikali itusaidie kufanikisha jambo hili” Alisistiza Bw. Kamanga.

Aliiahidi Serikali kwamba Shirika lake linatarajia kuongeza gawiwo zaidi za kiasi hicho kilichotolewa kutokana na mikakati kabambe ya kiabiashara waliyojiwekea.

No comments:

Post a Comment