Monday, May 29, 2017

WANANCHI WILAYANI MBOGWE MKOANI GEITA WAPOKEA KWA KISHINDO ZOEZI LA USAJILI WA VYETI VYA KUZALIWA KWA WATOTO WENYE UMRI CHINI YA MIAKA MITANO

Kata ya Iponya Wilayani Mbogwe,mkoani Geita,imevuka lengo la uandikishaji watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa ajili ya kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kwa zaidi ya watoto 900 sawa na 154.7%

Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa zoezi la usajili wa watoto chini ya umri wa  miaka mitano wa wilaya ya Mbogwe,Fredrick Chotamasege, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya uandikishaji kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe aliyefanya ziara ya ufuatiliaji katika kata ya Iponya.

“Kata ya Iponya imefanikiwa kuvuka lengo katika zoezi la uandikishaji watoto chini ya umri wa miaka mitano zoezi linaoendeshwa na wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA). Kata ya Iponya iliwekewa lengo la kuandikisha watoto 1,806 lakini hadi kufikia tarehe 16/05/2017 ilikuwa imeandikisha watoto 2,794” alisema Fredrick. Aliongeza kuwa usajili huo ni sawa na ongezeko la watoto 988 waliosajiliwa sawa na 54.7%.

Pamoja na mafanikio makubwa ya zoezi hilo,zipo changamoto za mawasiliano ya mtandao wa Tigo unaotumika kutuma takwimu hizo. Aliongeza kuwa mtandao huo umekuwa ukitumia muda mrefu kutuma majina na hivyo kusababisha kuwa na takwimu tofauti kati ya zile zilizopo kwenye vitabu na zile za kwenye mtandao wa RITA.

Haya yalielezwa wakati Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Elias Kayandabila, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya zoezi la uandikishaji watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika kata za Masumbwe na Iponya wilayani Mbogwe.

Hata hivyo, baada ya Mkurugenzi Bw. Kayandabila kuridhika na hatua za uandikishaji aliwaagiza waratibu wa zoezi hilo kwenye kata kufanya ukaguzi wa vitabu (physical verification) ili kupata takwimu halisi kama alivyoshiriki yeye mwenyewe kwenye kata ya Iponya na Masumbwe ,ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tatizo la kimtandao.

Bw.Kayandabila alisisitiza kuwa “ Mbogwe ni miongoni mwa wilaya zenye mwingiliano wa watu na nchi jirani, hivyo amewaagiza waratibu wa zoezi kuorodhesha watoto wote ambao wanakuja bila kadi ya kliniki au tangazo la kuzaliwa ili waweze kufuatiliwa na kujiridhisha kama kweli wamezaliwa hapa nchini licha ya kupata barua za utambulisho kutoka serikali ya kijiji.

Mkurugenzi amewasihi wazazi wa watoto kuwa na makubaliano ya majina kabla hawajaenda kwenye vituo vya kusajilia ili kupunguza changamoto iliyojitokeza kwa baadhi ya wazazi kutoelewana juu ya majina ya watoto na hivyo kusababisha kuharibika kwa vyeti .

No comments:

Post a Comment